Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 13:14-25

2 Wafalme 13:14-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi Elisha alikuwa ameshikwa na ugonjwa wake uliomwua; naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatelemka amtazame, akamlilia mbele yake, akasema, Baba yangu! Baba yangu! Gari la Israeli na wapanda farasi wake! Elisha akamwambia, Twaa uta na mishale; naye akatwaa uta na mishale. Akamwambia mfalme wa Israeli, Weka mkono wako katika uta; naye akaweka mkono wake juu yake. Elisha akaweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme. Akasema, Lifungue dirisha linaloelekea mashariki; akalifungua. Basi Elisha akasema, Piga; akapiga. Akasema, Mshale wa BWANA wa kushinda, naam, mshale wa kushinda Shamu, kwa maana utawapiga Washami katika Afeki hata utakapowaangamiza. Akasema, Itwae mishale; akaitwaa. Akamwambia mfalme wa Israeli, Piga chini; akaipiga nchi mara tatu, akaacha. Yule mtu wa Mungu akamkasirikia, akasema, Ingalikupasa kupiga mara tano au mara sita; ndipo ungaliipiga Shamu hata kuiangamiza; bali sasa utaipiga Shamu mara tatu tu. Elisha akafa, nao wakamzika. Basi vikosi vya Wamoabi wakaingia katika nchi mwanzo wa mwaka. Ikawa, walipokuwa wakimzika mtu, angalia, waliona kikosi; wakamtupa yule mtu kaburini mwa Elisha; mara yule maiti alipoigusa mifupa ya Elisha, alifufuka, akasimama kwa miguu. Na Hazaeli mfalme wa Shamu akawaonea Israeli siku zote za Yehoahazi. Lakini BWANA akawahurumia, akawasikitikia, na kuwaangalia, kwa ajili ya agano lake na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, wala hakutaka kuwaangamiza, wala hakuwatupa usoni pake bado. Akafa Hazaeli mfalme wa Shamu, na Ben-hadadi mwanawe akatawala mahali pake. Naye Yehoashi, mwana wa Yehoahazi, akaitwaa tena mkononi mwa Ben-hadadi mwana wa Hazaeli miji ile aliyoitwaa yeye mkononi mwa Yehoahazi baba yake vitani. Mara tatu Yehoashi akamshinda, akairudisha miji ya Israeli.

2 Wafalme 13:14-25 Biblia Habari Njema (BHN)

Nabii Elisha aliugua ugonjwa mbaya sana. Alipokuwa karibu kufa, mfalme Yehoashi wa Israeli alimtembelea. Alipomfikia Elisha, alilia, akisema, “Baba yangu, baba yangu! Magari ya Israeli na wapandafarasi wake!” Elisha akamwamuru, “Hebu lete upinde na mishale!” Yehoashi akavileta. Elisha akamwambia ajitayarishe kupiga mishale. Mfalme akajitayarisha na Elisha akaiweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme. Mfalme alifuata maagizo ya nabii na kufungua dirisha ambalo lilielekea Aramu. Elisha akatoa amri “Tupa mshale!” Mara tu mfalme alipotupa mshale, nabii akasema, “Wewe ndio mshale wa Mwenyezi-Mungu, ambao kwao atapata ushindi juu ya Waaramu. Utapigana na Waaramu huko Afeka mpaka uwashinde.” Ndipo Elisha akamwambia mfalme achukue mishale mingine na kuipiga chini. Mfalme akapiga mishale chini mara tatu, kisha akaacha. Elisha alikasirika sana, akamwambia mfalme, “Mbona hukupiga mara tano au sita? Hivyo ungewaangamiza Waaramu kabisa. Lakini sasa utawashinda mara tatu tu.” Elisha alifariki, akazikwa. Kila mwaka, makundi ya Wamoabu yalikuja kuishambulia nchi ya watu wa Israeli. Wakati mmoja, wakati wa mazishi, watu waliona kundi mojawapo la watu waliobeba maiti wakamtupa yule maiti kaburini mwa Elisha na kukimbia. Mara maiti huyo alipogusa mifupa ya Elisha, alifufuka na kusimama wima. Mfalme Hazaeli wa Aramu aliwanyanyasa sana watu wa Israeli wakati wote wa enzi ya Yehoahazi. Lakini Mwenyezi-Mungu aliwarehemu na kuwaonea huruma. Aliwaangalia kwa wema kwa sababu ya agano lake na Abrahamu, Isaka na Yakobo. Hakuwaangamiza wala hajawaacha kamwe mpaka leo. Hazaeli mfalme wa Aramu alipofariki, Ben-hadadi mwanawe alitawala mahali pake. Mfalme Yehoashi alimshinda Ben-hadadi mara tatu na kuikomboa miji yote iliyotekwa wakati wa utawala wa Yehoahazi, baba yake Yehoashi.

