Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wakorintho 10

10
Onyo kutoka historia ya Waisraeli
1Ndugu zangu, sitaki mkose kufahamu ukweli huu kwamba baba zetu walikuwa wote chini ya wingu na kwamba wote walipita katikati ya bahari. 2Wote wakabatizwa kuwa wa Musa ndani ya lile wingu na ndani ya ile bahari. 3Wote walikula chakula kile kile cha roho, 4na wote wakanywa kile kile kinywaji cha roho, kwa maana walikunywa kutoka ule mwamba wa roho uliofuatana nao, nao ule mwamba ulikuwa Al-Masihi. 5Lakini Mungu hakupendezwa na wengi wao, kwa hiyo miili yao ilitapakaa jangwani.
6Basi mambo haya yalifanyika kama mifano ili kutuzuia tusiweke mioyo yetu katika mambo maovu kama wao walivyofanya. 7Msiwe waabudu sanamu, kama baadhi yao walivyokuwa, kama ilivyoandikwa, “Watu waliketi chini kula na kunywa, kisha wakainuka kucheza na kufanya sherehe za kipagani.”#10:7 Kutoka 32:6 8Wala tusifanye uzinzi kama baadhi yao walivyofanya, wakafa watu elfu ishirini na tatu kwa siku moja. 9Wala tusimjaribu Al-Masihi, kama baadhi yao walivyofanya, wakafa kwa kuumwa na nyoka. 10Msinung’unike kama baadhi yao walivyofanya, wakaangamizwa na malaika mharibifu.
11Mambo haya yote yaliwapata wao ili yawe mifano kwa wengine, nayo yaliandikwa ili yatuonye sisi ambao mwisho wa nyakati umetufikia. 12Hivyo, yeye ajidhaniaye amesimama, aangalie asianguke. 13Hakuna jaribu lolote lililowapata ambalo si la kawaida kwa wanadamu. Naye Mungu ni mwaminifu; hataruhusu mjaribiwe kupita mnavyoweza. Lakini mnapojaribiwa atawapa njia ya kushinda ili mweze kustahimili.
Karamu za sanamu na Chakula cha Bwana Isa
14Kwa hiyo wapendwa wangu, zikimbieni ibada za sanamu. 15Nasema watu wenye ufahamu, amueni wenyewe kuhusu haya niyasemayo. 16Je, kikombe cha baraka ambacho tunakibariki, si ushirika katika damu ya Al-Masihi? Mkate tunaoumega, si ushirika wa mwili wa Al-Masihi? 17Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja, kwa kuwa wote twashiriki mkate mmoja.
18Waangalieni watu wa Israeli: Je, wale wote walao dhabihu si ni wale watendao kazi madhabahuni? 19Je, nina maana kwamba sadaka iliyotolewa kwa sanamu ni kitu chenye maana yoyote? Au kwamba sanamu ni kitu chenye maana yoyote? 20La hasha! Lakini sadaka za watu wasiomjua Mungu hutolewa kwa mashetani, wala si kwa Mungu. Nami sitaki ninyi mwe na ushirika na mashetani. 21Hamwezi kunywa katika kikombe cha Bwana Isa na cha mashetani pia. Hamwezi kuwa na sehemu katika Chakula cha Bwana Isa na katika chakula cha mashetani pia. 22Je, tunataka kuamsha wivu wa Mwenyezi Mungu? Je, sisi tuna nguvu kuliko yeye?
Fanyeni yote kwa utukufu wa Mwenyezi Mungu
23“Vitu vyote ni halali,” lakini si vitu vyote vilivyo na faida. “Vitu vyote ni halali,” lakini si vyote vinavyojenga. 24Mtu yeyote asitafute yaliyo yake mwenyewe, bali kila mtu atafute yale yanayowafaa wengine.
25Kuleni chochote kinachouzwa sokoni, bila kuuliza swali lolote kwa ajili ya dhamiri. 26Kwa maana, “Dunia na vyote vilivyomo ni mali ya Mwenyezi Mungu.”#10:26 Zaburi 24:1
27Ukikaribishwa chakula na mtu asiyeamini nawe ukikubali kwenda, kula kila kitu kitakachowekwa mbele yako bila kuuliza maswali kwa ajili ya dhamiri. 28Lakini kama mtu yeyote akikuambia, “Hiki kimetolewa sadaka kwa sanamu,” basi usikile kwa ajili ya huyo aliyekuambia na kwa ajili ya dhamiri. 29Nina maana dhamiri ya huyo aliyekuambia, wala si kwa ajili ya dhamiri yako. Lakini kwa nini uhuru wangu uhukumiwe na dhamiri ya mtu mwingine? 30Nikila kwa shukrani, kwa nini nashutumiwa kwa ajili ya kile ambacho ninamshukuria Mungu?
31Basi, lolote mfanyalo, kama ni kula au kunywa, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu. 32Msiwe kikwazo kwa mtu yeyote, wawe Wayahudi au Wayunani, au kwa kundi la waumini la Mungu, 33kama hata mimi ninavyojaribu kumpendeza kila mtu kwa kila namna. Kwa maana sitafuti mema kwa ajili yangu mwenyewe bali kwa ajili ya wengi, ili waweze kuokolewa.

Iliyochaguliwa sasa

1 Wakorintho 10: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia