Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 2:14-41

Matendo 2:14-41 NEN

Ndipo Petro akasimama pamoja na wale mitume kumi na mmoja, akainua sauti yake na kuhutubia ule umati wa watu, akasema: “Wayahudi wenzangu na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, jueni jambo hili mkanisikilize. Hakika watu hawa hawakulewa kama mnavyodhania, kwa kuwa sasa ni saa tatu asubuhi! La, hili ni jambo lililotabiriwa na nabii Yoeli, akisema: “ ‘Katika siku za mwisho, asema Mungu, nitamimina Roho wangu juu ya wote wenye mwili. Wana wenu na binti zenu watatabiri, vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto. Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile nitamimina Roho wangu, nao watatabiri. Nami nitaonyesha maajabu juu mbinguni, na ishara chini duniani: damu, moto, na mawimbi ya moshi. Jua litakuwa giza na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kuja siku ile kuu ya Bwana iliyo tukufu. Na kila mtu atakayeliitia jina la Bwana, ataokolewa.’ “Enyi Waisraeli, sikilizeni maneno haya nisemayo: Yesu wa Nazareti alikuwa mtu aliyethibitishwa kwenu na Mungu kwa miujiza, maajabu na ishara, ambayo Mungu alitenda miongoni mwenu kupitia kwake, kama ninyi wenyewe mjuavyo. Huyu mtu akiisha kutolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa kwa kujua kwake Mungu tangu zamani, ninyi, kwa mikono ya watu wabaya, mlimuua kwa kumgongomea msalabani. Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu akamwondolea uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana yeye kushikiliwa na nguvu za mauti. Kwa maana Daudi asema kumhusu yeye: “ ‘Nalimwona Bwana mbele yangu daima. Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume, sitatikisika. Kwa hiyo moyo wangu unafurahia, na ulimi wangu unashangilia; mwili wangu nao utapumzika kwa tumaini. Kwa maana hutaniacha kaburini, wala hutamwacha Aliye Mtakatifu wako kuona uharibifu. Umenionyesha njia za uzima, utanijaza na furaha mbele zako.’ “Ndugu zangu Waisraeli, nataka niwaambie kwa uhakika kwamba baba yetu Daudi alikufa na kuzikwa, nalo kaburi lake lipo hapa mpaka leo. Lakini alikuwa nabii na alijua ya kuwa Mungu alikuwa amemwahidi kwa kiapo kwamba angemweka mmoja wa wazao wake penye kiti chake cha enzi. Daudi, akiona mambo yaliyoko mbele, akanena juu ya kufufuka kwa Kristo, kwamba hakuachwa kaburini, wala mwili wake haukuona uharibifu. Mungu alimfufua huyu Yesu na sisi sote ni mashahidi wa jambo hilo. Basi ikiwa yeye ametukuzwa kwa mkono wa kuume wa Mungu, amepokea kutoka kwa Baba ahadi ya Roho Mtakatifu, naye amemimina kile mnachoona sasa na kusikia. Kwa kuwa Daudi hakupaa kwenda mbinguni, lakini anasema, “ ‘BWANA alimwambia Bwana wangu: “Keti mkono wangu wa kuume, hadi nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako.” ’ “Kwa hiyo Israeli wote na wajue jambo hili kwa uhakika kwamba: Mungu amemfanya huyu Yesu, ambaye ninyi mlimsulubisha, kuwa Bwana na Kristo.” Watu waliposikia maneno haya yakawachoma mioyo yao, wakawauliza Petro na wale mitume wengine, “Ndugu zetu tufanye nini?” Petro akawajibu, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu kwa jina la Yesu Kristo, ili mpate kusamehewa dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu na watoto wenu, na kwa wote walio mbali, na kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita amjie.” Petro akawaonya kwa maneno mengine mengi na kuwasihi akisema, “Jiepusheni na kizazi hiki kilichopotoka.” Wale wote waliopokea ujumbe wa Petro kwa furaha wakabatizwa na siku ile waliongezeka watu wapatao 3,000.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Matendo 2:14-41