1 Samweli Utangulizi
Utangulizi
Katika andiko la Kiebrania, vitabu vya 1 Samweli na 2 Samweli vilikuwa kitabu kimoja. Kugawanyika na kuwa vitabu viwili kulifanyika katika tafsiri ya “Septuagint” (yaani Agano la Kale la Kiyunani), ambayo iliviita “Kitabu cha Kwanza na cha Pili cha Ufalme.” Kitabu cha 1 Samweli kinaanza kuelezea kuzaliwa kwa Samweli na mafundisho yake hekaluni. Kinaelezea jinsi alivyoiongoza Israeli kama nabii, kuhani na mwamuzi.
Wakati wana wa Israeli walitaka kuwa na mfalme, Samweli, kwa uongozi wa Mungu, alimtia Sauli mafuta kuwa mfalme wa kwanza wa Waisraeli. Lakini Sauli aliacha kumtii Mungu, naye Mungu akamkataa asiendelee kuwa mfalme. Kisha Mungu akamwongoza Samweli kumtia Daudi mafuta kwa siri kuwa mfalme badala ya Sauli. Sehemu ya kitabu hiki iliyobaki inaelezea mapambano kati ya Sauli na Daudi.
Mwandishi
Inawezekana ni Samweli hadi mahali kifo chake kimenakiliwa; pia maandishi ya manabii Nathani na Gadi yamejumuishwa.
Kusudi
Kitabu cha 1 Samweli kinaonyesha historia ya Israeli chini ya uongozi wa waamuzi, kuonyesha mabadiliko ya uongozi katika Israeli kutoka mfumo wa uongozi wa waamuzi kwenda kwa uongozi wa wafalme, na kuweka kumbukumbu za maisha ya watu ambao kupitia kwao Masiya angezaliwa.
Mahali
Katika nchi ya Israeli.
Tarehe
Wakati kitabu hiki kiliandikwa haujulikani.
Wahusika Wakuu
Eli, Hana, Samweli, Sauli, Yonathani, na Daudi.
Wazo Kuu
Kuanzishwa kwa ufalme wa Waisraeli, na vile huo ufalme uliendelea chini ya mfalme Sauli na Daudi.
Mambo Muhimu
Kitabu cha 1 Samweli kinaonyesha kumomonyoka kwa maadili kwa waamuzi wakati wa Samweli; mwanzo wa kushindwa kwa ufalme wakati wa Sauli; Daudi kutiwa mafuta na kujaribiwa kwa uzoefu wake; na pia, mwisho wa Sauli.
Mgawanyo
Eli, kuhani na mwamuzi, na Samweli (1:1–7:17)
Samweli na Sauli, kiongozi wa Israeli (8:1–15:35)
Mfalme Sauli, na Daudi (16:1–31:13).
Iliyochaguliwa sasa
1 Samweli Utangulizi: NEN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.
Used with Permission. All Rights Reserved Worldwide.