Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Amosi 9:1-10

Amosi 9:1-10 NEN

Nilimwona Bwana akiwa amesimama kando ya madhabahu, naye akasema: “Piga vichwa vya nguzo ili vizingiti vitikisike. Viangushe juu ya vichwa vya watu wote; na wale watakaosalia nitawaua kwa upanga. Hakuna awaye yote atakayekimbia, hakuna atakayetoroka. Wajapojichimbia chini mpaka kwenye vina vya kuzimu, kutoka huko mkono wangu utawatoa. Wajapopanda juu hadi kwenye mbingu, kutoka huko nitawashusha. Wajapojificha juu ya kilele cha Karmeli, huko nitawawinda na kuwakamata. Wajapojificha kutoka kwenye uso wangu katika vilindi vya bahari, huko nako nitaamuru joka kuwauma. Wajapopelekwa uhamishoni na adui zao, huko nako nitaamuru upanga uwaue. Nitawakazia macho yangu kwa mabaya wala si kwa mazuri.” Bwana, BWANA Mwenye Nguvu Zote, yeye agusaye dunia nayo ikayeyuka, na wote wakaao ndani mwake wakaomboleza: nayo nchi yote huinuka kama Naili, kisha hushuka kama mto wa Misri; yeye ambaye hujenga jumba lake la kifalme katika mbingu na kuisimika misingi yake juu ya dunia, yeye aitaye maji ya bahari na kuyamwaga juu ya uso wa nchi: BWANA ndilo jina lake. “Je, Waisraeli, ninyi si sawa kwangu kama Wakushi?” asema BWANA. “Je, sikuleta Israeli kutoka Misri, Wafilisti kutoka Kaftori, na Washamu kutoka Kiri? “Hakika macho ya BWANA Mwenyezi yako juu ya ufalme wenye dhambi. Nami nitauangamiza kutoka kwenye uso wa dunia: hata hivyo sitaiangamiza kabisa nyumba ya Yakobo,” asema BWANA. “Kwa kuwa nitatoa amri, na nitaipepeta nyumba ya Israeli miongoni mwa mataifa yote, kama vile nafaka ipepetwavyo katika ungo, na hakuna hata punje moja itakayoanguka chini. Watenda dhambi wote miongoni mwa watu wangu watauawa kwa upanga, wale wote wasemao, ‘Maafa hayatatupata wala kutukuta.’