1 Wakorintho 4:1-7
1 Wakorintho 4:1-7 NENO
Basi, watu na watuhesabu sisi kuwa tu watumishi wa Al-Masihi na mawakili wa siri za Mungu. Tena, litakiwalo ni mawakili waonekane kuwa waaminifu. Lakini kwangu mimi ni jambo dogo sana kwamba nihukumiwe na ninyi au na mahakama yoyote ya kibinadamu. Naam, hata mimi mwenyewe sijihukumu. Dhamiri yangu ni safi, lakini hilo halinihesabii kuwa asiye na hatia. Bwana Isa ndiye anihukumuye. Kwa hiyo msihukumu jambo lolote kabla ya wakati wake. Ngojeni hadi Bwana Isa atakapokuja. Yeye atayaleta nuruni mambo yale yaliyofichwa gizani, na kuweka wazi nia za mioyo ya wanadamu. Wakati huo kila mmoja atapokea sifa anayostahili kutoka kwa Mungu. Basi ndugu zangu, mambo haya nimeyafanya kwangu binafsi na Apolo kwa faida yenu, ili mweze kujifunza kutoka kwetu maana ya ule usemi usemao, “Msivuke zaidi ya yale yaliyoandikwa.” Hivyo hamtajivunia mtu fulani na kumdharau mwingine. Kwa maana ni nani aliyewafanya kuwa tofauti na wengine? Ni nini mlicho nacho ambacho hamkupokea? Nanyi kama mlipokea, kwa nini mnajivuna kama vile hamkupokea?