Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Yohana 2

2
Al-Masihi mwombezi wetu
1Watoto wangu wapendwa, nawaandikia haya ili msitende dhambi. Lakini mtu yeyote akitenda dhambi, tunaye Mwombezi kwa Baba: ndiye Isa Al-Masihi, Mwenye Haki. 2Yeye ndiye dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu, wala si kwa ajili ya dhambi zetu tu, bali pia kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote.
3Basi katika hili twajua ya kuwa tumemjua, tukizishika amri zake. 4Mtu yeyote asemaye kuwa, “Ninamjua,” lakini hazishiki amri zake, ni mwongo, wala ndani ya mtu huyo hamna kweli. 5Lakini mtu yeyote anayelitii neno lake, upendo wa Mungu umekamilika ndani yake kweli kweli. Katika hili twajua kuwa tumo ndani yake: 6Yeyote anayesema anakaa ndani yake hana budi kuenenda kama Isa alivyoenenda.
Amri mpya
7Wapendwa, siwaandikii ninyi amri mpya bali ile ya zamani, ambayo mmekuwa nayo tangu mwanzo. Amri hii ya zamani ni lile neno mlilosikia. 8Lakini nawaandikia amri mpya, yaani lile neno lililo kweli ndani yake na ndani yenu, kwa sababu giza linapita na ile nuru ya kweli tayari inang’aa.
9Yeyote anayesema yumo nuruni lakini anamchukia ndugu yake bado yuko gizani. 10Yeye ampendaye ndugu yake anakaa nuruni, wala hakuna kitu chochote ndani yake cha kumkwaza. 11Lakini yeyote amchukiaye ndugu yake, yuko gizani na anaenenda gizani, wala hajui anakoenda, kwa sababu giza limempofusha macho.
12Nawaandikia ninyi, watoto wadogo,
kwa sababu dhambi zenu
zimesamehewa kwa ajili ya Jina lake.
13Nawaandikia ninyi, akina baba,
kwa sababu mmemjua
yeye aliye tangu mwanzo.
Nawaandikia ninyi vijana
kwa sababu mmemshinda yule mwovu.
Nawaandikia ninyi watoto wadogo,
kwa sababu mmemjua Baba.
14Nawaandikia ninyi akina baba,
kwa sababu mmemjua
yeye aliye tangu mwanzo.
Nawaandikia ninyi vijana,
kwa sababu mna nguvu,
na neno la Mungu linakaa ndani yenu,
nanyi mmemshinda yule mwovu.
Msiupende ulimwengu
15Msiupende ulimwengu wala mambo yaliyo ulimwenguni. Mtu yeyote akiupenda ulimwengu, upendo wa Baba haumo ndani yake. 16Kwa maana kila kitu kilichomo ulimwenguni, yaani tamaa ya mwili, tamaa ya macho na kiburi cha uzima, havitokani na Baba bali hutokana na ulimwengu. 17Nao ulimwengu unapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu milele.
Onyo dhidi ya wanaompinga Al-Masihi
18Watoto wadogo, huu ni wakati wa mwisho! Kama mlivyosikia kwamba anayempinga Al-Masihi anakuja, hivyo basi wanaompinga Al-Masihi wengi wamekwisha kuja. Kutokana na hili twajua kwamba huu ni wakati wa mwisho. 19Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu hasa. Kwa maana kama wangekuwa wa kwetu, wangekaa pamoja nasi; lakini kutoka kwao kulionesha kwamba hakuna hata mmoja wao aliyekuwa wa kwetu.
20Lakini ninyi mmepakwa mafuta na yeye Aliye Mtakatifu, nanyi nyote mnaijua kweli. 21Siwaandikii kwa sababu hamuijui kweli, bali kwa sababu mnaijua, nanyi mnajua hakuna uongo unaotoka katika kweli. 22Je, mwongo ni nani? Mwongo ni mtu yule asemaye kwamba Isa si Al-Masihi. Mtu kama huyo ndiye anayempinga Al-Masihi, yaani yeye humkana Baba na Mwana. 23Hakuna yeyote amkanaye Mwana aliye na Baba. Yeyote anayemkubali Mwana anaye na Baba pia.
24Bali ninyi, hakikisheni kwamba lile mlilosikia tangu mwanzo linadumu ndani yenu. Kama lile mlilosikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu, ninyi nanyi mtakaa ndani ya Mwana na ndani ya Baba. 25Hii ndiyo ahadi yake kwetu, yaani uzima wa milele.
26Nawaandikia mambo haya kuhusu wale watu ambao wanajaribu kuwapotosha. 27Bali ninyi, upako mlioupata kutoka kwake unadumu ndani yenu, wala ninyi hamna haja ya mtu yeyote kuwafundisha. Lakini kama vile upako wake unavyowafundisha kuhusu mambo yote nayo ni kweli wala si uongo, basi kama ulivyowafundisha kaeni ndani yake.
Watoto wa Mwenyezi Mungu
28Sasa basi, watoto wapendwa, kaeni ndani yake, ili atakapofunuliwa, tuwe na ujasiri, wala tusiaibike mbele zake wakati wa kuja kwake.
29Mkijua kuwa yeye ni mwenye haki, mwajua kwamba kila atendaye haki amezaliwa naye.

Iliyochaguliwa sasa

1 Yohana 2: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia