1 Wakorintho 11
11
1Igeni mfano wangu, kama ninavyouiga mfano wa Al-Masihi.
Utaratibu katika ibada
2Ninawasifu kwa kunikumbuka katika kila jambo na kwa kushika mapokeo kama nilivyowapatia.
3Napenda mfahamu kwamba kichwa cha kila mwanaume ni Al-Masihi, na kichwa cha mwanamke ni mwanaume, nacho kichwa cha Al-Masihi ni Mungu. 4Kila mwanaume anayeomba au kutoa unabii akiwa amefunika kichwa chake, anakiaibisha kichwa chake. 5Naye kila mwanamke anayeomba au kutoa unabii pasipo kufunika kichwa chake, anakiaibisha kichwa chake, kwani ni sawa na yeye aliyenyoa nywele. 6Kama mwanamke hatajifunika kichwa chake, basi inampasa kunyoa nywele zake. Lakini kama ni aibu kwa mwanamke kukata au kunyoa nywele zake, basi afunike kichwa chake.
7Haimpasi mwanaume kufunika kichwa chake kwa kuwa yeye ni mfano wa Mungu na utukufu wa Mungu; lakini mwanamke ni utukufu wa mwanaume. 8Kwa maana mwanaume hakutoka kwa mwanamke, bali mwanamke alitoka kwa mwanaume. 9Wala mwanaume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanaume. 10Kwa sababu hii na kwa sababu ya malaika, inampasa mwanamke awe na ishara ya mamlaka juu yake. 11Lakini katika Bwana Isa, mwanamke hajitegemei pasipo mwanaume na mwanaume hajitegemei pasipo mwanamke. 12Kama vile mwanamke alivyoumbwa kutoka kwa mwanaume, vivyo hivyo mwanaume huzaliwa na mwanamke. Lakini vitu vyote vyatoka kwa Mungu.
13Hukumuni ninyi wenyewe: Je, inafaa kwa mwanamke kumwomba Mungu bila kufunika kichwa chake? 14Je, maumbile ya asili hayatufundishi kuwa ni aibu kwa mwanaume kuwa na nywele ndefu? 15Lakini mwanamke akiwa na nywele ndefu ni utukufu kwake? Kwa maana mwanamke amepewa nywele ndefu ili kumfunika. 16Kama mtu anataka kubishana kuhusu jambo hili, sisi wala makundi ya waumini ya Mungu hatutambui desturi nyingine.
Matumizi mabaya ya Chakula cha Bwana Isa
17Basi katika maagizo yafuatayo, siwezi kuwasifu, kwa sababu mkutanikapo si kwa ajili ya faida bali kwa hasara. 18Kwanza, mnapokutana kama kundi la waumini, nasikia kwamba kuna mgawanyiko miongoni mwenu, nami kwa kiasi fulani nasadiki kuwa ndivyo ilivyo. 19Bila shaka lazima pawe na tofauti miongoni mwenu ili kuonesha ni nani anayekubaliwa na Mungu. 20Mkutanikapo pamoja si Chakula cha Bwana Isa mnachokula, 21kwa kuwa mnapokula, kila mmoja wenu anakula bila kuwangoja wengine. Mmoja hukaa njaa na mwingine analewa. 22Je, hamna nyumbani kwenu ambako mnaweza kula na kunywa? Au mnalidharau kundi la waumini la Mungu na kuwadhalilisha wale wasio na kitu? Niwaambie nini? Je, niwasifu kuhusu jambo hili? La, hasha!
Kushiriki Chakula cha Bwana Isa
(Mathayo 26:26-29; Marko 14:22-25; Luka 22:14-20)
23Kwa maana mimi nilipokea kutoka kwa Bwana Isa yale niliyowapa ninyi, kwamba Bwana Isa, usiku ule aliposalitiwa, alitwaa mkate, 24naye baada ya kushukuru, akaumega, akasema, “Huu ndio mwili wangu, uliotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” 25Vivyo hivyo baada ya kula, akakitwaa kikombe, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu. Fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.” 26Maana kila mlapo mkate huu na kunywea kikombe hiki, mnatangaza mauti ya Bwana Isa hadi ajapo.
Kushiriki Chakula cha Bwana Isa isivyostahili
27Kwa hiyo, mtu yeyote alaye mkate huo au kukinywea kikombe hicho cha Bwana Isa isivyostahili, atakuwa na hatia ya dhambi juu ya mwili na damu ya Bwana Isa. 28Inampasa mtu ajichunguze mwenyewe, kabla ya kula mkate na kukinywea kikombe. 29Kwa maana mtu yeyote alaye na kunywa pasipo kuutambua mwili wa Bwana Isa, hula na kunywa hukumu juu yake mwenyewe. 30Hii ndiyo sababu wengi miongoni mwenu ni wagonjwa na dhaifu na wengine wenu hata wamekufa. 31Lakini kama tungejichunguza wenyewe tusingehukumiwa. 32Tunapohukumiwa na Bwana Isa, tunaadibishwa ili tusije tukahukumiwa pamoja na ulimwengu.
33Kwa hiyo, ndugu zangu, mkutanikapo pamoja ili kula, mngojane. 34Kama mtu akiwa na njaa, ale nyumbani mwake ili mkutanapo pamoja msije mkahukumiwa.
Nami nitakapokuja nitawapa maelekezo zaidi.
Iliyochaguliwa sasa
1 Wakorintho 11: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.