Amosi Utangulizi
Utangulizi
Amosi maana yake ni “Mchukua mzigo”. Yeye alikuwa mchunga wanyama na pia mtunza mikuyu kutoka Tekoa, kijiji kilichokuwa karibu na Bethlehemu na kilomita 16 kutoka Yerusalemu. Mwenyezi Mungu alimwita kuwa nabii katika Ufalme wa Kaskazini (Israeli) na alifanya kazi wakati mmoja na nabii Hosea. Wakati huo ufalme ulikuwa na utajiri mwingi. Ujumbe wa Amosi unaonesha kwamba wakati huo ulikuwa wa mafanikio mengi kiuchumi na kisiasa katika Israeli kuliko nyakati zingine zote, isipokuwa zile za enzi ya Sulemani.
Hata hivyo, Amosi aliona uovu na ubatili mwingi katika miji ya Yuda iliyokuwa katika ufalme wa kaskazini. Watu wengi waliishi katika dimbwi la umaskini wakati matajiri waliishi maisha ya anasa na ya kifahari. Rushwa, ukosefu wa haki, na manyanyaso ya matajiri na wenye nguvu dhidi ya watu wanyonge vilikithiri. Kwa jumla, miji ilitawaliwa na uovu na haikuwa na uchaji kwa Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo, katika unabii wake, Amosi alikemea vikali hali hii na aliwaonya watu wamrudie Mwenyezi Mungu.
Mwandishi
Amosi.
Kusudi
Kukemea matendo maovu, kukosekana kwa uadilifu na kutangaza hukumu ya Mwenyezi Mungu dhidi ya watendao maovu hayo; kuwahimiza watu kutenda haki na kufanya ibada za kweli mbele za Mwenyezi Mungu.
Mahali
Samaria, Betheli, Gilgali.
Tarehe
Mnamo 760–755 K.K.
Wahusika Wakuu
Amosi, Amazia, na Yeroboamu wa Pili.
Wazo Kuu
Haki, uadilifu na hukumu ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya dhambi.
Mambo Muhimu
Amosi ametumia mifano ya maneno ya kusisimua kutokana na uzoefu wake wa ukulima na uchungaji wa wanyama: simba angurumaye, kipande cha kondoo kilichopokonywa kinywani mwa simba, ng’ombe walioshiba, kapu la matunda, na mifano mingine.
Yaliyomo
Hukumu kwa Israeli na mataifa jirani (1:1–2:16)
Uovu wa Israeli (3:1–6:14)
Maono matano (7:1–9:10)
Kurejeshwa kwa Israeli (9:11-15).
Iliyochaguliwa sasa
Amosi Utangulizi: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.