3 Yohana 1
1
Salamu
1Mzee.
Kwa Gayo rafiki yangu nimpendaye katika kweli.
Gayo anatiwa moyo
2Mpendwa, naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya njema kama vile roho yako ifanikiwavyo. 3Ilinifurahisha sana baadhi ya ndugu walipokuja na kutueleza kuhusu uaminifu wako katika kweli na jinsi unavyoendelea kuenenda katika hiyo kweli. 4Sina furaha kubwa kuliko hii, ya kusikia kwamba watoto wangu wanaenenda katika kweli.
5Rafiki mpendwa, wewe ni mwaminifu kwa yale unayowatendea ndugu, ingawa wao ni wageni kwako. 6Wameshuhudia kuhusu upendo wako mbele ya jumuiya ya waumini. Utafanya vyema ukiwasafirisha kama inavyostahili kwa Mungu. 7Ilikuwa ni kwa ajili ya hilo Jina waliondoka, bila kukubali kupokea msaada wowote kutoka kwa watu wasiomwamini Al-Masihi. 8Kwa hiyo imetupasa sisi kuonesha ukarimu kwa watu kama hao ili tuweze kutenda kazi pamoja kwa ajili ya kweli.
Deotrefe anakemewa
9Nililiandikia kundi la waumini, lakini Deotrefe, yeye apendaye kujifanya wa kwanza, hakubali mamlaka yetu. 10Hivyo nikija, nitakumbuka matendo yake atendayo, akitusingizia kwa maneno ya hila. Wala hatosheki na hayo anayotusingizia, bali pia hukataa kuwakaribisha ndugu, na hata huwazuia wale walio tayari kufanya hivyo na kuwafukuza watoke miongoni mwa waumini.
Demetrio anasifiwa
11Rafiki mpendwa, usiige lile lililo baya bali lile lililo jema. Yeyote atendaye mema anatoka kwa Mungu, bali atendaye mabaya hajamwona Mungu.
12Kila mtu ameshuhudia mema kuhusu Demetrio, vivyo hivyo hata na hiyo kweli yenyewe. Sisi pia twashuhudia mema juu yake, nanyi mwajua kwamba ushuhuda wetu ni kweli.
Hitimisho
13Ninayo mambo mengi ya kukuandikia, lakini sipendi kuandika kwa kalamu na wino. 14Badala yake, nataraji kukuona upesi, nasi tutaongea pamoja ana kwa ana.
15Amani iwe kwako.
Rafiki zetu walio hapa wanakusalimu. Wasalimu hao rafiki zetu walio huko, kila mmoja kwa jina lake.
Iliyochaguliwa sasa
3 Yohana 1: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.