YouVersion logo
Dugme za pretraživanje

Yohana 12

12
Mariamu ampaka Isa mafuta huko Bethania
(Mathayo 26:6-13; Marko 14:3-9; Luka 7:35-38)
1Siku sita kabla ya Pasaka, Isa alienda Bethania, makao ya Lazaro, aliyekuwa amemfufua kutoka kwa wafu. 2Wakaandaa karamu kwa heshima ya Isa. Martha akawahudumia, wakati Lazaro alikuwa miongoni mwa waliokaa mezani pamoja na Isa. 3Kisha Mariamu akachukua chupa ya painti moja#12:3 painti moja ni kama nusu lita yenye manukato ya nardo#12:3 aina ya mafuta yaliyokuwa yanatengenezwa kutokana na mimea yenye mizizi inayotoa harufu nzuri safi ya thamani kubwa, akayamimina miguuni mwa Isa na kuifuta kwa nywele zake. Nyumba nzima ikajaa harufu nzuri ya manukato.
4Ndipo Yuda Iskariote mwana wa Simoni, mmoja wa wanafunzi wa Isa, ambaye baadaye angemsaliti Isa, akasema, 5“Kwa nini manukato haya hayakuuzwa kwa dinari mia tatu#12:5 Dinari 300 ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku 300., na fedha hizo wakapewa maskini?” 6Yuda hakusema hivi kwa kuwa aliwajali maskini, bali kwa kuwa alikuwa mwizi; ndiye alikuwa akitunza mfuko wa fedha, na akawa akiiba zile fedha.
7Isa akasema, “Mwacheni. Aliyanunua manukato hayo ili ayaweke kwa ajili ya siku ya maziko yangu. 8Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote.”
Njama ya kumuua Lazaro
9Umati mkubwa wa Wayahudi walipojua kwamba Isa alikuwa huko Bethania, walikuja si tu kwa ajili ya Isa, lakini pia kumwona Lazaro ambaye Isa alikuwa amemfufua. 10Kwa hiyo viongozi wa makuhani wakapanga njama ya kumuua Lazaro pia, 11kwa kuwa kutokana na habari za kufufuliwa kwake, Wayahudi wengi walikuwa wanamfuata Isa na kumwamini.
Isa aingia Yerusalemu kwa shangwe
(Mathayo 21:1-11; Marko 1:1-11; Luka 19:28-40)
12Siku iliyofuata umati mkubwa wa watu waliokuwa wamekuja kwenye Sikukuu walisikia kwamba Isa angekuja Yerusalemu. 13Basi wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki, huku wakipaza sauti wakisema,
“Hosana!”#12:13 Kiebrania kusema Okoa; basi likawa neno la shangwe.
“Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Mwenyezi Mungu!”#12:13 Zaburi 118:25, 26
“Amebarikiwa mfalme wa Israeli!”
14Isa akamkuta mwana-punda, akampanda, kama ilivyoandikwa,
15“Usiogope, ewe Binti Sayuni;
tazama, mfalme wako anakuja,
amepanda mwana-punda!”#12:15 Zekaria 9:9
16Wanafunzi wake Isa mwanzoni hawakuelewa mambo haya. Lakini Isa alipotukuzwa, ndipo walipokumbuka kuwa mambo haya yalikuwa yameandikwa kwa ajili yake na alitendewa yeye.
17Wale waliokuwepo Isa alipomwita Lazaro kutoka kaburini na kumfufua kutoka kwa wafu waliendelea kushuhudia. 18Na kwa sababu walikuwa wamesikia kwamba alikuwa ametenda muujiza huu, umati wa watu wakaenda kumlaki. 19Hivyo Mafarisayo#12:19 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. walipoona hayo, wakaambiana, “Mnaona, hamwezi kufanya lolote. Angalieni, ulimwengu wote unamfuata yeye!”
Isa atabiri kifo chake
20Basi palikuwa Wayunani fulani miongoni mwa wale waliokuwa wameenda kuabudu wakati wa Sikukuu. 21Hawa wakaenda kwa Filipo, aliyekuwa raia wa Bethsaida huko Galilaya, wakiwa na ombi. Wakamwambia, “Tungependa kumwona Isa.” 22Filipo akaenda akamweleza Andrea, nao wote wawili wakamwambia Isa.
