Mwanzo 15
15
Agano la Mwenyezi Mungu na Abramu
1Baada ya jambo hili, neno la Mwenyezi Mungu likamjia Abramu katika maono, akaambiwa:
“Usiogope, Abramu.
Mimi ni ngao yako,
na thawabu yako kubwa sana.”
2Lakini Abramu akasema, “Ee Bwana Mungu Mwenyezi, utanipa nini na mimi sina mtoto, na atakayerithi nyumba yangu ni huyu Eliezeri Mdameski?” 3Abramu akasema, “Hukunipa watoto, hivyo mtumishi katika nyumba yangu ndiye atakuwa mrithi wangu.”
4Ndipo neno la Mwenyezi Mungu lilipomjia, likanena: “Mtu huyu hatakuwa mrithi wako, bali mwana atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi.” 5Akamtoa nje na kusema, “Tazama juu mbinguni na uhesabu nyota, kama hakika utaweza kuzihesabu.” Ndipo akamwambia, “Hivyo ndivyo uzao wako utakavyokuwa.”
6Abramu akamwamini Mwenyezi Mungu, naye kwake jambo hili likahesabiwa kuwa haki.
7Pia akamwambia, “Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, niliyekutoa Uru ya Wakaldayo nikupe nchi hii uimiliki.”
8Lakini Abramu akasema, “Ee Bwana Mungu Mwenyezi, nitawezaje kujua kwamba nitaimiliki?”
9Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia, “Niletee ndama jike, mbuzi, na kondoo dume, kila mmoja wa miaka mitatu, pamoja na hua na kinda la njiwa.”
10Abramu akamletea hivi vyote, akampasua kila mnyama vipande viwili, akavipanga kila kimoja kuelekea mwenzake, lakini hata hivyo ndege hakuwapasua vipande viwili. 11Kisha ndege walao nyama wakatua juu ya mizoga, lakini Abramu akawafukuza.
12Jua lilipokuwa linatua, Abramu akashikwa na usingizi mzito, na giza nene na la kutisha likaja juu yake. 13Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia, “Ujue hakika kwamba wazao wako watakuwa wageni katika nchi isiyo yao, nao watafanywa watumwa na kuteswa kwa miaka mia nne. 14Lakini nitaliadhibu taifa lile watakalolitumikia kama watumwa, na baadaye watatoka huko na mali nyingi. 15Wewe hata hivyo utaenda kwa baba zako kwa amani, na kuzikwa katika uzee mwema. 16Katika kizazi cha nne wazao wako watarudi hapa, kwa maana uovu wa Waamori bado haujafikia kipimo.”
17Jua lilipokuwa limezama na giza limeingia, tanuru la moshi na mwali wa moto unaowaka vikatokea na kupita kati ya vile vipande vya nyama. 18Siku hiyo Mwenyezi Mungu akafanya agano na Abramu, na kumwambia, “Nitawapa wazao wako nchi hii, kuanzia Kijito cha Misri#15:18 Kijito cha Misri ina maana Wadi-el-Arish kwenye mpaka wa kusini wa Yuda. hadi mto ule mkubwa, Frati: 19yaani nchi ya Wakeni, Wakenizi, Wakadmoni, 20Wahiti, Waperizi, Warefai, 21Waamori, Wakanaani, Wagirgashi na Wayebusi.”
Aktualisht i përzgjedhur:
Mwanzo 15: NENO
Thekso
Ndaje
Copy
A doni që theksimet tuaja të jenë të ruajtura në të gjitha pajisjet që keni? Regjistrohu ose hyr
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.