1 Wakorintho 12:1-8
1 Wakorintho 12:1-8 NENO
Basi ndugu zangu, kuhusu karama za rohoni, sitaki mkose kufahamu. Mnajua kwamba mlipokuwa watu wasiomjua Mungu, kwa njia moja au nyingine mlishawishika na kupotoshwa mkielekezwa kwa sanamu zisizonena. Kwa hiyo nawaambieni ya kuwa hakuna mtu anayeongozwa na Roho Mtakatifu wa Mungu anayeweza kusema, “Isa na alaaniwe.” Pia hakuna mtu awezaye kusema, “Isa ni Bwana,” isipokuwa ameongozwa na Roho wa Mungu. Kuna aina mbalimbali za karama, lakini Roho ni yule yule. Kuna huduma za aina mbalimbali, lakini Bwana Isa ni yule yule. Kisha kuna tofauti za kutenda kazi, lakini ni Mungu yule yule atendaye kazi zote kwa watu wote. Basi kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho wa Mungu kwa faida ya wote. Maana mtu mmoja kwa Roho hupewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa kwa Roho huyo huyo.