1 Wakorintho 14
14
Karama za unabii na lugha
1Fuateni upendo na kutaka sana karama za roho, hasa karama ya unabii. 2Kwa maana mtu yeyote anayesema kwa lugha, hasemi na wanadamu bali anasema na Mungu. Kwa kuwa hakuna mtu yeyote anayemwelewa, kwani anasema mambo ya siri kwa roho. 3Lakini anayetoa unabii anasema na watu akiwajenga, kuwatia moyo na kuwafariji. 4Anenaye kwa lugha hujijenga mwenyewe, bali atoaye unabii huwajenga waumini. 5Ningependa kila mmoja wenu anene kwa lugha, lakini ningependa zaidi nyote mtoe unabii. Kwa kuwa yeye atoaye unabii ni mkuu kuliko anenaye kwa lugha, isipokuwa atafsiri, ili waumini wote wapate kujengwa.
6Sasa ndugu zangu, nikija kwenu nikasema kwa lugha mpya, nitawafaidia nini kama sikuwaletea ufunuo au neno la maarifa au unabii au mafundisho? 7Hata vitu visivyo na uhai vitoapo sauti, kama vile filimbi au kinubi, mtu atajuaje ni wimbo gani unaoimbwa kusipokuwa na tofauti ya upigaji? 8Tena kama tarumbeta haitoi sauti inayoeleweka, ni nani atakayejiandaa kwa ajili ya vita? 9Vivyo hivyo na ninyi, mkinena maneno yasiyoeleweka katika akili, mtu atajuaje mnalosema? Kwa maana mtakuwa mnasema hewani tu. 10Bila shaka ziko sauti nyingi ulimwenguni, wala hakuna isiyo na maana. 11Basi kama sielewi maana ya hiyo sauti, nitakuwa mgeni kwa yule msemaji, naye atakuwa mgeni kwangu. 12Vivyo hivyo na ninyi. Kwa kuwa mnatamani kuwa na karama za rohoni, jitahidini kuzidi sana katika karama kwa ajili ya kuwajenga waumini.
13Kwa sababu hii, yeye anenaye kwa lugha na aombe kwamba apate kutafsiri kile anachonena. 14Kwa maana nikiomba kwa lugha, roho yangu inaomba, lakini akili yangu haina matunda. 15Nifanyeje basi? Nitaomba kwa roho, na pia nitaomba kwa akili yangu. Nitaimba kwa roho na nitaimba kwa akili yangu pia. 16Ikiwa unabariki kwa roho, mtu mwingine atakayejikuta miongoni mwa hao wasiojua, atawezaje kusema “Amen” katika kushukuru kwako, wakati haelewi unachosema? 17Mnaweza kuwa mnatoa shukrani kweli, sawa, lakini huyo mtu mwingine hajengeki.
18Namshukuru Mungu kwamba mimi nanena kwa lugha kuliko ninyi nyote. 19Lakini katika kundi la waumini ni afadhali niseme maneno matano ya kueleweka ili niwafundishe wengine kuliko kusema maneno elfu kumi kwa lugha.
20Ndugu zangu, msiwe kama watoto katika kufikiri kwenu, afadhali kuhusu uovu mwe kama watoto wachanga, lakini katika kufikiri kwenu, mwe watu wazima. 21Katika Torati imeandikwa kwamba:
“Kupitia kwa watu wenye lugha ng’eni
na kupitia midomo ya wageni,
nitasema na watu hawa,
lakini hata hivyo hawatanisikiliza,
asema Mwenyezi Mungu.”#14:21 Isaya 28:11, 12
22Basi kunena kwa lugha ni ishara, si kwa waaminio, bali kwa wasioamini, wakati unabii si kwa ajili ya wasioamini, bali kwa ajili ya waaminio. 23Kwa hiyo kama kundi la waumini wote wakikutana na kila mmoja akanena kwa lugha, kisha wakaingia wageni wasioelewa au wasioamini, je, hawatasema kwamba wote mna wazimu? 24Lakini kama mtu asiyeamini au asiyeelewa akiingia wakati kila mtu anatoa unabii, ataaminishwa na watu wote kuwa yeye ni mwenye dhambi na kuhukumiwa na wote, 25nazo siri za moyo wake zitawekwa wazi. Kwa hiyo ataanguka chini na kumwabudu Mungu akikiri, “Kweli Mungu yuko kati yenu!”
Kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa utaratibu
26Basi tuseme nini ndugu zangu? Mnapokutana pamoja, kila mmoja ana wimbo, au neno la mafundisho, au ufunuo, lugha mpya au atatafsiri. Mambo yote yatendeke kwa ajili ya kulijenga kundi la waumini. 27Kama mtu yeyote akinena kwa lugha, basi waseme watu wawili au watatu, si zaidi, mmoja baada ya mwingine, na lazima awepo mtu wa kutafsiri. 28Lakini kama hakuna mtu wa kutafsiri, hao watu na wanyamaze kimya katika kundi la waumini, na wanene na nafsi zao wenyewe na Mungu.
29Manabii wawili au watatu wanene, na wengine wapime kwa makini yale yasemwayo. 30Kama mtu yeyote aliyeketi karibu, akipata ufunuo, basi yule wa kwanza na anyamaze. 31Kwa maana wote mnaweza kutoa unabii, mmoja baada ya mwingine, ili kila mtu apate kufundishwa na kutiwa moyo. 32Roho za manabii huwatii manabii. 33Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko bali ni Mungu wa amani.
Kama ilivyo katika makusanyiko yote ya watakatifu, 34wanawake wanapaswa kuwa kimya katika kundi la waumini. Hawaruhusiwi kusema, bali wanyenyekee kama Torati isemavyo. 35Wakitaka kuuliza kuhusu jambo lolote, wawaulize waume zao nyumbani. Kwa maana ni aibu kwa mwanamke kuzungumza katika kundi la waumini.
36Je, neno la Mungu lilianzia kwenu? Au ni ninyi tu ambao neno la Mungu limewafikia? 37Kama mtu yeyote akidhani kwamba yeye ni nabii, au ana karama za rohoni, basi na akubali kwamba haya ninayoandika ni maagizo kutoka kwa Bwana Isa. 38Kama mtu akipuuza jambo hili yeye mwenyewe atapuuzwa.
39Kwa hiyo ndugu zangu, takeni sana kutoa unabii na msikataze watu kusema kwa lugha. 40Lakini kila kitu kitendeke kwa ufasaha na kwa utaratibu.
Iliyochaguliwa sasa
1 Wakorintho 14: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.