Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wakorintho 13

13
Karama ya upendo
1Hata kama nikisema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa kengele inayolia au toazi linalovuma. 2Ningekuwa na karama ya unabii na kujua siri zote na maarifa yote, hata kama nina imani kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, mimi si kitu. 3Nikitoa mali yote niliyo nayo, na nikijitolea mwili wangu uchomwe moto, kama sina upendo, hainifaidi kitu.
4Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno, hauna kiburi. 5Haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya. 6Upendo haufurahii mabaya bali hufurahi pamoja na kweli. 7Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.
8Upendo haushindwi kamwe. Lakini ukiwepo unabii, utakoma; zikiwepo lugha, zitakoma; yakiwepo maarifa, yatapita. 9Kwa maana tunafahamu kwa sehemu na tunatoa unabii kwa sehemu. 10Lakini ukamilifu ukija, yale yasiyo kamili hutoweka. 11Nilipokuwa mtoto, nilisema kama mtoto, niliwaza kama mtoto, nilifikiri kama mtoto. Nilipokuwa mtu mzima niliacha mambo ya kitoto. 12Kwa maana sasa tunaona taswira kama kwa kioo, lakini wakati huo tutaona wazi. Sasa nafahamu kwa sehemu, wakati huo nitafahamu kikamilifu, kama vile mimi ninavyofahamika kikamilifu.
13Basi sasa, yanadumu mambo haya matatu: Imani, tumaini na upendo. Lakini lililo kuu miongoni mwa haya matatu ni upendo.

Iliyochaguliwa sasa

1 Wakorintho 13: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia