2 Samweli 23
23
Maneno ya mwisho ya Daudi
1Haya ni maneno ya mwisho ya Daudi:
“Neno la Daudi mwana wa Yese,
neno la mtu aliyeinuliwa na Aliye Juu Sana,
mtu aliyepakwa mafuta na Mungu wa Yakobo,
mwimbaji wa nyimbo wa Israeli:
2“Roho wa Mwenyezi Mungu alinena kupitia kwangu,
neno lake lilikuwa katika ulimi wangu.
3Mungu wa Israeli alinena,
mwamba wa Israeli akaniambia:
‘Mtu anatawala watu kwa haki,
wakati anapotawala
akiwa na hofu ya Mungu,
4yeye ni kama mwanga wa asubuhi jua lichomozapo
asubuhi isiyo na mawingu,
kama mwanga baada ya mvua
unaochipuza majani kutoka ardhini.’
5“Je, si hivyo ilivyo nyumba yangu
mbele za Mungu?
Je, hajafanya agano la milele nami,
lililopangwa na kuimarishwa
kila sehemu?
Je, hatanifanya niufurahie wokovu wangu
na kunijalia matakwa yangu yote?
6Lakini watu waovu wote
watatupwa kando kama miiba,
ambayo haikusanywi kwa mkono.
7Yeyote agusaye miiba
hutumia chombo cha chuma
au mpini wa mkuki,
nayo huchomwa pale ilipo.”
Mashujaa wa Daudi
(1 Nyakati 11:10-41)
8Haya ndiyo majina ya mashujaa wa Daudi:
Yosheb-Bashebethi#23:8 au Yashobeamu (1 Nyakati 11:11) Mtahkemoni, alikuwa kiongozi wa wale Watatu; yeye aliinua mkuki wake dhidi ya watu mia nane, aliowaua katika pambano moja.
9Wa pili wake alikuwa Eleazari mwana wa Dodai#23:9 tafsiri nyingine zinamwita Dodo Mwahohi. Akiwa mmoja wa wale mashujaa watatu, alikuwa pamoja na Daudi wakati waliwadhihaki Wafilisti waliokuwa wamekusanyika huko Pas-Damimu kwa ajili ya vita. Kisha Waisraeli wakarudi nyuma, 10lakini yeye alisimama imara, akawaua Wafilisti hadi mkono wake ukachoka na kugandamana na upanga. Mwenyezi Mungu akawapa ushindi mkubwa siku ile. Vikosi vikarudi kwa Eleazari kuteka tu nyara za waliokufa.
11Aliyefuata alikuwa Shama mwana wa Agee Mharari. Wafilisti walipokusanyika pamoja mahali palipokuwa shamba lililojaa dengu, vikosi vya Israeli viliwakimbia. 12Lakini Shama akasimama imara katikati ya lile shamba. Akalipigania na kuwaua Wafilisti, naye Mwenyezi Mungu akawapa ushindi mkubwa.
13Wakati wa mavuno, viongozi watatu kati ya wale mashujaa thelathini wakuu walimwendea Daudi katika pango la Adulamu, wakati kikundi cha Wafilisti kilikuwa kimepiga kambi katika Bonde la Warefai. 14Wakati huo Daudi alikuwa katika ngome, na kambi ya Wafilisti ilikuwa huko Bethlehemu. 15Daudi akatamani maji, akasema, “Laiti mtu angenipatia maji ya kunywa kutoka kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu!” 16Basi mashujaa hao watatu wakapenya katikati ya Wafilisti, wakaenda kuchota maji kutoka kwa kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu, wakamletea Daudi. Lakini Daudi akakataa kuyanywa. Badala yake, aliyamimina mbele za Mwenyezi Mungu. 17Akasema, “Iwe mbali nami, Ee Mwenyezi Mungu, kufanya kitu hiki. Je, hii si damu ya watu ambao walienda kwa kuhatarisha maisha yao?” Naye Daudi hakuyanywa.
Haya yalifanywa na hao mashujaa watatu.
18Abishai ndugu yake Yoabu mwana wa Seruya ndiye alikuwa kiongozi wa hao Watatu. Aliinua mkuki wake dhidi ya watu mia tatu ambao aliwaua, kwa hiyo naye akawa na sifa kama hao Watatu. 19Je, hakupata heshima kubwa kuliko hao Watatu? Alikuwa jemadari wao, ingawa hakuhesabiwa miongoni mwao.
20Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa mpiganaji hodari kutoka Kabseeli ambaye alifanya mambo makubwa ya ujasiri. Aliwaua mashujaa wawili waliokuwa hodari kuliko wote wa Moabu. Pia alishuka shimoni kulipokuwa na theluji na kumuua simba. 21Pia alimuua Mmisri mrefu mkubwa. Ingawa Mmisri alikuwa na mkuki mkononi mwake, Benaya alimwendea akiwa na rungu. Alipokonya mkuki kutoka mkononi mwa Mmisri na kumuua kwa mkuki wake mwenyewe. 22Haya yalikuwa mambo ya ushujaa ya Benaya mwana wa Yehoyada; naye pia alikuwa maarufu kama wale mashujaa watatu. 23Yeye aliheshimiwa zaidi ya wale Thelathini, lakini hakujumuishwa miongoni mwa wale Watatu. Daudi akamweka kuwa kiongozi wa walinzi wake.
24Miongoni mwa wale Thelathini walikuwa:
Asaheli ndugu wa Yoabu;
Elhanani mwana wa Dodo kutoka Bethlehemu;
25Shama Mharodi;
Elika Mharodi;
26Helesi Mpalti;
Ira mwana wa Ikeshi kutoka Tekoa;
27Abiezeri kutoka Anathothi;
Mebunai Mhushathi;
28Salmoni Mwahohi;
Maharai Mnetofathi;
29Heledi mwana wa Baana Mnetofathi;
Itai mwana wa Ribai kutoka Gibea ya Benyamini;
30Benaya Mpirathoni;
Hidai kutoka mabonde ya Gaashi;
31Abi-Alboni Mwaribathi;
Azmawethi Mbarhumi;
32Eliaba Mshaalboni;
wana wa Yasheni;
Yonathani 33mwana wa Shama Mharari;
Ahiamu mwana wa Sharari Mharari;
34Elifeleti mwana wa Ahasbai Mmaakathi;
Eliamu mwana wa Ahithofeli Mgiloni;
35Hezro Mkarmeli;
Paarai Mwarbi;
36Igali mwana wa Nathani kutoka Soba;
Bani Mgadi;
37Seleki Mwamoni;
Naharai Mbeerothi, aliyekuwa mbeba silaha za Yoabu mwana wa Seruya;
38Ira Mwithiri;
Garebu Mwithiri;
39na Uria Mhiti.
Jumla yao wote walikuwa watu thelathini na saba.
Iliyochaguliwa sasa
2 Samweli 23: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.