2 Wafalme 13:14-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi Elisha alikuwa ameshikwa na ugonjwa wake uliomwua; naye Yehoashi mfalme wa Israeli akateremka amtazame, akamlilia mbele yake, akasema, Baba yangu! Baba yangu! Gari la Israeli na wapanda farasi wake! Elisha akamwambia, Twaa uta na mishale; naye akatwaa uta na mishale. Akamwambia mfalme wa Israeli, Weka mkono wako katika uta; naye akaweka mkono wake juu yake. Elisha akaweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme. Akasema, Lifungue dirisha linaloelekea mashariki; akalifungua. Basi Elisha akasema, Piga; akapiga. Akasema, Mshale wa BWANA wa kushinda, naam, mshale wa kushinda Shamu, kwa maana utawapiga Washami katika Afeki hata utakapowaangamiza. Akasema, Itwae mishale; akaitwaa. Akamwambia mfalme wa Israeli, Piga chini; akaipiga nchi mara tatu, akaacha. Yule mtu wa Mungu akamkasirikia, akasema, Ingalikupasa kupiga mara tano au mara sita; ndipo ungaliipiga Shamu hata kuiangamiza; bali sasa utaipiga Shamu mara tatu tu. Elisha akafa, nao wakamzika. Basi vikosi vya Wamoabi wakaingia katika nchi mwanzo wa mwaka. Ikawa, walipokuwa wakimzika mtu, angalia, waliona kikosi; wakamtupa yule mtu kaburini mwa Elisha; mara yule maiti alipoigusa mifupa ya Elisha, alifufuka, akasimama kwa miguu. Na Hazaeli mfalme wa Shamu akawaonea Israeli siku zote za Yehoahazi. Lakini BWANA akawahurumia, akawasikitikia, na kuwaangalia, kwa ajili ya agano lake na Abrahamu, na Isaka, na Yakobo, wala hakutaka kuwaangamiza, wala hakuwatupa usoni pake bado. Akafa Hazaeli mfalme wa Shamu, na Ben-hadadi mwanawe akatawala mahali pake. Naye Yehoashi, mwana wa Yehoahazi, akaitwaa tena mkononi mwa Ben-hadadi mwana wa Hazaeli miji ile aliyoitwaa yeye mkononi mwa Yehoahazi baba yake vitani. Mara tatu Yehoashi akamshinda, akairudisha miji ya Israeli.

2 Wafalme 13:14-25 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Wakati huu, Elisha alikuwa anaumwa na ugonjwa ambao baadaye ulimuua. Yehoashi mfalme wa Israeli akashuka kwenda kumwona na kumlilia. Akalia, “Baba yangu! Baba yangu! Magari ya vita ya Israeli na wapanda farasi wake!” Elisha akasema, “Leta upinde na baadhi ya mishale,” naye mfalme akafanya hivyo. Elisha akamwambia mfalme wa Israeli, “Shika upinde mikononi mwako.” Alipokwisha kuichukua, Elisha akaweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme. Elisha akasema, “Fungua dirisha la mashariki,” naye akalifungua. Elisha akasema, “Piga mshale!” Naye akapiga mshale. Elisha akasema, “Mshale wa ushindi wa BWANA, mshale wa ushindi juu ya Aramu! Utawaangamiza Waaramu kabisa huko Afeki.” Kisha akasema, “Chukua mishale,” naye mfalme akaichukua. Elisha akamwambia, “Piga ardhi kwa hiyo mishale.” Akaipiga mara tatu, halafu akaacha. Mtu wa Mungu akamkasirikia na akasema, “Ungepiga chini mara tano au sita, ndipo ungeishinda Aramu na kuiangamiza kabisa. Lakini sasa utaishinda mara tatu tu.” Elisha akafa, nao wakamzika. Vikosi vya Wamoabu vilikuwa vinashambulia nchi kwa vita kila mwaka wakati wa vuli. Ikawa Waisraeli fulani walipokuwa wanamzika mtu, ghafula wakaona kikosi cha washambuliaji, basi wakaitupa ile maiti ya yule mtu ndani ya kaburi la Elisha. Wakati ile maiti ilipogusa mifupa ya Elisha, yule mtu akafufuka na kusimama kwa miguu yake. Hazaeli mfalme wa Aramu aliwatesa Israeli wakati wote wa utawala wa Yehoahazi. Lakini BWANA akawarehemu na akawahurumia, akaonyesha kujishughulisha nao kwa sababu ya Agano lake na Abrahamu, Isaki na Yakobo. Hadi leo, hajawaangamiza wala kuwafukuza mbele zake. Hazaeli mfalme wa Shamu akafa, naye Ben-Hadadi mwanawe akawa mfalme baada yake. Kisha Yehoashi mwana wa Yehoahazi akateka tena kutoka kwa Ben-Hadadi mwana wa Hazaeli ile miji aliyokuwa ameitwaa kwa vita kutoka kwa baba yake Yehoahazi. Yehoashi alimshinda mara tatu, hivyo akaweza kuiteka tena ile miji ya Waisraeli.