1 Nyakati 29:1-9
1 Nyakati 29:1-9 NENO
Ndipo Mfalme Daudi akawaambia kusanyiko lote: “Mwanangu Sulemani, yeye ambaye Mungu amemchagua, ni kijana mdogo na asiye na uzoefu. Kazi hii ni kubwa, kwa sababu Hekalu hili la fahari si kwa ajili ya mwanadamu bali ni kwa ajili ya BWANA Mungu. Kwa uwezo wangu wote nimetenga mali kwa ajili ya Hekalu la Mungu wangu: dhahabu kwa kazi za dhahabu, fedha kwa ajili ya fedha, shaba kwa kazi za shaba, chuma kwa kazi za chuma na miti kwa kazi za miti, vivyo hivyo vito vya shohamu kwa ajili ya kutia kwenye vijalizo, almasi, mawe ya rangi mbalimbali, aina zote za vito vya thamani na marumaru; haya yote kwa wingi mno. Zaidi ya hayo, kwa kujitolea kwangu kwa ajili ya Hekalu la Mungu wangu, sasa ninatoa hazina zangu mwenyewe za dhahabu na fedha kwa ajili ya Hekalu la Mungu wangu, zaidi ya mali niliyotoa kwa ajili ya Hekalu hili takatifu: talanta elfu tatu za dhahabu (dhahabu ya Ofiri), na talanta elfu saba za fedha safi iliyosafishwa, kwa ajili ya kufunika kuta za Hekalu, kwa kazi ya dhahabu na kazi ya fedha na kwa kazi yote itakayofanywa na mafundi. Basi, ni nani anayependa kujitoa kwa BWANA leo?” Ndipo viongozi wa jamaa, maafisa wa makabila ya Israeli, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, pamoja na maafisa waliokuwa wasimamizi wa kazi za mfalme wakatoa kwa hiari. Wakatoa kwa ajili ya kazi ya Hekalu la Mungu talanta elfu tano na darkoni elfu kumi za dhahabu, talanta elfu kumi za fedha, talanta elfu kumi na nane za shaba, na talanta elfu mia moja za chuma. Kila mmoja aliyekuwa na vito vya thamani akavitoa katika hazina ya Hekalu la BWANA, chini ya uangalizi wa Yehieli Mgershoni. Watu wakafurahi kwa sababu ya itikio la hiari la viongozi wao, kwa kuwa walikuwa wametoa kwa hiari na kwa moyo wote kwa BWANA. Mfalme Daudi pia akafurahi sana.


