Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wakorintho 1:3-11

2 Wakorintho 1:3-11 NENO

Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Isa Al-Masihi, Baba wa huruma na Mungu wa faraja yote. Yeye hutufariji katika taabu zetu, ili tuweze kuwafariji walio katika taabu yoyote kwa faraja ambayo sisi wenyewe tumepokea kutoka kwa Mungu. Kama vile mateso ya Al-Masihi yanavyozidi maishani mwetu, hivyo ndivyo faraja yetu inavyofurika kupitia kwa Al-Masihi. Ikiwa tunataabika, ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu; tukifarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu, iwaleteayo saburi ya mateso yale yale yanayotupata. Nalo tumaini letu kwenu ni thabiti, kwa sababu tunajua kwamba kama vile mnavyoshiriki mateso yetu, ndivyo pia mnavyoshiriki faraja yetu. Ndugu wapendwa, hatutaki mkose kujua kuhusu zile taabu tulizopata huko jimbo la Asia. Kwa maana tulilemewa na mizigo sana, kiasi cha kushindwa kuvumilia, hata tulikata tamaa ya kuishi. Kwa kweli, mioyoni mwetu tulihisi tumekabiliwa na hukumu ya kifo, ili tusijitegemee sisi wenyewe bali tumtegemee Mungu afufuaye wafu. Yeye ametuokoa kwenye hatari kubwa ya kifo, na atatuokoa tena. Kwake yeye tumeweka tumaini letu kwamba ataendelea kutuokoa, kama vile mnavyoungana kusaidiana nasi katika maombi. Hivyo wengi watatoa shukrani kwa niaba yetu kwa ajili ya baraka za neema tulizopata kwa majibu ya maombi ya wengi.