1 Wakorintho 9
9
Haki za Mtume Paulo
1Je, mimi si huru? Je, mimi si mtume? Je, mimi sikumwona Isa, Bwana wetu? Je, ninyi si matunda ya kazi yangu katika Bwana? 2Hata kama mimi si mtume kwa wengine, hakika mimi ni mtume kwenu, kwa maana ninyi ni muhuri wa utume wangu katika Bwana Isa.
3Huu ndio utetezi wangu kwa hao wanaokaa kunihukumu. 4Je, hatuna haki ya kula na kunywa? 5Je, hatuna haki ya kusafiri na mke anayeamini, kama wanavyofanya mitume wengine na ndugu zake Bwana Isa na Kefa#9:5 yaani Petro? 6Au ni mimi na Barnaba tu inatubidi kufanya kazi ili tuweze kupata mahitaji yetu?
7Ni askari yupi aendaye vitani kwa gharama zake mwenyewe? Ni nani apandaye shamba la mizabibu na asile matunda yake? Ni nani achungaye kundi na asipate maziwa yake. 8Je, nasema mambo haya katika mtazamo wa kibinadamu tu? Je, Torati haisemi vivyo hivyo? 9Kwa maana imeandikwa katika Torati ya Musa: “Usimfunge maksai kinywa apurapo nafaka.”#9:9 Kumbukumbu 25:4 Je, Mungu hapa anahusika na ng’ombe? 10Je, Mungu hasemi haya hasa kwa ajili yetu? Hakika yameandikwa kwa ajili yetu, kwa sababu mtu anapolima na mpuraji akapura nafaka, wote wanapaswa kufanya hivyo wakiwa na tumaini la kushiriki mavuno. 11Je, ikiwa sisi tulipanda mbegu ya kiroho miongoni mwenu, itakuwa ni jambo kubwa iwapo tutavuna vitu vya mwili kutoka kwenu? 12Kama wengine wana haki ya kupata msaada kutoka kwenu, isingepasa tuwe na haki hiyo hata zaidi?
Lakini sisi hatukutumia haki hii. Kinyume chake, tunavumilia kila kitu ili tusije tukazuia Injili ya Al-Masihi. 13Je, hamjui kwamba, watu wafanyao kazi hekaluni hupata chakula chao kutoka hekaluni, nao wale wahudumiao madhabahuni hushiriki kile kitolewacho madhabahuni? 14Vivyo hivyo, Bwana Isa ameamuru kwamba wale wanaohubiri Injili wapate riziki yao kutokana na Injili.
15Lakini sijatumia hata mojawapo ya haki hizi. Nami siandiki haya nikitumaini kwamba mtanifanyia mambo hayo. Heri nife kuliko mtu yeyote kuninyima huku kujisifu kwangu. 16Lakini ninapohubiri Injili siwezi kujisifu maana ninalazimika kuhubiri. Ole wangu nisipoihubiri Injili! 17Nikihubiri kwa hiari, ninayo thawabu. Lakini kama si kwa hiari, basi ninachofanya ni kutekeleza tu uwakili niliowekewa. 18Basi je, thawabu yangu ni nini? Thawabu yangu ni hii: Ya kwamba katika kuhubiri Injili niitoe bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu uwezo wangu nilio nao katika Injili.
19Ingawa mimi ni huru, wala si mtumwa wa mtu yeyote, nimejifanya mtumwa wa kila mtu, ili niweze kuwavuta wengi kadiri iwezekanavyo. 20Kwa Wayahudi, nilikuwa kama Myahudi, ili niwapate Wayahudi. Kwa watu wale walio chini ya Torati, nilikuwa kama aliye chini ya Torati (ingawa mimi siko chini ya Torati), ili niweze kuwapata wale walio chini ya Torati. 21Kwa watu wasio na Torati nilikuwa kama asiye na Torati (ingawa siko huru mbali na Torati ya Mungu, bali niko chini ya sheria ya Al-Masihi), ili niweze kuwapata wale wasio na sheria. 22Kwa walio dhaifu nilikuwa dhaifu, ili niweze kuwapata walio dhaifu. Nimekuwa mtu wa hali zote kwa watu wote ili kwa njia yoyote niweze kuwaokoa baadhi yao. 23Nafanya haya yote kwa ajili ya Injili, ili nipate kushiriki baraka zake.
24Je, hamjui kwamba katika mashindano ya mbio wote wanaoshindana hukimbia, lakini ni mmoja wao tu apewaye tuzo? Kwa hiyo kimbieni katika mashindano ili mkapata tuzo.
25Kila mmoja anayeshiriki katika mashindano hufanya mazoezi makali. Wao hufanya hivyo ili wapokee taji lisilodumu, lakini sisi tunafanya hivyo ili kupata taji linalodumu milele. 26Kwa hiyo mimi sikimbii kama mtu akimbiaye bila lengo, sipigani kama mtu anayepiga hewa. 27La, bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha, ili nikiisha kuwahubiria wengine, nisije nikakataliwa.
Iliyochaguliwa sasa
1 Wakorintho 9: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.