Matendo 4:12-22
Matendo 4:12-22 NEN
Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hakuna jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.” Wale viongozi na wazee walipoona ujasiri wa Petro na Yohana na kujua ya kuwa walikuwa watu wa kawaida, wasio na elimu, walishangaa sana, wakatambua kwamba hawa watu walikuwa na Yesu. Lakini kwa kuwa walikuwa wanamwona yule kiwete aliyeponywa amesimama pale pamoja nao, hawakuweza kusema lolote kuwapinga. Wakawaamuru watoke nje ya Baraza la Wayahudi wakati wakisemezana jambo hilo wao kwa wao. Wakaulizana, “Tuwafanyie nini watu hawa? Hatuwezi kukanusha muujiza huu mkubwa walioufanya ambao ni dhahiri kwa kila mtu Yerusalemu. Lakini ili kuzuia jambo hili lisiendelee kuenea zaidi kwa watu, ni lazima tuwaonye watu hawa ili wasiseme tena na mtu yeyote kwa jina la Yesu.” Kisha wakawaita tena ndani na kuwaamuru wasiseme wala kufundisha kamwe kwa hili jina la Yesu. Lakini Petro na Yohana wakajibu, “Amueni ninyi wenyewe iwapo ni haki mbele za Mungu kuwatii ninyi kuliko kumtii Mungu. Lakini sisi hatuwezi kuacha kusema yale tuliyoyaona na kuyasikia.” Baada ya vitisho vingi, wakawaacha waende zao. Hawakuona njia yoyote ya kuwaadhibu, kwa sababu ya watu, kwa kuwa watu wote walikuwa wakimsifu Mungu kwa kile kilichokuwa kimetukia. Kwa kuwa umri wa yule mtu aliyekuwa ameponywa kwa muujiza ulikuwa zaidi ya miaka arobaini.