Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Fal 15:9-24

1 Fal 15:9-24 SUV

Mwaka wa ishirini wa Yeroboamu mfalme wa Israeli, Asa alianza kutawala juu ya Yuda. Akatawala miaka arobaini na mmoja huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Maaka, binti Absalomu. Basi, Asa akafanya yaliyo mema machoni pa Mungu, kama alivyofanya babaye Daudi. Akawafukuza mahanithi katika nchi, akaziondoa sanamu zote walizozifanya baba zake. Hata na Maaka, mamaye, akamwondolea daraja yake asiwe malkia, kwa kuwa amefanya sanamu ya kuchukiza kwa Ashera; basi Asa akaikata sanamu yake akaiteketeza penye kijito cha Kidroni. Lakini mahali pa juu hapakuondoshwa; ila moyo wake Asa ulikuwa mkamilifu kwa BWANA siku zake zote. Akavileta vile vitu alivyovitakasa baba yake, na vile alivyovitakasa yeye mwenyewe, katika nyumba ya BWANA, fedha; na dhahabu, na vyombo. Kulikuwa na vita kati ya Asa na Baasha mfalme wa Israeli siku zao zote. Kisha, Baasha mfalme wa Israeli akaondoka juu ya Yuda, akaujenga Rama, ili asimwache mtu ye yote kutoka wala kuingia kwa Asa mfalme wa Yuda. Ndipo Asa akazitwaa fedha zote na dhahabu zilizosalia katika hazina za nyumba ya BWANA, na hazina za nyumba ya mfalme, akazitia mikononi mwa watumishi wake; mfalme Asa akawatuma kwa Ben-hadadi, mwana wa Tabrimoni, mwana wa Hezioni, mfalme wa Shamu, aliyekaa Dameski, akasema, Tumepatana mimi nawe, na baba yangu na baba yako; angalia, nimekuletea zawadi, fedha na dhahabu; basi nenda, uyavunje mapatano yako na Baasha mfalme wa Israeli, ili aniondokee mimi. Naye Ben-hadadi akamsikiliza mfalme Asa, akawatuma wakuu wa majeshi yake juu ya miji ya Israeli, akapiga Iyoni, na Dani, na Abel-beth-maaka na Kinerothi yote, na nchi yote ya Naftali. Ikawa Baasha aliposikia habari hiyo akaacha kuujenga Rama, akaenda akakaa Tirza. Ndipo mfalme Asa akatangaza kwa Yuda pia; asiachiliwe mtu; nao wakayachukua mawe ya Rama na miti yake, aliyoijengea Baasha; naye mfalme Asa akajenga kwa vitu hivyo Geba wa Benyamini na Mispa. Na mambo yote ya Asa yaliyosalia, na nguvu zake zote, na yote aliyoyafanya, na miji aliyoijenga, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda? Lakini alipokuwa mzee alikuwa na ugonjwa wa miguu. Asa akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze mjini mwa Daudi baba yake. Na Yehoshafati mwanawe akatawala mahali pake.