Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 2

2
Maombi ya Hana
1Kisha Hana akaomba na kusema:
“Moyo wangu wamshangilia Mwenyezi Mungu,
katika Mwenyezi Mungu pembe#2:1 pembe inawakilisha nguvu yangu imeinuliwa juu.
Kinywa changu chajisifu juu ya adui zangu,
kwa kuwa naufurahia wokovu wako.
2“Hakuna yeyote aliye mtakatifu kama Mwenyezi Mungu,
hakuna mwingine zaidi yako;
hakuna Mwamba kama Mungu wetu.
3“Msiendelee kusema kwa kiburi hivyo
wala msiache vinywa vyenu kunena kwa kiburi,
kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mungu ajuaye,
na yeye hupima matendo.
4“Pinde za mashujaa zimevunjika,
lakini wale wanaojikwaa wamevikwa nguvu.
5Wale waliokuwa na chakula tele wamejikodisha wenyewe
ili kupata chakula,
lakini wale waliokuwa na njaa
hawana njaa tena.
Mwanamke yule aliyekuwa tasa
amezaa watoto saba,
lakini yule aliyekuwa na wana wengi
amedhoofika.
6“Mwenyezi Mungu huua na huhuisha;
yeye hushusha hadi kaburini#2:6 Kaburini maana yake ni Kuzimu; kwa Kiebrania ni Sheol. na hufufua.
7Mwenyezi Mungu humfanya mtu maskini naye hutajirisha,
hushusha na hukweza.
8Humwinua maskini kutoka mavumbini
na humwinua mhitaji kutoka lundo la majivu;
huwaketisha pamoja na wakuu,
na kuwafanya warithi kiti cha utawala cha heshima.
“Kwa kuwa misingi ya dunia ni ya Mwenyezi Mungu;
juu yake ameuweka ulimwengu.
9Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake,
lakini waovu watanyamazishwa kwenye giza.
“Si kwa nguvu mtu hushinda;
10wale wampingao Mwenyezi Mungu
wataharibiwa kabisa.
Atapiga radi dhidi yao kutoka mbinguni;
Mwenyezi Mungu ataihukumu miisho ya dunia.
“Atampa nguvu mfalme wake,
na kuitukuza pembe
ya mpakwa mafuta wake.”
11Kisha Elkana akaenda nyumbani Rama, lakini mtoto akahudumu mbele za Mwenyezi Mungu chini ya kuhani Eli.
Wana Waovu wa Eli
12Wana wa Eli walikuwa watu waovu kabisa, hawakumheshimu Mwenyezi Mungu. 13Basi ilikuwa desturi ya makuhani pamoja na watu kwamba kila mara yeyote anapotoa dhabihu na huku nyama ikiwa inachemshwa, mtumishi wa kuhani angekuja na uma wenye meno matatu mkononi mwake. 14Angeutumbukiza huo uma kwenye sufuria au birika au sufuria kubwa au chungu, naye kuhani angejichukulia chochote uma ungekileta. Hivi ndivyo walivyowatendea Waisraeli wote waliokuja Shilo. 15Lakini hata kabla mafuta ya mnyama hayajachomwa, mtumishi wa kuhani angekuja na kusema kwa mtu aliyekuwa akitoa dhabihu, “Mpe kuhani nyama akaoke, kwani hatapokea nyama iliyochemshwa kutoka kwako, ila iliyo mbichi tu.”
16Mtu yule akimwambia, “Mafuta ya mnyama na yachomwe kwanza, ndipo uchukue chochote unachotaka,” mtumishi angejibu, “Hapana, nipe sasa; kama hunipi, nitaichukua kwa nguvu.”
17Hii dhambi ya hawa vijana ilikuwa kubwa sana machoni pa Mwenyezi Mungu, kwa kuwa waliitendea dhabihu ya Mwenyezi Mungu kwa dharau.
18Lakini Samweli alikuwa akihudumu mbele za Mwenyezi Mungu, kijana akivaa kizibau cha kitani. 19Kila mwaka mama yake alimshonea joho dogo na kumpelekea alipokwea pamoja na mumewe kutoa dhabihu ya mwaka. 20Eli alikuwa akiwabariki Elkana na mkewe, akisema, “Mwenyezi Mungu na akupe watoto kwa mwanamke huyu ili kuchukua nafasi ya yule aliyekuwa amemwomba na akamtoa kwa Mwenyezi Mungu.” Kisha wakawa wanaenda nyumbani. 21Mwenyezi Mungu akawa mwenye neema kwa Hana, naye akapata mimba akazaa wana wa kiume watatu na binti wawili. Wakati huo, kijana Samweli akaendelea kukua mbele za Mwenyezi Mungu.
