Matendo 16
16
Timotheo aungana na Paulo na Sila
1Paulo akafika Derbe na kisha Listra, ambako kulikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, ambaye mama yake alikuwa Myahudi aliyeamini, lakini baba yake alikuwa Myunani. 2Alikuwa amesifiwa sana na wale ndugu waliokuwa wameamini huko Listra na Ikonio 3Paulo alitaka Timotheo aandamane naye, hivyo akamtahiri kwa sababu ya Wayahudi walioishi eneo lile, kwa maana wote walimjua baba yake ni Myunani. 4Walipokuwa wakienda mji kwa mji, wakawa wanawapa maamuzi yaliyotolewa na mitume na wazee huko Yerusalemu ili wayafuate. 5Hivyo makundi ya waumini yakaimarika katika imani, na wakaongezeka kwa idadi kila siku.
6Paulo pamoja na wenzake wakasafiri sehemu za Frigia na Galatia, kwa kuwa Roho wa Mungu hakuwaruhusu kulihubiri neno huko jimbo la Asia. 7Walipofika mpaka wa Misia, wakajaribu kuingia Bithinia lakini Roho wa Isa hakuwaruhusu. 8Kwa hiyo wakapita Misia, wakafika Troa. 9Wakati wa usiku Paulo akaona maono, mtu wa Makedonia amesimama akimsihi, “Vuka uje huku Makedonia utusaidie.” 10Baada ya Paulo kuona maono haya, tulijiandaa kwa haraka kuondoka kwenda Makedonia tukiwa tumesadiki kuwa Mungu alikuwa ametuita kuhubiri Injili huko.
Kuokoka kwa Lidia
11Tukasafiri kwa meli kutoka Troa na kwenda moja kwa moja hadi Samothrake, na kesho yake tukafika Neapoli. 12Kutoka huko tukasafiri hadi Filipi, mji mkuu wa jimbo hilo la Makedonia, uliokuwa koloni ya Warumi. Nasi tukakaa huko siku kadhaa.
13Siku ya Sabato tukaenda nje ya lango la mji kando ya mto, ambapo tulitarajia kupata mahali pa kufanyia maombi. Tukaketi, tukaanza kuongea na baadhi ya wanawake waliokuwa wamekusanyika huko. 14Mmoja wa wale wanawake waliotusikiliza aliitwa Lidia, mfanyabiashara wa nguo za zambarau, raia wa mji wa Thiatira, aliyekuwa mcha Mungu. Mwenyezi Mungu akaufungua moyo wake akaupokea ujumbe wa Paulo. 15Basi alipokwisha kubatizwa yeye na watu wa nyumba yake, alitukaribisha nyumbani mwake, akisema, “Kama mmeona kweli mimi nimemwamini Bwana Isa, karibuni mkae nyumbani mwangu.” Naye akatushawishi.
Paulo na Sila watiwa gerezani
16Siku moja, tulipokuwa tukienda mahali pa kusali, tulikutana na mjakazi aliyekuwa na pepo wa uaguzi. Naye alikuwa amewapa mabwana zake mapato makubwa ya fedha kwa ubashiri. 17Huyu mjakazi alikuwa akimfuata Paulo na sisi akipaza sauti na kusema, “Watu hawa ni watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, wao wanawatangazieni njia ya wokovu.” 18Akaendelea kufanya hivi kwa siku nyingi, lakini Paulo akiwa ameudhika sana, akageuka na kumwambia yule pepo mchafu, “Ninakuamuru katika jina la Isa Al-Masihi, umtoke!” Yule pepo mchafu akamtoka mara hiyo.
19Basi mabwana wa yule mjakazi walipoona kuwa tumaini lao la kuendelea kujipatia fedha limetoweka, wakawakamata Paulo na Sila wakawaburuta hadi sokoni mbele ya viongozi wa mji. 20Baada ya kuwafikisha mbele ya mahakimu wakawashtaki wakisema, “Hawa watu wanaleta ghasia katika mji wetu, nao ni Wayahudi. 21Wanafundisha desturi ambazo sisi raia wa Rumi hatuwezi kuzikubali au kuzitimiza.”
22Umati wa watu wakajiunga kuwashambulia Paulo na Sila, na wale mahakimu wakaamuru wavuliwe nguo zao na wapigwe mijeledi. 23Baada ya kuwapiga sana, wakawatupa gerezani na kumwagiza mkuu wa gereza awalinde kikamilifu. 24Kufuata maelekezo haya, yule mkuu wa gereza akawaweka katika chumba cha ndani sana mle gerezani, na akawafunga miguu yao kwa minyororo.
25Ilipokaribia usiku wa manane, Paulo na Sila walikuwa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, nao wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. 26Ghafula pakatokea tetemeko kubwa la ardhi, hata msingi wa gereza ukatikisika. Mara milango ya gereza ikafunguka na ile minyororo iliyowafunga kila mmoja ikafunguka. 27Yule mkuu wa gereza alipoamka na kuona milango ya gereza iko wazi, akachomoa upanga wake akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wote wametoroka. 28Lakini Paulo akapaza sauti kwa nguvu, akisema, “Usijidhuru kwa maana sisi sote tuko hapa!”
29Yule askari wa gereza akaagiza taa ziletwe, akaingia ndani ya kile chumba cha gereza, akapiga magoti akitetemeka mbele ya Paulo na Sila. 30Kisha akawaleta nje akisema, “Bwana zangu, nifanye nini nipate kuokoka?”
31Wakamjibu, “Mwamini Bwana Isa Al-Masihi, nawe utaokoka, pamoja na watu wa nyumbani mwako.” 32Wakamwambia neno la Bwana Isa, yeye pamoja na wote waliokuwa nyumbani mwake. 33Wakati ule ule, yule mkuu wa gereza akawachukua, akawaosha majeraha yao, kisha akabatizwa yeye pamoja na wote waliokuwa nyumbani mwake bila kuchelewa. 34Akawapandisha nyumbani mwake akawaandalia chakula, yeye pamoja na nyumba yake yote wakafurahi sana kwa kuwa sasa walikuwa wamemwamini Mungu.
35Kulipopambazuka wale mahakimu wakawatuma maafisa wao kwa mkuu wa gereza wakiwa na agizo linalosema, “Wafungue wale watu, waachie waende zao.” 36Mkuu wa gereza akamwambia Paulo “Mahakimu wameagiza niwaachie huru, kwa hiyo tokeni na mwende zenu kwa amani.”
37Lakini Paulo akawaambia wale maafisa, “Wametupiga hadharani bila kutufanyia mashtaka na kutuhoji, nao wakatutupa gerezani, hata ingawa sisi ni raia wa Rumi. Nao sasa wanataka kututoa gerezani kwa siri? Hapana! Wao na waje wenyewe watutoe humu gerezani.”
38Wale maafisa wakarudi na kuwaambia wale mahakimu maneno haya, wakaogopa sana walipofahamu kuwa Paulo na Sila ni raia wa Rumi. 39Kwa hiyo wakaja wakawaomba msamaha, wakawatoa gerezani, wakawaomba waondoke katika ule mji. 40Baada ya Paulo na Sila kutoka gerezani walienda nyumbani mwa Lidia, ambapo walikutana na waumini, wakawatia moyo, ndipo wakaondoka.
Iliyochaguliwa sasa
Matendo 16: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.