1 Nyakati 17
17
Ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa Daudi
(2 Samweli 7:1-17)
1Baada ya Daudi kuingia rasmi katika jumba lake la kifalme, akamwambia nabii Nathani, “Hebu tazama, mimi ninakaa kwenye nyumba nzuri iliyojengwa kwa mwerezi, wakati Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu liko ndani ya hema.”
2Nathani akamjibu Daudi, “Lolote ulilo nalo moyoni mwako litende, kwa maana Mungu yu pamoja nawe.”
3Usiku ule neno la Mungu likamjia Nathani, kusema:
4“Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Wewe hutanijengea mimi nyumba ili nikae humo. 5Mimi sijakaa ndani ya nyumba tangu siku niliyowatoa Israeli kutoka Misri hadi leo. Nimehama kutoka hema moja hadi jingine, na kutoka mahali pamoja hadi pengine. 6Popote nilipoenda pamoja na Waisraeli wote, je, kuna wakati nilimuuliza kiongozi yeyote niliyemwagiza kuwachunga watu wangu, “Kwa nini hujanijengea nyumba ya mwerezi?” ’
7“Sasa basi, mwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: Nilikutoa malishoni na kutoka kulisha mifugo, ili uwaongoze watu wangu Israeli. 8Nimekuwa pamoja nawe popote ulipoenda, nami nimekuondolea mbali adui zako wote mbele yako. Basi nitalifanya jina lako kuwa kuu kama majina ya watu walio wakuu sana duniani. 9Nami nitawapatia watu wangu Israeli mahali na nitawapa ili wawe na mahali pao wenyewe pa kuishi na wasisumbuliwe tena. Watu waovu hawatawatesa tena, kama walivyofanya mwanzoni, 10na ambavyo wamefanya siku zote tangu nilipowachagua viongozi kwa ajili ya watu wangu Israeli. Pia nitawatiisha adui zenu wote.
“ ‘Pamoja na hayo ninakuambia kwamba Mwenyezi Mungu atakujengea nyumba: 11Siku zako zikiisha, nawe ukaenda kulala na baba zako, nitamwinua mzao wako kuwa mfalme baada yako, mmoja wa wana wako mwenyewe, nami nitauimarisha ufalme wake. 12Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili yangu, nami nitakiimarisha kiti cha ufalme wake milele. 13Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Kamwe sitaondoa upendo wangu kwake, kama nilivyouondoa kwa yule aliyekutangulia. 14Nitamweka juu ya nyumba yangu na ufalme wangu milele; kiti chake cha utawala nitakiimarisha milele.’ ”
15Nathani akamwarifu Daudi maneno yote ya maono haya.
Maombi ya Daudi
(2 Samweli 7:18-29)
16Ndipo Mfalme Daudi akaingia ndani, akaketi mbele za Mwenyezi Mungu, akasema:
“Mimi ni nani, Ee Bwana Mwenyezi Mungu, na jamaa yangu ni nini, hata umenileta hadi hapa? 17Kana kwamba hili halitoshi machoni pako, Ee Mungu, umenena pia kuhusu siku zijazo za nyumba ya mtumishi wako. Umeniangalia kama mtu aliyetukuka kuliko watu wote, Ee Bwana Mwenyezi Mungu.
18“Daudi aweza kukuambia nini zaidi kuhusu kumheshimu mtumishi wako? Kwa maana wewe unamjua mtumishi wako, 19Ee Mwenyezi Mungu. Kwa ajili ya mtumishi wako, tena sawasawa na mapenzi yako, umefanya jambo hili kuu na kujulisha ahadi hizi zote zilizo kuu sana.
20“Hakuna aliye kama wewe, Ee Mwenyezi Mungu, wala hakuna Mungu ila wewe, kama vile tulivyosikia kwa masikio yetu wenyewe. 21Naye ni nani aliye kama watu wako Israeli: taifa pekee duniani ambalo Mungu wake alitoka kwenda kulikomboa kwa ajili yake mwenyewe, na kujifanyia jina kwa ajili yake mwenyewe, na kufanya maajabu makubwa na ya kutisha, kwa kuwafukuza mataifa mbele ya watu wako, ambao uliwakomboa kutoka Misri? 22Uliwafanya watu wako Israeli kuwa watu wako wewe mwenyewe milele, nawe, Ee Mwenyezi Mungu, umekuwa Mungu wao.
23“Basi sasa, Ee Mwenyezi Mungu, ahadi uliyoweka kuhusu mtumishi wako na nyumba yake, na uithibitishe milele. Fanya kama ulivyoahidi, 24ili ithibitike na jina lako litakuwa kuu milele. Kisha watu watasema, ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu aliye juu ya Israeli, ndiye Mungu wa Israeli.’ Nayo nyumba ya mtumishi wako Daudi itafanywa imara mbele zako.
25“Wewe, Mungu wangu, umemfunulia mtumishi wako Daudi kwamba utamjengea nyumba. Hivyo mtumishi wako amekuwa na ujasiri wa kukuomba maombi haya. 26Ee Mwenyezi Mungu, wewe ndiwe Mungu! Umemwahidi mtumishi wako mambo haya mazuri. 27Basi imekupendeza kuibariki nyumba ya mtumishi wako, ili idumu milele machoni pako; kwa ajili yako, Ee Mwenyezi Mungu, umeibariki, nayo itabarikiwa milele.”
Iliyochaguliwa sasa
1 Nyakati 17: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.