23Isa akawajibu, “Saa imewadia ya Mwana wa Adamu kutukuzwa. 24Amin, amin nawaambia, mbegu ya ngano isipoanguka ardhini na kufa, hubakia kama mbegu peke yake. Lakini ikifa, huzaa mbegu nyingi. 25Mtu yeyote anayependa maisha yake atayapoteza, naye ayachukiaye maisha yake katika ulimwengu huu atayaokoa hata kwa uzima wa milele. 26Mtu yeyote akinitumikia lazima anifuate, nami mahali nilipo ndipo mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu akinitumikia, Baba yangu atamheshimu.
27“Sasa roho yangu imefadhaika sana. Niseme nini? ‘Baba, niokoe katika saa hii’? Lakini ni kwa kusudi hili nimeufikia wakati huu. 28Baba, litukuze jina lako.”
Ndipo ikaja sauti kutoka mbinguni, ikasema, “Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.” 29Umati ule wa watu waliokuwa mahali pale waliisikia ile sauti, nao wakasema hiyo ilikuwa sauti ya radi; wengine wakasema malaika ameongea naye.
30Isa akawaambia, “Sauti hii imesikika kwa faida yenu, wala si kwa faida yangu. 31Sasa ni saa ya hukumu kwa ajili ya ulimwengu huu, sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje. 32Lakini mimi, nikiinuliwa kutoka nchi, nitawavuta watu wote waje kwangu.” 33Isa aliyasema haya akionesha ni kifo gani atakachokufa.
34Umati ule wa watu wakapaza sauti, wakasema, “Tumesikia kutoka Torati kwamba Al-Masihi#12:34 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta. adumu milele; hivyo wewe wawezaje kusema, ‘Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu’? Huyu ‘Mwana wa Adamu’ ni nani?”
35Ndipo Isa akawaambia, “Bado kitambo kidogo nuru ingali pamoja nanyi. Nendeni maadamu mna nuru, msije mkakumbwa na giza. Mtu anayetembea gizani hajui anakoenda. 36Wekeni tumaini lenu katika nuru hiyo ili mpate kuwa wana wa nuru.” Baada ya kusema haya, Isa aliondoka, akajificha wasimwone.
Wayahudi waendelea kutokuamini
37Hata baada ya Isa kufanya miujiza hii yote mbele yao, bado hawakumwamini. 38Hili lilikuwa ili kutimiza lile neno la nabii Isaya lililosema:
“Mwenyezi Mungu, ni nani aliyeamini ujumbe wetu,
na mkono wa Mwenyezi Mungu umefunuliwa kwa nani?”#12:38 Isaya 53:1
39Kwa hivyo hawakuamini, kwa sababu Isaya anasema mahali pengine:
40“Amewafanya vipofu,
na kuifanya mioyo yao kuwa migumu,
ili wasiweze kuona kwa macho yao,
wala kuelewa kwa mioyo yao,
wasije wakageuka nami nikawaponya.”#12:40 Isaya 6:10
41Isaya alisema haya alipoona utukufu wa Isa na kunena habari zake.
42Lakini wengi miongoni mwa viongozi wa Wayahudi walimwamini, lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakukiri waziwazi kwa maana waliogopa kufukuzwa katika masinagogi.#12:42 Nyumba za ibada na mafunzo. 43Wao walipenda sifa za wanadamu kuliko sifa zinazotoka kwa Mungu.
Amwaminiye Isa hatabaki gizani
44Isa akapaza sauti akasema, “Yeyote aniaminiye, haniamini mimi peke yangu, bali pia yeye aliyenituma. 45Yeyote anionaye mimi amemwona yeye aliyenituma. 46Mimi nimekuja kama nuru ulimwenguni, ili kila mtu aniaminiye asibaki gizani.
47“Mimi simhukumu mtu yeyote anayesikia maneno yangu na asiyatii, kwa maana sikuja kuuhukumu ulimwengu, bali kuuokoa. 48Yuko anayehukumu yule anayenikataa mimi na kuyakataa maneno yangu; yale maneno niliyoyasema yenyewe yatamhukumu siku ya mwisho. 49Kwa maana sisemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba aliyenituma aliniamuru ni nini cha kusema na jinsi ya kukisema. 50Nami ninajua amri zake huongoza hadi kwenye uzima wa milele. Hivyo lolote nisemalo, ndilo lile Baba aliloniambia niseme.”

Trenutno izabrano:

Yohana 12: NENO

Istaknuto

Podijeli

Kopiraj

None

Želiš li da tvoje istaknuto bude sačuvano na svim tvojim uređajima? Kreiraj nalog ili se prijavi