1 Wakorintho 12
12
Karama za rohoni
1Basi ndugu zangu, kuhusu karama za rohoni, sitaki mkose kufahamu. 2Mnajua kwamba mlipokuwa watu wasiomjua Mungu, kwa njia moja au nyingine mlishawishika na kupotoshwa mkielekezwa kwa sanamu zisizonena. 3Kwa hiyo nawaambieni ya kuwa hakuna mtu anayeongozwa na Roho Mtakatifu wa Mungu anayeweza kusema, “Isa na alaaniwe.” Pia hakuna mtu awezaye kusema, “Isa ni Bwana,” isipokuwa ameongozwa na Roho wa Mungu.
4Kuna aina mbalimbali za karama, lakini Roho ni yule yule. 5Kuna huduma za aina mbalimbali, lakini Bwana Isa ni yule yule. 6Kisha kuna tofauti za kutenda kazi, lakini ni Mungu yule yule atendaye kazi zote kwa watu wote.
7Basi kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho wa Mungu kwa faida ya wote. 8Maana mtu mmoja kwa Roho hupewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa kwa Roho huyo huyo. 9Mtu mwingine imani kwa huyo Roho na mwingine karama za kuponya kwa huyo Roho mmoja. 10Kwa mwingine matendo ya miujiza, kwa mwingine unabii, kwa mwingine kupambanua roho, kwa mwingine kunena aina mbalimbali za lugha, na kwa mwingine bado, tafsiri za lugha. 11Haya yote hufanywa na huyo huyo Roho mmoja, Roho naye humgawia kila mtu, kama apendavyo.
Mwili mmoja wenye viungo vingi
12Kama vile mwili ulivyo mmoja nao una viungo vingi; navyo viungo vyote vya mwili ingawa ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Al-Masihi. 13Kwa maana katika Roho mmoja wa Mungu wote tulibatizwa katika mwili mmoja, kama ni Wayahudi au Wayunani, kama ni watumwa au watu huru, nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.
14Basi mwili si kiungo kimoja, bali ni viungo vingi. 15Kama mguu ungesema, “Kwa kuwa mimi si mkono basi mimi si wa mwili,” hiyo isingefanya huo mguu usiwe sehemu ya mwili. 16Na kama sikio lingesema, “Kwa kuwa mimi si jicho, basi mimi si wa mwili,” hiyo isingefanya hilo sikio lisiwe sehemu ya mwili. 17Kama mwili wote ungakuwa jicho tu, kusikia kungekuwa wapi? Au kama mwili wote ungekuwa sikio, kunusa kungekuwa wapi? 18Lakini kama ilivyo, Mungu ameweka viungo katika mwili, kila kimoja kama alivyopenda. 19Kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? 20Kama ulivyo, una viungo vingi, lakini mwili ni mmoja.
21Jicho haliwezi kuuambia mkono, “Sina haja nawe!” Wala kichwa hakiwezi kuiambia miguu, “Sina haja na ninyi!” 22Lakini badala yake, vile viungo vya mwili vinavyoonekana kuwa dhaifu, ndivyo ambavyo ni vya muhimu sana. 23Navyo vile viungo tunavyoviona havina heshima, ndivyo tunavipa heshima maalum. Vile viungo vya mwili ambavyo havina uzuri, tunavipa heshima ya pekee; 24wakati vile viungo vyenye uzuri havihitaji utunzaji wa pekee. Lakini Mungu ameviweka pamoja viungo vya mwili na akavipa heshima zaidi vile vilivyopungukiwa, 25ili pasiwe na mafarakano katika mwili, bali viungo vyote vihudumiane kwa usawa kila kimoja na mwenzake. 26Kama kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia pamoja nacho; kama kiungo kimoja kikipewa heshima, viungo vyote hufurahi pamoja nacho.
27Sasa ninyi ni mwili wa Al-Masihi na kila mmoja wenu ni sehemu ya huo mwili. 28Mungu ameweka katika jumuiya ya waumini kwanza mitume, pili manabii, tatu walimu, kisha watenda miujiza, pia karama za kuponya, karama za kusaidiana, karama za uongozi, na aina mbalimbali za lugha. 29Je, wote ni mitume? Je, wote ni manabii? Je, wote ni walimu? Je, wote wanatenda miujiza? 30Je, wote wana karama ya kuponya? Je, wote hunena kwa lugha mpya? Je, wote wanatafsiri? 31Basi tamanini sana karama zilizo kuu.
Nami nitawaonesha njia iliyo bora zaidi.
Iliyochaguliwa sasa
1 Wakorintho 12: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.