2 Wafalme 13:14-25
2 Wafalme 13:14-25 NEN
Wakati huu, Elisha alikuwa anaumwa na ugonjwa ambao baadaye ulimuua. Yehoashi mfalme wa Israeli akashuka kwenda kumwona na kumlilia. Akalia, “Baba yangu! Baba yangu! Magari ya vita ya Israeli na wapanda farasi wake!” Elisha akasema, “Leta upinde na baadhi ya mishale,” naye mfalme akafanya hivyo. Elisha akamwambia mfalme wa Israeli, “Shika upinde mikononi mwako.” Alipokwisha kuichukua, Elisha akaweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme. Elisha akasema, “Fungua dirisha la mashariki,” naye akalifungua. Elisha akasema, “Piga mshale!” Naye akapiga mshale. Elisha akasema, “Mshale wa ushindi wa BWANA, mshale wa ushindi juu ya Aramu! Utawaangamiza Waaramu kabisa huko Afeki.” Kisha akasema, “Chukua mishale,” naye mfalme akaichukua. Elisha akamwambia, “Piga ardhi kwa hiyo mishale.” Akaipiga mara tatu, halafu akaacha. Mtu wa Mungu akamkasirikia na akasema, “Ungepiga chini mara tano au sita, ndipo ungeishinda Aramu na kuiangamiza kabisa. Lakini sasa utaishinda mara tatu tu.” Elisha akafa, nao wakamzika. Vikosi vya Wamoabu vilikuwa vinashambulia nchi kwa vita kila mwaka wakati wa vuli. Ikawa Waisraeli fulani walipokuwa wanamzika mtu, ghafula wakaona kikosi cha washambuliaji, basi wakaitupa ile maiti ya yule mtu ndani ya kaburi la Elisha. Wakati ile maiti ilipogusa mifupa ya Elisha, yule mtu akafufuka na kusimama kwa miguu yake. Hazaeli mfalme wa Aramu aliwatesa Israeli wakati wote wa utawala wa Yehoahazi. Lakini BWANA akawarehemu na akawahurumia, akaonyesha kujishughulisha nao kwa sababu ya Agano lake na Abrahamu, Isaki na Yakobo. Hadi leo, hajawaangamiza wala kuwafukuza mbele zake. Hazaeli mfalme wa Shamu akafa, naye Ben-Hadadi mwanawe akawa mfalme baada yake. Kisha Yehoashi mwana wa Yehoahazi akateka tena kutoka kwa Ben-Hadadi mwana wa Hazaeli ile miji aliyokuwa ameitwaa kwa vita kutoka kwa baba yake Yehoahazi. Yehoashi alimshinda mara tatu, hivyo akaweza kuiteka tena ile miji ya Waisraeli.