1 Yohana 4
4
Zijaribuni roho
1Wapendwa, msiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho mwone kama zimetoka kwa Mungu, kwa sababu manabii wengi wa uongo wametokea ulimwenguni. 2Hivi ndivyo mnavyoweza kutambua Roho wa Mungu: Kila roho inayokubali kwamba Isa Al-Masihi amekuja katika mwili yatoka kwa Mungu. 3Lakini kila roho ambayo haimkubali Isa haitoki kwa Mungu. Hii ndiyo roho ya anayempinga Al-Masihi, ambayo mmesikia kwamba inakuja na sasa tayari iko ulimwenguni.
4Watoto wapendwa, ninyi mmetokana na Mungu, nanyi mmewashinda kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika ulimwengu. 5Wao wanatokana na ulimwengu na kwa hiyo hunena yaliyo ya ulimwengu, hivyo ulimwengu huwasikiliza. 6Sisi twatokana na Mungu na yeyote anayemjua Mungu hutusikiliza, lakini asiyetokana na Mungu hatusikilizi. Hivi ndivyo tunavyoweza kutambua Roho wa Kweli na roho ya upotovu.
Mwenyezi Mungu ni pendo
7Wapendwa, tupendane, kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu. Kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. 8Yeye asiyependa hamjui Mungu, kwa sababu Mungu ni pendo. 9Hivi ndivyo Mungu alivyoonesha pendo lake kwetu: Mungu alimtuma Mwanawe wa pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kupitia kwake. 10Hili ndilo pendo: si kwamba tulimpenda Mungu, bali yeye alitupenda, akamtuma Mwanawe, ili yeye awe dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu. 11Wapendwa, kama Mungu alivyotupenda sisi, imetupasa na sisi kupendana. 12Hakuna mtu yeyote aliyemwona Mungu wakati wowote. Lakini tukipendana, Mungu anakaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu.
13Tunajua kwamba twakaa ndani yake na yeye ndani yetu, kwa sababu ametupatia sisi sehemu ya Roho wake Mtakatifu. 14Nasi tumeona na kushuhudia kwamba Baba#4:14 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. amemtuma Mwanawe ili awe Mwokozi wa ulimwengu. 15Kila akiriye kwamba Isa ni Mwana wa Mungu, basi Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu. 16Hivyo nasi twajua na kulitumainia pendo la Mungu alilo nalo kwa ajili yetu.
Mungu ni Upendo. Kila akaaye katika upendo hukaa ndani ya Mungu na Mungu hukaa ndani yake. 17Kwa njia hii, pendo hukamilishwa miongoni mwetu ili tupate kuwa na ujasiri katika siku ya hukumu, kwa sababu kama alivyo ndivyo tulivyo sisi katika ulimwengu huu. 18Katika pendo hakuna hofu. Lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa sababu hofu inahusika na adhabu. Kila mwenye hofu hakukamilika katika pendo.
19Twampenda yeye kwa sababu yeye alitupenda kwanza. 20Ikiwa mtu atasema, “Nampenda Mungu,” lakini anamchukia ndugu yake, yeye ni mwongo. Kwa maana kila mtu asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona, atampendaje Mungu asiyemwona? 21Naye ametupatia amri hii: Yeyote anayempenda Mungu lazima pia ampende ndugu yake.
Iliyochaguliwa sasa
1 Yohana 4: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.