1 Samweli 13
13
Samweli amkemea Sauli
1Sauli alikuwa na umri wa miaka thelathini, alipokuwa mfalme, akatawala Israeli miaka arobaini na mbili.
2Sauli alichagua watu elfu tatu kutoka Israeli; miongoni mwa hao, watu elfu mbili walikuwa naye huko Mikmashi na katika nchi ya vilima ya Betheli; nao watu elfu moja walikuwa na Yonathani huko Gibea ya Benyamini. Watu waliosalia aliwarudisha nyumbani mwao.
3Yonathani akashambulia ngome ya Wafilisti huko Geba, nao Wafilisti wakapata habari hizo. Kisha Sauli akaamuru tarumbeta ipigwe nchi yote na kusema, “Waebrania na wasikie!” 4Hivyo Israeli wote wakasikia habari kwamba: “Sauli ameshambulia ngome ya Wafilisti, na sasa Israeli wamekuwa harufu mbaya kwa Wafilisti.” Basi watu waliitwa kuungana na Sauli huko Gilgali.
5Wafilisti wakakusanyika ili kupigana na Israeli, wakiwa na magari ya vita elfu tatu, waendesha magari ya vita elfu sita, na askari wa miguu wengi kama mchanga wa ufuoni mwa bahari. Walipanda na kupiga kambi huko Mikmashi, mashariki mwa Beth-Aveni. 6Waisraeli walipoona kuwa hali yao ni ya hatari na kuwa jeshi lao limesongwa sana, wakajificha katika mapango na katika vichaka, katika miamba, kwenye mashimo na kwenye mahandaki. 7Hata baadhi ya Waebrania wakavuka Yordani hadi nchi ya Gadi na Gileadi.
Sauli akabaki huko Gilgali, navyo vikosi vyote vilivyokuwa pamoja naye vilikuwa vikitetemeka kwa hofu. 8Akangoja kwa siku saba, muda uliowekwa na Samweli; lakini Samweli hakuja Gilgali, nao watu wa Sauli wakaanza kutawanyika. 9Basi akasema, “Nileteeni hapa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani.” Naye Sauli akatoa sadaka ya kuteketezwa. 10Mara alipomaliza kutoa hiyo sadaka, Samweli akatokea, naye Sauli akaondoka kwenda kumlaki.
11Samweli akamuuliza, “Umefanya nini?”
Sauli akajibu, “Nilipoona kwamba watu wanatawanyika, na kwamba hukuja wakati uliopangwa na kwamba Wafilisti walikuwa wakikusanyika huko Mikmashi, 12nikawaza, ‘Sasa Wafilisti watateremka dhidi yangu huko Gilgali nami sijaomba kibali kwa Mwenyezi Mungu.’ Hivyo nikalazimika kutoa sadaka ya kuteketezwa.”
13Samweli akamwambia Sauli, “Umetenda kwa upumbavu. Hukuyashika maagizo ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako, aliyokupa. Kama ungetii, angeudumisha ufalme wako juu ya Israeli kwa wakati wote. 14Lakini sasa ufalme wako hautadumu; Mwenyezi Mungu amemtafuta mtu aupendezaye moyo wake, na amemchagua awe kiongozi wa watu wake, kwa sababu hukuyatii maagizo ya Mwenyezi Mungu.”
15Kisha Samweli akaondoka Gilgali, akapanda Gibea ya Benyamini, naye Sauli akawahesabu watu aliokuwa nao. Jumla yao walikuwa watu mia sita.
Israeli bila silaha
16Sauli, mwanawe Yonathani na watu waliokuwa pamoja nao walikuwa wakiishi huko Gibea ya Benyamini, wakati Wafilisti wakiwa wamepiga kambi huko Mikmashi. 17Makundi ya wavamiaji walikuja kutoka kambi ya Wafilisti katika vikosi vitatu. Kikosi kimoja kilielekea Ofra karibu na Shuali, 18kikosi kingine kilielekea Beth-Horoni, nacho kikosi cha tatu kilielekea kwenye nchi ya mpakani ielekeayo Bonde la Seboimu linalotazamana na jangwa.
19Hapakuwa na mhunzi ambaye angeweza kupatikana katika nchi yote ya Israeli, kwa sababu Wafilisti walikuwa wamesema, “Waebrania wasije wakatengeneza panga au mikuki!” 20Hivyo Waisraeli wote waliteremka kwa Wafilisti ili kila mtu kunoa plau yake, jembe lake, shoka lake, au mundu wake. 21Bei ilikuwa fedha theluthi mbili za shekeli#13:21 Theluthi mbili za shekeli za fedha ni sawa na gramu 8. kunoa majembe ya plau na majembe ya mkono, na theluthi moja ya shekeli#13:21 Theluthi moja ya shekeli ya fedha ni sawa na gramu 4. kunoa uma, na shoka, na mchokoo.
22Kwa hiyo siku ya vita hakuna askari yeyote kambini na Sauli na Yonathani aliyekuwa na upanga wala mkuki mkononi mwake; Sauli na mwanawe Yonathani tu ndio walikuwa navyo.
Yonathani awashambulia Wafilisti
23Basi kikosi cha Wafilisti kilikuwa kimetoka kuelekea njia iendayo Mikmashi.
Iliyochaguliwa sasa
1 Samweli 13: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.