1
Salamu
1Paulo, Silvano#1:1 yaani Sila na Timotheo.
Kwa kundi la waumini la Wathesalonike mlio katika Mungu, Baba#1:1 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. yetu, na Bwana Isa Al-Masihi.
2Neema na amani zinazotoka kwa Mungu Baba Mwenyezi na kwa Bwana Isa Al-Masihi ziwe nanyi.
Shukrani na maombi
3Ndugu, inatupasa kumshukuru Mungu kwa ajili yenu siku zote, na inastahili hivyo kwa sababu imani yenu inazidi kukua sana, nao upendo wa kila mmoja wenu kwa mwenzake unazidi kuongezeka. 4Ndiyo sababu miongoni mwa makundi ya waumini ya Mungu, tunajivunia saburi yenu na imani mliyo nayo katika mateso yote na dhiki mnazostahimili.
5Haya yote ni uthibitisho kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na kwa sababu hiyo ninyi mtahesabiwa kwamba mnastahili kuwa wa ufalme wa Mungu, mnaoteswa kwa ajili yake. 6Mungu ni mwenye haki: yeye atawalipa mateso wale wanaowatesa ninyi, 7na kuwapa ninyi mnaoteseka amani pamoja na sisi, wakati Bwana Isa atadhihirishwa kutoka mbinguni katika mwali wa moto pamoja na malaika wake wenye nguvu. 8Atawaadhibu wale wasiomjua Mungu na ambao hawakuitii Injili ya Bwana wetu Isa. 9Wataadhibiwa kwa uangamivu wa milele na kutengwa na uso wa Mwenyezi Mungu na utukufu wa uweza wake, 10siku hiyo atakapokuja kutukuzwa katika watakatifu wake na kustaajabiwa miongoni mwa wote walioamini. Ninyi pia mtakuwa miongoni mwa hawa kwa sababu mliamini ushuhuda wetu kwenu.
11Kwa sababu hii, tunawaombea ninyi bila kukoma, ili Mungu wetu apate kuwahesabu kuwa mnastahili wito wake na kwamba kwa uwezo wake apate kutimiza kila kusudi lenu jema na kila tendo linaloongozwa na imani yenu. 12Tunaomba hivi ili Jina la Bwana wetu Isa lipate kutukuzwa ndani yenu, nanyi ndani yake, kulingana na neema ya Mungu wetu na Bwana Isa Al-Masihi.