Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wathesalonike 2

2
Yule mtu wa kuasi
1Ndugu, kuhusu kuja kwake Bwana wetu Isa Al-Masihi na kukusanyika kwetu pamoja mbele zake, tunawasihi, 2msiyumbishwe kwa urahisi wala msitiwe wasiwasi na roho, wala neno la unabii, au barua inayosemekana kuwa imetoka kwetu, kusema kwamba siku ya Mwenyezi Mungu imekwisha kuwepo. 3Mtu yeyote asiwadanganye kwa namna yoyote kwa maana siku ile haitakuja hadi uasi utokee kwanza, na yule mtu wa kuasi adhihirishwe, yule ambaye amehukumiwa kuangamizwa kabisa. 4Yeye atapingana na kujitukuza juu ya kila kitu kiitwacho Mungu au kinachoabudiwa, ili kujiweka juu katika Hekalu la Mungu, akijitangaza mwenyewe kuwa ndiye Mungu.
5Je, hamkumbuki kwamba nilipokuwa pamoja nanyi niliwaambia mambo haya? 6Nanyi sasa mnajua kinachomzuia, ili apate kudhihirishwa wakati wake utakapowadia. 7Maana ile nguvu ya siri ya uasi tayari inatenda kazi, lakini yule anayeizuia ataendelea kufanya hivyo hadi atakapoondolewa. 8Hapo ndipo yule mwasi atafunuliwa, ambaye Bwana Isa atamteketeza kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kabisa kwa utukufu wa kuja kwake. 9Kuja kwa yule mwasi kutalingana na vile Shetani hufanya kazi. Atatumia nguvu za aina mbalimbali katika miujiza, na ishara na ajabu za uongo, 10na katika njia zote ambazo uovu hudanganya wanaoangamia. Wanaangamia kwa sababu walikataa kuipenda kweli ili wapate kuokolewa. 11Kwa sababu hii, Mungu anawatumia nguvu ya udanganyifu, ili waamini uongo, 12na hivyo wahukumiwe wote ambao hawakuiamini ile kweli, bali wamefurahia uovu.
Simameni imara
13Lakini inatupasa kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu, ndugu mpendwao na Bwana Isa, kwa sababu Mungu aliwachagua ninyi tangu mwanzo ili mwokolewe kwa kutakaswa na Roho wa Mungu kwa kuiamini kweli. 14Kwa kusudi hili Mungu aliwaita ninyi kupitia Injili tuliyowahubiria, ili mpate kushiriki katika utukufu wa Bwana wetu Isa Al-Masihi.
15Hivyo basi, ndugu wapendwa, simameni imara na myashike sana yale mafundisho tuliyowapa ikiwa ni kwa maneno ya kinywa au kwa barua.
16Bwana wetu Isa Al-Masihi mwenyewe na Mungu, Baba yetu, aliyetupenda na kwa neema yake akatupatia faraja ya milele na tumaini jema, 17awafariji mioyo yenu na kuwaimarisha katika kila neno na tendo jema.

Iliyochaguliwa sasa

2 Wathesalonike 2: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia