Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 1

1
Mafunzo ya Danieli huko Babeli
1Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, Nebukadneza mfalme wa Babeli alikuja akazingira Yerusalemu. 2Bwana akamtia Yehoyakimu mfalme wa Yuda mkononi mwa Nebukadneza, pamoja na baadhi ya vyombo kutoka Hekalu la Mungu. Nebukadneza akavichukua hadi kwenye hekalu la mungu wake huko Shinari#1:2 yaani Babeli, naye akaviweka nyumbani ya hazina ya mungu wake.
3Kisha mfalme akamwagiza Ashpenazi, mkuu wa maafisa wa mfalme, kumletea baadhi ya Waisraeli kutoka jamaa ya mfalme na kutoka jamaa kuu: 4vijana wa kiume wasio na dosari mwilini, wenye sura nzuri, wanaoonesha kipaji katika kila aina ya elimu, wenye ufahamu mzuri, wepesi kuelewa, na waliofuzu kuhudumu katika jumba la kifalme. Alikuwa awafundishe lugha na maandiko ya Wakaldayo. 5Mfalme akawaagizia kiasi cha chakula na divai ya kila siku kutoka meza ya mfalme. Walikuwa wafundishwe kwa miaka mitatu, na hatimaye waingie kwenye utumishi wa mfalme.
6Baadhi ya hawa vijana walitoka Yuda: Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria. 7Mkuu wa maafisa akawapa majina mapya: Danieli akamwita jina Belteshaza, Hanania akamwita jina Shadraki, Mishaeli akamwita jina Meshaki, na Azaria akamwita jina Abednego.
8Lakini Danieli alikusudia kuwa hatajinajisi kwa chakula cha mfalme na divai, naye akamwomba mkuu wa maafisa ruhusa ili asijinajisi kwa njia hii. 9Basi Mungu alikuwa amemfanya huyo mkuu wa maafisa kuonesha upendeleo na huruma kwa Danieli. 10Lakini huyo mkuu wa maafisa akamwambia Danieli, “Ninamwogopa bwana wangu mfalme, aliyeagizia chakula na kinywaji chenu. Kwa nini aone nyuso zenu zikiwa mbaya kuliko za vijana wengine wa rika lenu? Mfalme atakata kichwa changu kwa sababu yenu.”
11Ndipo Danieli akamwambia mlinzi aliyeteuliwa na huyo mkuu wa maafisa kuwasimamia Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria, 12“Tafadhali wajaribu watumishi wako kwa siku kumi. Usitupe chochote ila nafaka na mboga za majani#1:12 yaani zeroimu kwa Kiebrania; ina maana ya aina za ngano na shayiri, na jamii ya kunde kama maharagwe, dengu, choroko, na zingine tule, na maji ya kunywa. 13Baadaye ulinganishe sura zetu na vijana wanaokula chakula cha mfalme, ukawatendee watumishi wako kulingana na unachoona.” 14Basi akakubali jambo hili, akawajaribu kwa siku kumi.
15Mwisho wa zile siku kumi, walionekana kuwa na afya na kunawiri kuliko yeyote kati ya vijana waliokula chakula cha mfalme. 16Hivyo mlinzi wao akaondoa chakula chao na divai yao waliopangiwa kula na kunywa, akawapa nafaka na mboga za majani badala yake.
17Mungu akawapa hawa vijana wanne maarifa na ufahamu wa kila aina ya maandiko na elimu. Naye Danieli aliweza kufahamu maono na aina zote za ndoto.
18Mwisho wa muda uliowekwa na mfalme ili kuwaingiza kwake, mkuu wa maafisa akawaleta mbele ya Mfalme Nebukadneza. 19Mfalme akazungumza nao, akaona hakuna aliyelingana na Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria. Hivyo wakaingia katika utumishi wa mfalme. 20Katika kila jambo la hekima na ufahamu kuhusu kile mfalme alichowauliza, aliwapata kuwa bora mara kumi zaidi ya waganga na wasihiri wote katika ufalme wake wote.
21Naye Danieli akabaki huko hadi mwaka wa kwanza wa utawala wa Mfalme Koreshi.

Iliyochaguliwa sasa

Danieli 1: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia