Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wakorintho 15

15
Kufufuka kwa Al-Masihi
1Basi ndugu zangu nataka niwakumbushe kuhusu Injili niliyowahubiria, mkaipokea na ambayo katika hiyo mmesimama. 2Kwa Injili hii mnaokolewa mkishikilia kwa uthabiti neno nililowahubiria ninyi. La sivyo, mmeamini katika ubatili.
3Kwa maana yale niliyopokea ndiyo niliyowapa ninyi, kama yenye umuhimu wa kwanza: Kwamba Al-Masihi alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama Maandiko yanavyosema, 4ya kuwa alizikwa na alifufuliwa siku ya tatu, kama Maandiko yanavyosema, 5na kwamba alimtokea Kefa#15:5 yaani Petro, kisha akawatokea wale kumi na wawili. 6Baadaye akawatokea wale ndugu waumini zaidi ya mia tano kwa pamoja, ambao wengi wao bado wako hai, ingawa wengine wamelala. 7Ndipo akamtokea Yakobo na kisha mitume wote. 8Mwisho wa wote, akanitokea mimi pia, ambaye ni kama aliyezaliwa si kwa wakati wake.
9Kwa maana mimi ndiye mdogo kuliko mitume wote, nisiyestahili kuitwa mtume, kwa sababu niliwatesa waumini wa Mungu. 10Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo, na neema yake kwangu haikuwa kitu bure. Bali nilizidi sana kufanya kazi kuliko mitume wote, lakini haikuwa mimi, bali ni ile neema ya Mungu iliyokuwa pamoja nami. 11Hivyo basi, kama ilikuwa mimi au wao, hili ndilo tunalohubiri, na hili ndilo mliloamini.
Ufufuo wa wafu
12Basi kama tumehubiri kwamba Al-Masihi alifufuliwa kutoka kwa wafu, mbona baadhi yenu mnasema hakuna ufufuo wa wafu? 13Lakini kama hakuna ufufuo wa wafu, basi hata Al-Masihi hakufufuliwa. 14Tena ikiwa Al-Masihi hakufufuliwa kutoka kwa wafu, kuhubiri kwetu kumekuwa ni bure na imani yenu ni batili. 15Zaidi ya hayo, twaonekana kuwa mashahidi wa uongo kuhusu Mungu, kwa sababu tumeshuhudia kumhusu Mungu kwamba alimfufua Al-Masihi kutoka kwa wafu, lakini hilo haliwezi kuwa kweli kama wafu hawafufuliwi. 16Kwa kuwa kama wafu hawafufuliwi, basi hata Al-Masihi hajafufuka. 17Tena kama Al-Masihi hajafufuliwa, imani yenu ni batili; nanyi bado mko katika dhambi zenu. 18Hivyo basi, wote waliolala katika Al-Masihi wamepotea. 19Ikiwa tumaini letu ndani ya Al-Masihi ni kwa ajili ya maisha haya tu, sisi tunastahili kuhurumiwa kuliko watu wote.
20Lakini kweli Al-Masihi amefufuliwa kutoka kwa wafu, tunda la kwanza la wale wote waliolala. 21Kwa maana kama vile mauti ilivyokuja kupitia kwa mtu mmoja, vivyo hivyo, ufufuo wa wafu umekuja kupitia kwa mtu mmoja. 22Kwa maana kama vile katika Adamu watu wote wanakufa, vivyo hivyo katika Al-Masihi wote watafanywa hai. 23Lakini kila mmoja kwa wakati wake: Al-Masihi, tunda la kwanza kisha, wale walio wake, wakati atakapokuja. 24Ndipo mwisho utafika, atakapomkabidhi Mungu Baba#15:24 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. Mwenyezi ufalme, baada ya kuangamiza kila utawala na kila mamlaka na nguvu. 25Kwa maana lazima Al-Masihi atawale hadi awe amewaweka adui zake wote chini ya miguu yake. 26Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni mauti. 27Kwa maana Mungu “ameweka vitu vyote chini ya miguu yake”#15:27 Zaburi 8:6. Lakini isemapo kwamba “vitu vyote” vimewekwa chini yake, ni wazi kwamba Mungu aliyetiisha vitu vyote chini ya Al-Masihi hayumo miongoni mwa hivyo vilivyotiishwa. 28Atakapokuwa amekwisha kuyafanya haya, ndipo Mwana mwenyewe atatiishwa chini yake yeye aliyetiisha vitu vyote, ili Mungu awe yote katika yote.
29Basi kama hakuna ufufuo, watafanyaje wale wabatizwao kwa ajili ya wafu? Kama wafu hawafufuliwi kamwe, mbona watu wanabatizwa kwa ajili yao? 30Nasi kwa upande wetu kwa nini tunajihatarisha kila saa? 31Kama majivuno yangu kwa ajili yenu katika Al-Masihi Isa Bwana wetu ni kweli, ndugu zangu, ninakufa kila siku. 32Kama kwa sababu za kibinadamu tu nilipigana na wanyama wakali huko Efeso, ningekuwa nimepata faida gani? Kama wafu hawafufuliwi,
“Tuleni na kunywa,
kwa kuwa kesho tutakufa.”#15:32 Isaya 22:13
33Msidanganyike: “Ushirika na watu wabaya huharibu tabia njema.” 34Zindukeni mwe na akili kama iwapasavyo, wala msitende dhambi tena; kwa maana watu wengine hawamjui Mungu. Nasema mambo haya ili mwone aibu.
Mwili wa ufufuo
35Lakini mtu anaweza kuuliza, “Wafu wafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?” 36Ninyi wapumbavu kiasi gani? Mpandacho hakiwi hai kama hakikufa. 37Mpandapo, hampandi mwili ule utakao kuwa, bali mwapanda mbegu tu, pengine ya ngano au ya kitu kingine. 38Lakini Mungu huipa mbegu umbo kama alivyokusudia mwenyewe na kila aina ya mbegu huipa umbo lake. 39Kwa maana nyama zote si za aina moja. Binadamu wana nyama ya aina moja, wanyama wana aina nyingine, kadhalika ndege na samaki wana nyama tofauti. 40Pia kuna miili ya mbinguni na miili ya duniani, lakini fahari ya ile miili ya mbinguni ni ya aina moja, na fahari ya ile miili ya duniani ni ya aina nyingine. 41Jua lina fahari ya aina moja, mwezi nao una fahari yake na nyota pia, nazo nyota hutofautiana katika fahari.
42Hivyo ndivyo itakavyokuwa wakati wa ufufuo wa wafu. Ule mwili wa kuharibika uliopandwa, utafufuliwa usioharibika; 43unapandwa katika aibu, unafufuliwa katika utukufu, unapandwa katika udhaifu, unafufuliwa katika nguvu, 44unapandwa mwili wa asili, unafufuliwa mwili wa kiroho.
Kama kuna mwili wa asili, basi kuna mwili wa kiroho pia. 45Kwa hiyo imeandikwa, “Mtu wa kwanza Adamu alifanyika kiumbe hai”#15:45 Mwanzo 2:7; Adamu wa mwisho, yeye ni roho iletayo uzima. 46Lakini si ule wa kiroho uliotangulia, bali ni ule wa asili, kisha ule wa kiroho. 47Mtu wa kwanza aliumbwa kwa mavumbi ya ardhini, mtu wa pili alitoka mbinguni. 48Kama vile alivyokuwa yule wa ardhini, ndivyo walivyo wale walio wa ardhini; na kwa vile alivyo mtu yule aliyetoka mbinguni, ndivyo walivyo wale walio wa mbinguni. 49Kama vile tulivyochukua mfano wa mtu wa ardhini, ndivyo tutakavyochukua mfano wa yule mtu aliyetoka mbinguni.
50Ndugu zangu nisemalo ni hili: mwili na damu haviwezi kuurithi ufalme wa Mungu, wala kuharibika kurithi kutokuharibika. 51Sikilizeni, nawaambia siri: Sote hatutalala, lakini sote tutabadilishwa: 52ghafula, kufumba na kufumbua, parapanda ya mwisho itakapolia. Kwa kuwa parapanda italia, nao wafu watafufuliwa na miili isiyoharibika, nasi tutabadilishwa. 53Kwa maana mwili huu wa kuharibika lazima uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa lazima uvae kutokufa. 54Kwa hiyo, mwili huu wa kuharibika utakapovaa kutokuharibika, nao huu mwili wa kufa utakapovaa kutokufa, ndipo lile neno lililoandikwa litakapotimia: “Mauti imemezwa kwa kushinda.”#15:54 Isaya 25:8
55“Kuko wapi, ee mauti, kushinda kwako?
Uko wapi, ee mauti, uchungu wako?”#15:55 Hosea 13:14
56Uchungu wa mauti ni dhambi na nguvu ya dhambi ni sheria. 57Lakini Mungu apewe shukrani, yeye atupaye ushindi kupitia kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi.
58Kwa hiyo, ndugu zangu wapendwa, simameni imara. Msitikisike. Mzidi sana katika kuitenda kazi ya Bwana Isa, kwa maana mnajua ya kuwa, kazi yenu katika Bwana Isa si bure.

Iliyochaguliwa sasa

1 Wakorintho 15: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia