2 Samweli 11
11
Daudi na Bathsheba
1Katika mwanzo wa mwaka mpya, wakati wafalme hutoka kwenda vitani, Daudi akamtuma Yoabu pamoja na watu wa mfalme na jeshi lote la Israeli. Wakawaangamiza Waamoni na kuuzingira mji wa Raba. Lakini Daudi akabaki Yerusalemu.
2Ikawa siku moja wakati wa jioni Daudi aliinuka kitandani mwake na kutembeatembea juu ya paa la jumba lake la kifalme. Akiwa kule kwenye paa, akamwona mwanamke akioga. Mwanamke huyo alikuwa mzuri sana wa sura, 3naye Daudi akatuma mtu mmoja kuuliza habari za huyo mwanamke. Huyo mtu akamwambia Daudi, “Je, huyu si Bathsheba binti Eliamu, naye ni mke wa Uria Mhiti?” 4Ndipo Daudi akatuma wajumbe kumleta. Huyo mwanamke akaja kwa Daudi, Daudi akakutana naye kimwili. (Huyo mwanamke ndipo tu alikuwa amejitakasa kutoka siku zake za hedhi.) Kisha akarudi nyumbani mwake. 5Huyo mwanamke akapata mimba akampelekea Daudi ujumbe, kusema, “Mimi ni mjamzito.”
6Ndipo Daudi akapeleka ujumbe kwa Yoabu, “Unipelekee Uria Mhiti.” Naye Yoabu akamtuma Uria kwa Daudi. 7Uria alipofika, Daudi akamuuliza habari za Yoabu, hali za askari na vita kwamba inaendeleaje. 8Kisha Daudi akamwambia Uria, “Teremka nyumbani mwako ukanawe miguu yako.” Basi Uria akatoka jumba la kifalme, tena zawadi zikamfuata kutoka kwa mfalme. 9Lakini Uria akalala kwenye ingilio la jumba la kifalme pamoja na watumishi wote wa bwana wake, na hakuteremka kwenda nyumbani mwake.
10Daudi alipoambiwa kwamba, “Uria hakuenda nyumbani,” Daudi akamuuliza, “Je, si ndiyo tu umefika kutoka safari ya mbali? Kwa nini hukuenda nyumbani?”
11Uria akamwambia Daudi, “Sanduku la Mungu, na Israeli na Yuda wanakaa kwenye mahema, naye bwana wangu Yoabu na watu wa bwana wangu wamepiga kambi mahali pa wazi. Ningewezaje kwenda nyumbani mwangu ili nile, ninywe na kukutana na mke wangu? Hakika kama uishivyo sitafanya jambo kama hilo!”
12Ndipo Daudi akamwambia, “Kaa hapa siku moja zaidi, nami kesho nitakutuma urudi.” Kwa hiyo Uria akakaa Yerusalemu siku ile na siku iliyofuata. 13Kwa ukaribisho wa Daudi, Uria akala na kunywa pamoja naye, Daudi akamlevya. Lakini jioni Uria alitoka kwenda kulala juu ya mkeka wake miongoni mwa watumishi wa bwana wake, hakuenda nyumbani.
14Kesho yake asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu barua, akamtuma Uria kuipeleka. 15Ndani ya barua aliandika, “Mweke Uria mstari wa mbele ambapo mapigano ni makali sana. Kisha wewe uondoke ili Uria aangushwe chini na kuuawa.”
16Hivyo Yoabu alipokuwa ameuzingira mji kwa jeshi, akamweka Uria mahali alipojua kuwa ulinzi wa adui ulikuwa imara sana. 17Wanaume wa mji walipotoka kwenda kupigana dhidi ya Yoabu, baadhi ya watu katika jeshi la Daudi wakauawa; zaidi ya hayo, Uria Mhiti akafa.
18Yoabu akampelekea Daudi maelezo yote ya vita. 19Akamwagiza mjumbe hivi, “Utakapokuwa umemaliza kumpa mfalme maelezo ya vita, 20hasira ya mfalme yaweza kuwaka, naye aweza kukuuliza, ‘Kwa nini mlisogea karibu hivyo na mji kupigana? Hamkujua kuwa wangeweza kuwapiga mishale kutoka ukutani? 21Ni nani aliyemuua Abimeleki mwana wa Yerub-Besheth? Je, mwanamke hakutupa juu yake jiwe la juu la kusagia kutoka ukutani, kwa hiyo akafa huko Thebesi? Kwa nini mlisogea hivyo karibu ya ukuta?’ Akikuuliza hivi, ndipo umwambie, ‘Pia mtumishi wako Uria Mhiti amekufa.’ ”
22Mjumbe akaondoka. Alipowasili akamwambia Daudi kila kitu alichokuwa ametumwa na Yoabu kusema. 23Mjumbe akamwambia Daudi, “Watu walituzidi nguvu wakatoka nje ya mji dhidi yetu kwenye eneo la wazi, lakini tuliwarudisha nyuma hadi ingilio la mji. 24Ndipo wapiga upinde walitupa mishale kwa watumishi wako kutoka ukutani, na baadhi ya watu wa mfalme wakafa. Zaidi ya hayo, Uria Mhiti, mtumishi wako, amekufa.”
25Daudi akamwambia mjumbe, “Ukamwambie Yoabu hivi, ‘Jambo hili lisikutie wasiwasi, upanga hula huyu sawa na ulavyo mwingine. Zidisha mashambulizi dhidi ya mji na uangamize.’ Mwambie Yoabu hivi ili kumtia moyo.”
26Mke wa Uria aliposikia kwamba mumewe amekufa, akamwombolezea. 27Baada ya muda wa maombolezo kwisha, Daudi akatumana aletwe nyumbani mwake. Naye akawa mkewe, na akamzalia mwana. Lakini jambo alilofanya Daudi lilimchukiza Mwenyezi Mungu.
Iliyochaguliwa sasa
2 Samweli 11: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.