1 Wafalme 15:9-24
1 Wafalme 15:9-24 NENO
Katika mwaka wa ishirini wa utawala wa Yeroboamu mfalme wa Israeli, Asa akawa mfalme wa Yuda, naye akatawala katika Yerusalemu miaka arobaini na moja. Bibi yake aliitwa Maaka binti Abishalomu. Asa akatenda yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu, kama alivyokuwa ametenda Daudi, baba yake. Akawafukuza mahanithi wa mahali pa ibada za sanamu kutoka nchi, na kuondoa sanamu zote ambazo baba zake walikuwa wametengeneza. Hata akamwondoa bibi yake Maaka kwenye wadhifa wake kama mama malkia, kwa sababu alikuwa ametengeneza nguzo ya Ashera ya kuchukiza. Asa akaikata hiyo nguzo na kuiteketeza kwa moto katika Bonde la Kidroni. Ijapokuwa hakuondoa mahali pa juu pa kuabudia, moyo wa Asa ulikuwa umejiweka kwa Mwenyezi Mungu kikamilifu maisha yake yote. Akaleta ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu fedha na dhahabu na vyombo ambavyo yeye na baba yake walikuwa wameviweka wakfu. Kulikuwa na vita kati ya Asa na Baasha, mfalme wa Israeli siku zote za utawala wao. Mfalme Baasha wa Israeli akashambulia Yuda na kuweka ngome katika mji wa Rama ili kumzuia yeyote asitoke wala kuingia katika nchi ya Mfalme Asa wa Yuda. Kisha Asa akachukua fedha yote na dhahabu zilizokuwa zimeachwa katika hazina za Hekalu la Mwenyezi Mungu na katika jumba lake la kifalme. Kisha akawakabidhi maafisa wake na kuwatuma kwa Ben-Hadadi mwana wa Tabrimoni, mwana wa Hezioni, mfalme wa Aramu, aliyekuwa akitawala Dameski. Akasema, “Na tufanye mkataba kati yangu na wewe, kama ilivyokuwa kati ya baba yangu na baba yako. Tazama, nimekuletea zawadi ya fedha na dhahabu. Sasa vunja mkataba wako na Baasha, mfalme wa Israeli ili aniondokee.” Ben-Hadadi akakubaliana na Mfalme Asa na kutuma majemadari wa majeshi yake dhidi ya miji ya Israeli. Akaishinda miji ya Iyoni, Dani, Abel-Beth-Maaka na Kinerethi yote, pamoja na Naftali. Baasha aliposikia jambo hili, akasimamisha ujenzi wa Rama, akaenda kuishi Tirsa. Kisha Mfalme Asa akatoa amri kwa Yuda yote, pasipo kumwacha hata mmoja, kubeba mawe na mbao kutoka Rama, ambazo Baasha alikuwa akizitumia huko. Mfalme Asa akazitumia kujengea Geba iliyo Benyamini na Mispa. Kwa matukio yote ya utawala wa Asa, mafanikio yake yote, yote aliyofanya na miji aliyoijenga, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Hata hivyo, katika uzee wake alishikwa na ugonjwa wa miguu. Kisha Asa akalala na baba zake, naye akazikwa pamoja nao katika mji wa Daudi, baba yake. Naye Yehoshafati mwanawe akawa mfalme baada yake.