22Basi Eli, aliyekuwa mzee sana, alisikia kuhusu kila kitu ambacho wanawe walikuwa wakiwafanyia Israeli wote na jinsi walivyokutana kimwili na wanawake waliohudumu kwenye ingilio la Hema la Kukutania. 23Hivyo akawaambia, “Kwa nini mmefanya mambo kama haya? Nimesikia kutoka kwa watu wote kuhusu haya matendo yenu maovu. 24Sivyo, wanangu, hii si habari nzuri ninayosikia ikienea miongoni mwa watu wa Mwenyezi Mungu. 25Mtu akifanya dhambi dhidi ya mtu mwenzake, mtu mwingine aweza kumwombea kwa Mungu, lakini kama mtu akimfanyia Mungu dhambi, ni nani atakayemwombea?” Hata hivyo wanawe hawakusikia maonyo ya baba yao, kwa sababu Mwenyezi Mungu alitaka kuwaua.
26Naye kijana Samweli akaendelea kukua katika kimo, akimpendeza Mwenyezi Mungu na wanadamu.
Unabii dhidi ya nyumba ya Eli
27Basi mtu wa Mungu akaja kwa Eli na kumwambia, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Je, sikujifunua waziwazi kwa nyumba ya baba yako wakati walikuwa huko Misri chini ya Farao? 28Nilimchagua baba yako kati ya makabila yote ya Israeli kuwa kuhani wangu, kukwea kwenye madhabahu yangu, kufukiza uvumba na kuvaa kizibau mbele yangu. Pia niliwapa nyumba ya baba yako sadaka zote zilizotolewa kwa moto na Waisraeli. 29Kwa nini unadharau dhabihu zangu na sadaka nilizoziamuru kwa ajili ya makao yangu? Kwa nini unawaheshimu wanao kuliko mimi kwa kujinenepesha wenyewe kwa kula sehemu zilizo bora za kila sadaka zinazotolewa na watu wangu wa Israeli?’
30“Kwa hiyo, Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asema: ‘Niliahidi kuwa nyumba yako na nyumba ya baba yako wangehudumu mbele zangu milele.’ Lakini sasa Mwenyezi Mungu anasema: ‘Jambo hili na liwe mbali nami! Wale wanaoniheshimu nitawaheshimu, wale wanaonidharau mimi watadharauliwa. 31Wakati unakuja nitakapozipunguza nguvu zenu na nguvu ya nyumba ya baba yenu, ili pasiwepo mtu katika jamaa yenu atakayeishi kuuona uzee, 32nanyi mtaona huzuni katika makao yangu. Ingawa Israeli watatendewa mema, katika jamaa yenu kamwe hapatakuwa na mtu atakayeishi hadi kuwa mzee. 33Kila mmoja wenu ambaye sitamkatilia mbali kutoka madhabahuni pangu atabakizwa tu kupofusha macho yenu kwa machozi na kuihuzunisha mioyo yenu, nao wazao wenu wote watakufa watakapokuwa wamefikia umri wa kustawi.
34“ ‘Kile kitakachotokea kwa wanao wawili, Hofni na Finehasi, kitakuwa ishara kwako. Wote wawili watakufa katika siku moja. 35Mimi mwenyewe nitajiinulia kuhani mwaminifu, ambaye atafanya sawasawa na kile kilichoko moyoni mwangu na akilini mwangu. Nitaiimarisha nyumba yake ya ukuhani, naye atahudumu mbele ya mpakwa mafuta wangu daima. 36Kisha kila mmoja aliyeachwa katika jamaa yenu atakuja na kusujudu mbele yake kwa ajili ya kipande cha fedha na ganda la mkate, akisema, “Niteue katika baadhi ya ofisi ya ukuhani ili niweze kupata chakula.” ’ ”

Iliyochaguliwa sasa

1 Samweli 2: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia