Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 7:40-51

1 Wafalme 7:40-51 Biblia Habari Njema (BHN)

Hiramu alitengeneza pia vyungu, sepetu na mabirika. Basi, Hiramu akamaliza kazi aliyoamriwa na mfalme Solomoni kuhusu nyumba ya Mwenyezi-Mungu: Nguzo mbili, mabakuli mawili ya taji zilizowekwa juu ya nguzo, na nyavu mbili kwa ajili ya kufunika hizo taji mbili, mifano ya makomamanga 400 kwa ajili ya nyavu hizo mbili, safu mbili za makomamanga kwa kila wavu ili kupamba zile taji mbili zilizokuwa juu ya nguzo. Hali kadhalika, alitengeneza magari kumi, na vishikio kumi katika magari hayo; na tangi lile moja na sanamu za mafahali kumi na wawili, chini ya hilo tangi. Halafu vile vyungu, sepetu na mabirika, vyombo hivyo vyote vilivyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu ambavyo Hiramu alimtengenezea mfalme Solomoni, vilikuwa vya shaba iliyongarishwa. Vitu hivyo vyote mfalme alivitengeneza katika uwanda wa Yordani, sehemu ya udongo wa mfinyanzi iliyokuwa kati ya Sukothi na Sarethani. Solomoni hakupima uzani wa vifaa hivi vyote kwa kuwa vilikuwa vingi sana, na kwa sababu uzani wa shaba haukujulikana. Solomoni alitengeneza vifaa vyote vilivyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu: Madhabahu ya dhahabu, meza ya dhahabu kwa ajili ya mikate ya kuwekwa mbele ya Mungu, vinara vya taa vya dhahabu safi vilivyowekwa mbele ya mahali patakatifu sana, vitano upande wa kusini na vitano upande wa kaskazini; maua, taa, koleo, vyote vikiwa vya dhahabu; vikombe, makasi ya kukatia tambi za mishumaa, mabakuli, vyetezo vya kuwekea ubani, miiko ya kuchukulia moto, vyote vya dhahabu safi; bawaba za milango ya sehemu ya ndani kabisa ya nyumba – pale mahali patakatifu sana – na bawaba za milango ya ukumbi wa ibada wa hekalu bawaba zote za dhahabu. Basi, mfalme Solomoni akamaliza kazi zote zilizohusu nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Kisha Solomoni akaleta mali yote ambayo baba yake Daudi, alikuwa ameiweka wakfu, yaani: Fedha, dhahabu na vyombo; akaiweka katika hazina za nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

1 Wafalme 7:40-51 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Tena Huramu akazifanya birika, na majembe, na mabakuli. Hivyo Huramu akazimaliza kazi zote alizomfanyia mfalme Sulemani katika nyumba ya BWANA; zile nguzo mbili, na vimbe mbili za taji zilikuwa juu ya nguzo; na nyavu mbili za kuzifunika hizo vimbe mbili za taji zilizokuwa juu ya nguzo; na makomamanga mia nne ya zile nyavu mbili; safu mbili za makomamanga kwa kila wavu, kuzifunika hizo vimbe mbili za taji zilizokuwa juu ya nguzo; na yale matako kumi, na birika kumi juu ya matako; na ile bahari moja, na ng’ombe kumi na wawili chini ya ile bahari; na masufuria, na majembe, na mabakuli; hata vyombo hivyo vyote, Huramu alivyomfanyia mfalme Sulemani, katika nyumba ya BWANA, vyote vilikuwa vya shaba iliyosuguliwa. Katika uwanda wa Yordani ndipo mfalme alipovisubu, katika udongo mzito kati ya Sukothi na Sarethani. Sulemani akaviacha vyombo vyote visipimwe kwa kuwa vilikuwa vingi mno; wala uzito wa shaba haukujulikana. Sulemani akavifanya vyombo vyote vilivyokuwamo nyumbani mwa BWANA; madhabahu ya dhahabu, na ile meza iliyokuwa na mikate ya wonyesho juu yake ilikuwa ya dhahabu; na vinara vya taa, vitano upande wa kuume, na vitano upande wa kushoto, mbele ya chumba cha ndani, vya dhahabu safi; na maua, na taa, na koleo ya dhahabu; na vikombe, na makasi, na mabakuli, na miiko, na vyetezo, vya dhahabu safi; na bawaba za dhahabu, za milango ya nyumba ya ndani, yaani, patakatifu pa patakatifu, na za milango ya nyumba, ndiyo hekalu. Hivyo ikamalizika kazi yote Sulemani mfalme aliyoifanya katika nyumba ya BWANA. Sulemani akaviingiza vile vitu alivyovitakasa Daudi baba yake, yaani, fedha, na dhahabu, na vyombo; akavitia ndani ya hazina za nyumba ya BWANA.

