Amosi Utangulizi
Utangulizi
Amosi maana yake ni “Mchukua mzigo.” Yeye alikuwa mchunga wanyama na pia mtunza mikuyu kutoka Tekoa, kijiji kilicho karibu na Bethlehemu na kilomita 16 kutoka Yerusalemu. Mungu alimwita kuwa nabii katika Ufalme wa Kaskazini (Israeli). Wakati huo ufalme ulikuwa na utajiri mwingi. Ujumbe wa Amosi unaonyesha kwamba wakati huo ulikuwa wa mafanikio mengi kiuchumi na kisiasa katika Israeli kuliko nyakati zingine zote, isipokuwa zile za enzi ya Solomoni.
Amosi aliwalaumu watu vikali kwa kuliacha neno la Mungu, kukosa haki katika jamii na kwa maskini, kuwa wakatili, kutawaliwa na ubinafsi, na kufuata anasa na kuabudu sanamu. Uwajibikaji wa Israeli ulikuwa mkubwa kuliko wa mataifa mengine yaliyowazunguka kwa sababu walikuwa wamepewa upendeleo mkubwa zaidi. Katika maono matano mfululizo, Amosi aliona kuwa siku ya maangamizi ilikuwa karibu. Aliwaonya watu kwamba iliwapasa kujiandaa kukutana na Mungu. Kwa wale waliokuwa wanampenda Mungu, Amosi alikuwa na neno la kuwapa matumaini. Siku ilikuwa inakuja ambapo ufalme wa Daudi ungekomeshwa ghafula lakini wacha Mungu wangeishi salama.
Mwandishi
Amosi.
Kusudi
Kutangaza hukumu ya Mungu dhidi ya Israeli kwa kuishi katika hali ya kutosheka na kuridhika, kuabudu sanamu na kuwadhulumu maskini.
Mahali
Samaria, Betheli, Gilgali.
Tarehe
760–750 K.K.
Wahusika Wakuu
Amosi, Amazia, na Yeroboamu wa Pili.
Wazo Kuu
Amosi aliwashutumu watu vikali kwa kuwagandamiza maskini. Kutokana na haya, alitangaza hukumu ya Mungu dhidi yao kwa sababu walikuwa wamemwacha Mungu.
Mambo Muhimu
Amosi ametumia mifano ya maneno ya kusisimua kutokana na uzoefu wake wa ukulima na uchungaji wa wanyama: Simba angurumaye, kipande cha kondoo kilichopokonywa kinywani mwa simba, ngʼombe walioshiba, kapu la matunda, n.k.
Mgawanyo
Hukumu kwa majirani wa Israeli (1:1–2:5)
Hukumu kwa Israeli (2:6-16)
Uovu wa Israeli (3:1–6:14)
Maono matano (7:1–9:10)
Matengenezo ya Israeli (9:11-15).
Iliyochaguliwa sasa
Amosi Utangulizi: NEN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.
Used with Permission. All Rights Reserved Worldwide.