4
Maisha yanayompendeza Mwenyezi Mungu
1Na kuhusu mambo mengine, ndugu, tuliwafundisha jinsi ya kuishi ili kumpendeza Mungu, kama vile mnavyoishi. Sasa tunawaomba na kuwasihi katika Bwana Isa mfanye hivi zaidi na zaidi. 2Kwa kuwa mnajua maagizo tuliyowapa kwa mamlaka ya Bwana Isa.
3Mapenzi ya Mungu ni ninyi mtakaswe, ili mjiepushe na uasherati, 4na kila mmoja wenu ajifunze kuutawala mwili wake mwenyewe katika utakatifu na heshima, 5bali si kwa tamaa mbaya kama watu wa Mataifa wasiomjua Mungu. 6Katika jambo hili mtu asimkosee ndugu yake wala kumlaghai. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mlipiza kisasi katika mambo haya yote, kama vile tulivyokwisha kuwaambia mapema na kuwaonya vikali. 7Kwa maana Mungu hakutuitia uchafu, bali utakatifu. 8Kwa hiyo, mtu yeyote anayekataa mafundisho haya hamkatai mwanadamu, bali anamkataa Mungu anayewapa ninyi Roho wake Mtakatifu.
9Sasa kuhusu upendo wa ndugu hamna haja mtu yeyote kuwaandikia, kwa maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana. 10Nanyi kwa kweli mnawapenda ndugu wote katika Makedonia nzima. Lakini ndugu, tunawasihi mzidi sana kuwapenda.
11Jitahidini kuishi maisha ya utulivu, kila mtu akijishughulisha na mambo yake mwenyewe na kufanya kazi kwa mikono yake, kama vile tulivyowaagiza, 12ili maisha yenu ya kila siku yajipatie heshima kutoka kwa watu walio nje, ili msimtegemee mtu yeyote.
Kurudi kwake Bwana Isa
13Lakini ndugu, hatutaki mkose kujua kuhusu wale waliolala katika mauti, ili msihuzunike kama watu wengine wasiokuwa na tumaini. 14Tunaamini kwamba Isa alikufa na kufufuka. Na kwa hivyo, tunaamini kwamba Mungu atawaleta pamoja naye wale waliolala katika Isa. 15Kulingana na neno la Bwana Isa mwenyewe, tunawaambia kwamba sisi ambao bado tuko hai, tuliobaki hadi kuja kwake Bwana Isa, hakika hatutawatangulia waliolala katika mauti. 16Kwa maana Bwana Isa mwenyewe atashuka kutoka mbinguni, akitoa amri kwa sauti kuu, pamoja na sauti ya malaika mkuu, na sauti ya tarumbeta ya Mungu. Nao waliokufa wakiwa katika Al-Masihi watafufuka kwanza. 17Baada ya hilo sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili kumlaki Bwana Isa hewani, hivyo tutakuwa pamoja na Bwana Isa milele. 18Kwa hiyo farijianeni kwa maneno haya.