Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 7:40-51

1 Wafalme 7:40-51 NEN

Pia akatengeneza masinia, masepetu na mabakuli ya kunyunyizia. Kwa hiyo Huramu akakamilisha kazi zote katika Hekalu la BWANA kama vile Mfalme Solomoni alikuwa amemwagiza, yaani: nguzo mbili; mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo; nyavu mbili za kupamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo; makomamanga 400 kwa ajili ya hizo nyavu mbili (safu mbili za makomamanga kwa kila wavu, yakipamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo); vitako kumi pamoja na masinia yake kumi; ile Bahari ya chuma na yale mafahali kumi na wawili chini yake; masufuria, masepetu na mabakuli ya kunyunyizia. Vyombo hivi vyote ambavyo Huramu alimtengenezea Mfalme Solomoni kwa ajili ya Hekalu la BWANA vilikuwa vya shaba iliyongʼarishwa. Mfalme akaamuru wavisubu katika kalibu ya udongo wa mfinyanzi katika uwanda wa Yordani ulio kati ya Sukothi na Sarethani. Solomoni akaviacha vitu hivi vyote bila kupima uzani wake, kwa sababu vilikuwa vingi sana hivi kwamba uzito wa shaba haungekadirika. Solomoni pia akatengeneza samani zote zilizokuwa ndani ya Hekalu la BWANA: madhabahu ya dhahabu; meza ya dhahabu za kuweka mikate ya Wonyesho; vinara vya taa vya dhahabu safi (vitano upande wa kuume na vitano upande wa kushoto, mbele ya Patakatifu pa Patakatifu); kazi ya maua ya dhahabu na taa na makoleo; masinia ya dhahabu safi, mikasi ya kusawazishia tambi, mabakuli ya kunyunyizia, vyano na vyetezo; na bawaba za dhahabu kwa ajili ya milango ya chumba cha ndani sana, yaani Patakatifu pa Patakatifu, na pia kwa ajili ya milango ya ukumbi mkuu wa Hekalu. Hivyo Mfalme Solomoni alipomaliza kazi ya Hekalu la BWANA, akaviingiza ndani vile vitu ambavyo Daudi baba yake alikuwa ameviweka wakfu: yaani fedha, dhahabu na samani; kisha akaviweka katika hazina za Hekalu la BWANA.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 1 Wafalme 7:40-51