Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 2:1-16

Danieli 2:1-16 NEN

Katika mwaka wa pili wa utawala wake, Nebukadneza aliota ndoto. Mawazo yake yakasumbuka na hakuweza kulala. Hivyo mfalme akawaita waganga, wasihiri, wachawi na wanajimu ili wamwambie ndoto yake aliyokuwa ameota. Walipoingia ndani na kusimama mbele ya mfalme, akawaambia, “Niliota ndoto inayonisumbua, nami nataka nijue maana yake.” Ndipo wanajimu wakamjibu mfalme kwa lugha ya Kiaramu, “Ee mfalme, uishi milele! Waambie watumishi wako hiyo ndoto, nasi tutaifasiri.” Mfalme akawajibu wanajimu, “Nimeamua hivi kwa uthabiti: Ikiwa hamtaniambia ndoto yangu ilikuwa ipi na kuifasiri, mtakatwa vipande vipande na nyumba zenu zitafanywa kuwa vifusi. Lakini mkiniambia ndoto yangu na kuielezea, mtapokea kwangu zawadi, tuzo na heshima kubwa. Basi niambieni ndoto yangu na mnifasirie.” Wakajibu kwa mara nyingine, “Mfalme na awaambie watumishi wake ndoto yake, nasi tutaifasiri.” Ndipo mfalme akajibu, “Nina hakika kuwa mnajaribu kupata muda zaidi, kwa sababu mnatambua kuwa nimeamua hivi kwa uthabiti: Ikiwa hamtaniambia ndoto yangu, ipo adhabu moja tu kwenu. Mmefanya shauri kuniambia habari za kunipotosha na mambo maovu, mkitumaini kwamba hali itabadilika. Hivyo basi, niambieni hiyo ndoto, nami nitajua kuwa mwaweza kunifasiria.” Wanajimu wakamjibu mfalme, “Hakuna mtu duniani ambaye anaweza kufanya analotaka mfalme! Vilevile hakuna mfalme hata awe mkuu na mwenye uweza namna gani, aliyeuliza kitu kama hicho kwa mganga au kwa msihiri, wala kwa mnajimu yeyote. Anachouliza mfalme ni kigumu mno. Hakuna yeyote awezaye kumfunulia mfalme isipokuwa miungu, nao hawaishi miongoni mwa wanadamu.” Jambo hili lilimkasirisha na kumghadhibisha mfalme mno hata kuagiza kuuawa kwa wenye hekima wote wa Babeli. Hivyo amri ikatolewa ya kuwaua wenye hekima, nao watu wakatumwa kuwatafuta Danieli na rafiki zake ili wawaue. Wakati Arioko, mkuu wa askari wa walinzi wa mfalme, alikuwa amekwenda kuwaua watu wenye hekima wa Babeli, Danieli akazungumza naye kwa hekima na busara. Akamuuliza huyo afisa wa mfalme, “Kwa nini mfalme ametoa amri kali hivyo?” Ndipo Arioko akamweleza Danieli jambo hilo. Aliposikia jambo hili, Danieli akamwendea mfalme, akamwomba ampe muda ili aweze kumfasiria ile ndoto.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Danieli 2:1-16