3
Timotheo atumwa Thesalonike
1Kwa hivyo tulipokuwa hatuwezi kuvumilia zaidi, tuliamua tubaki Athene peke yetu. 2Tukamtuma Timotheo ambaye ni ndugu yetu na mtumishi mwenzetu wa Mungu katika kuieneza Injili ya Al-Masihi, aje kuwaimarisha na kuwatia moyo katika imani yenu, 3ili mtu yeyote asifadhaishwe na mateso haya. Mnajua vyema kwamba tumewekewa hayo mateso. 4Kwa kweli, tulipokuwa pamoja nanyi tuliwaambia mara kwa mara kwamba tutateswa na imekuwa hivyo kama mnavyojua. 5Kwa sababu hii niliposhindwa kuvumilia zaidi, nilimtuma mtu ili nipate habari za imani yenu. Niliogopa kwamba kwa njia fulani yule mjaribu asiwe amewajaribu, nasi tukawa tumejitaabisha bure.
Taarifa ya Timotheo ya kutia moyo
6Lakini Timotheo amerejea kwetu hivi sasa kutoka kwenu, na ameleta habari njema kuhusu imani yenu na upendo wenu. Ametuambia kwamba siku zote mnatukumbuka kwa wema, na kwamba mna shauku ya kutuona kama vile sisi tulivyo na shauku ya kuwaona ninyi. 7Kwa hiyo, ndugu zetu, katika dhiki na mateso yetu yote tumefarijika kwa sababu ya imani yenu. 8Sasa kwa kuwa hakika tunaishi, kwa kuwa ninyi mmesimama imara katika Bwana Isa. 9Je, tutawezaje kumshukuru Mungu kiasi cha kutosha kwa ajili yenu, kutokana na furaha tuliyo nayo mbele za Mungu wetu kwa sababu yenu? 10Usiku na mchana tunaomba kwa bidii ili tupate kuwaona tena na kujaza kile kilichopungua katika imani yenu.
11Basi Mungu wetu na Baba yetu mwenyewe na Bwana wetu Isa atengeneze njia ya sisi kuja kwenu. 12Bwana Isa na auongeze upendo wenu na kuuzidisha kati yenu na kwa wengine wote, kama vile tulivyo na upendo mwingi kwenu. 13Tunamwomba Mungu aimarishe mioyo yenu ili msiwe na lawama katika utakatifu mbele za Mungu wetu aliye Baba yetu wakati wa kuja kwake Bwana wetu Isa pamoja na watakatifu wote.