1 Wafalme 7:40-51 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Pia akatengeneza masinia, masepetu na mabakuli ya kunyunyizia. Kwa hiyo Huramu akakamilisha kazi zote katika Hekalu la BWANA kama vile Mfalme Solomoni alikuwa amemwagiza, yaani: nguzo mbili; mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo; nyavu mbili za kupamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo; makomamanga 400 kwa ajili ya hizo nyavu mbili (safu mbili za makomamanga kwa kila wavu, yakipamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo); vitako kumi pamoja na masinia yake kumi; ile Bahari ya chuma na yale mafahali kumi na wawili chini yake; masufuria, masepetu na mabakuli ya kunyunyizia. Vyombo hivi vyote ambavyo Huramu alimtengenezea Mfalme Solomoni kwa ajili ya Hekalu la BWANA vilikuwa vya shaba iliyongʼarishwa. Mfalme akaamuru wavisubu katika kalibu ya udongo wa mfinyanzi katika uwanda wa Yordani ulio kati ya Sukothi na Sarethani. Solomoni akaviacha vitu hivi vyote bila kupima uzani wake, kwa sababu vilikuwa vingi sana hivi kwamba uzito wa shaba haungekadirika. Solomoni pia akatengeneza samani zote zilizokuwa ndani ya Hekalu la BWANA: madhabahu ya dhahabu; meza ya dhahabu za kuweka mikate ya Wonyesho; vinara vya taa vya dhahabu safi (vitano upande wa kuume na vitano upande wa kushoto, mbele ya Patakatifu pa Patakatifu); kazi ya maua ya dhahabu na taa na makoleo; masinia ya dhahabu safi, mikasi ya kusawazishia tambi, mabakuli ya kunyunyizia, vyano na vyetezo; na bawaba za dhahabu kwa ajili ya milango ya chumba cha ndani sana, yaani Patakatifu pa Patakatifu, na pia kwa ajili ya milango ya ukumbi mkuu wa Hekalu. Hivyo Mfalme Solomoni alipomaliza kazi ya Hekalu la BWANA, akaviingiza ndani vile vitu ambavyo Daudi baba yake alikuwa ameviweka wakfu: yaani fedha, dhahabu na samani; kisha akaviweka katika hazina za Hekalu la BWANA.

1 Wafalme 7:40-51 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Tena Huramu akazifanya birika, na majembe, na mabakuli. Hivyo Huramu akazimaliza kazi zote alizomfanyia mfalme Sulemani katika nyumba ya BWANA; zile nguzo mbili, na mabakuli mawili ya mataji yalikuwa juu ya nguzo; na nyavu mbili za kuvifunika hivyo viumbe viwili vya mataji yaliyokuwa juu ya nguzo; na makomamanga mia nne ya zile nyavu mbili; safu mbili za makomamanga kwa kila wavu, kuyafunika nayo mabakuli mawili ya mataji yaliyokuwa juu ya nguzo; na vile vitako kumi, na birika kumi juu ya vitako; na ile bahari moja, na ng'ombe kumi na wawili chini ya ile bahari; na masufuria, na majembe, na mabeseni; hata vyombo hivyo vyote, Huramu alivyomfanyia mfalme Sulemani, katika nyumba ya BWANA, vyote vilikuwa vya shaba iliyosuguliwa. Katika uwanda wa Yordani ndipo mfalme alipovisubu, katika udongo mzito kati ya Sukothi na Sarethani. Sulemani akaviacha vyombo vyote visipimwe kwa kuwa vilikuwa vingi mno; wala uzito wa shaba haukujulikana. Sulemani akavitengeneza vyombo vyote vilivyokuwamo nyumbani mwa BWANA; madhabahu ya dhahabu, na ile meza iliyokuwa na mikate ya wonyesho juu yake ilikuwa ya dhahabu; na vinara vya taa, vitano upande wa kulia, na vitano upande wa kushoto, mbele ya chumba cha ndani, vya dhahabu safi; na maua, na taa, na koleo ya dhahabu; na vikombe, na makasi, na mabakuli, na miiko, na vyetezo, vya dhahabu safi; na bawaba za dhahabu, za milango ya nyumba ya ndani, yaani, patakatifu pa patakatifu, na za milango ya nyumba, ndiyo hekalu. Hivyo kazi yote aliyoifanya mfalme Sulemani katika nyumba ya BWANA ikamalizika. Sulemani akaviingiza vile vitu alivyovitakasa Daudi baba yake, yaani, fedha, na dhahabu, na vyombo; akavitia ndani ya hazina za nyumba ya BWANA.