Matendo 23
23
1Paulo akawakazia macho wale wajumbe wa Baraza la Wayahudi#23:1 Baraza la Wayahudi ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi; liliundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu., akasema, “Ndugu zangu, nimetimiza wajibu wangu kwa Mungu kwa dhamiri safi kabisa hadi leo.” 2Kwa ajili ya jambo hili kuhani mkuu Anania akaamuru wale waliokuwa karibu na Paulo wampige kofi kinywani. 3Ndipo Paulo akamwambia, “Mungu atakupiga wewe, ewe ukuta uliopakwa chokaa! Wewe umeketi hapo ili kunihukumu kwa mujibu wa sheria, lakini wewe mwenyewe unakiuka sheria kwa kuamuru kwamba nipigwe kinyume cha sheria!”
4Wale watu waliokuwa wamesimama karibu na Paulo wakamwambia, “Je, wewe wathubutu kumtukana kuhani mkuu wa Mungu?”
5Paulo akajibu, “Ndugu zangu, sikujua kwamba yeye alikuwa kuhani mkuu. Kwa maana imeandikwa, ‘Usimnenee mabaya kiongozi wa watu wako.’#23:5 Kutoka 22:28”
6Paulo alipotambua ya kuwa baadhi yao walikuwa Masadukayo na wengine ni Mafarisayo#23:6 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli., akapaza sauti kwenye Baraza la Wayahudi, akasema, “Ndugu zangu, mimi ni Farisayo, mwana Farisayo. Hapa nimeshtakiwa kuhusu tumaini langu katika ufufuo wa wafu.” 7Aliposema haya, kukazuka mabishano kati ya Mafarisayo na Masadukayo, na baraza lote likagawanyika. 8(Kwa maana Masadukayo wanasema kwamba hakuna ufufuo, wala hakuna malaika au roho, lakini Mafarisayo wanaamini haya yote.)
9Kukawa na ghasia kubwa, nao baadhi ya walimu wa Torati ambao ni Mafarisayo, wakasimama wakapinga kwa nguvu wakisema, “Hatuoni kosa lolote la mtu huyu! Huenda ikawa roho au malaika amezungumza naye” 10Ugomvi ukawa mkubwa kiasi kwamba yule jemadari akahofu kuwa wangemrarua Paulo vipande vipande, akaamuru vikosi vya askari vishuke na kumwondoa Paulo katikati yao kwa nguvu na kumleta ndani ya ngome ya jeshi.
11Usiku uliofuata, Bwana Isa akasimama karibu naye akamwambia, “Jipe moyo! Kama vile ulivyonishuhudia hapa Yerusalemu, hivyo imekupasa kunishuhudia huko Rumi pia.”
Njama za kumuua Paulo
12Kulipopambazuka Wayahudi wakapanga njama pamoja na kujifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala kunywa hadi wawe wamemuua Paulo. 13Waliofanya mpango huo walikuwa zaidi ya watu arobaini. 14Wakaenda kwa viongozi wa makuhani na wazee na kusema, “Tumeapa kwamba hatutakula chochote hadi tuwe tumemuua Paulo. 15Sasa basi, wewe pamoja na Baraza la Wayahudi mwombeni jemadari amlete Paulo mbele yenu kwa kisingizio cha kutaka taarifa sahihi zaidi kuhusu kesi yake. Nasi tuko tayari kumuua kabla hajafika hapa.”
16Lakini mtoto wa dada yake Paulo aliposikia kuhusu njama hiyo, alienda kule kwenye ngome ya askari na kumweleza Paulo.
17Ndipo Paulo akamwita mmoja wa viongozi wa askari, akamwambia, “Mpeleke huyu kijana kwa jemadari, ana jambo la kumweleza.” 18Hivyo yule kiongozi wa askari akampeleka yule kijana kwa jemadari, akamwambia, “Paulo yule mfungwa aliniita na kuniomba nimlete huyu kijana kwako, kwa sababu ana neno la kukueleza.”
19Yule jemadari akamshika yule kijana mkono, akampeleka kando na kumuuliza, “Unataka kuniambia nini?”
20Yule kijana akasema, “Wayahudi wamekubaliana wakuombe umpeleke Paulo kwenye Baraza la Wayahudi kesho kwa kisingizio kwamba wanataka kufanya uchunguzi wa kina kumhusu. 21Lakini usishawishiwe nao kwa maana zaidi ya watu arobaini wanamvizia. Wameapa kwamba hawatakula wala kunywa hadi wamuue Paulo. Sasa wako tayari, wanangoja idhini yako kwa ombi lao.”
22Yule jemadari akamruhusu yule kijana aende na akamwonya, akisema, “Usimwambie mtu yeyote kwamba umenieleza habari hizi.”
Paulo ahamishiwa Kaisaria
23Kisha yule jemadari akawaita viongozi wake wawili wa askari akawaambia, “Jiandaeni kuondoka saa tatu usiku huu kuelekea Kaisaria pamoja na askari mia mbili, wapanda farasi sabini, na watu mia mbili wenye mikuki. 24Pia tayarisheni na farasi watakaotumiwa na Paulo, mkampeleke salama kwa mtawala Feliksi.”
25Kisha akaandika barua kwa Feliksi kama ifuatavyo:
26Klaudio Lisia.
Kwa Mtawala, Mtukufu Feliksi.
Salamu.
27Mtu huyu alikamatwa na Wayahudi wakakaribia kumuua, lakini nikaja na vikosi vyangu vya askari nikamwokoa, kwa kuwa nilipata habari kwamba yeye ni raia wa Rumi. 28Nilitaka kujua kwa nini walikuwa wanamshutumu, hivyo nikamleta mbele ya Baraza la Wayahudi. 29Ndipo nikaona kuwa alikuwa anashutumiwa kwa mambo yanayohusu sheria yao, lakini hakuwa ameshtakiwa kwa jambo lolote linalostahili kifo au kifungo. 30Nilipoarifiwa kuwa kulikuwa na njama dhidi ya mtu huyu, nilimtuma kwako mara moja. Niliwaagiza washtaki wake pia waeleze mashtaka yao dhidi yake mbele yako.
31Hivyo askari, kwa kufuata maelekezo waliyopewa, wakamchukua Paulo wakati wa usiku na kumleta hadi Antipatri. 32Kesho yake wakawaacha wale wapanda farasi waendelee na safari wakiwa na Paulo, wao wakarudi kwenye ngome ya askari. 33Askari walipofika Kaisaria, walimpa mtawala ile barua, na kumkabidhi Paulo kwake. 34Mtawala alipokwisha kuisoma ile barua alimuuliza Paulo alikuwa mtu wa jimbo gani. Alipojua kuwa anatoka Kilikia, 35alisema, “Nitasikiliza kesi yako washtaki wako watakapofika hapa.” Kisha akaamuru Paulo awekwe chini ya ulinzi kwenye jumba la kifalme la Herode.
Iliyochaguliwa sasa
Matendo 23: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.