Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 3:19-30

Danieli 3:19-30 NEN

Ndipo Nebukadneza akawa na ghadhabu kali sana kwa Shadraki, Meshaki na Abednego, nayo nia yake ikabadilika kwao. Akaagiza tanuru ichochewe moto mara saba kuliko kawaida yake na kuwaamuru baadhi ya askari wake wenye nguvu zaidi katika jeshi lake kuwafunga Shadraki, Meshaki na Abednego na kuwatupa ndani ya tanuru iwakayo moto. Hivyo watu hawa, walifungwa na kutupwa ndani ya tanuru iwakayo moto wakiwa wamevaa majoho yao, suruali, vilemba na nguo zao nyingine. Amri ya mfalme ilikuwa ya haraka sana na tanuru ilikuwa na moto mkali kiasi kwamba miali ya moto iliwaua wale askari waliowapeleka Shadraki, Meshaki na Abednego. Watu hawa watatu walianguka ndani ya tanuru iwakayo moto wakiwa wamefungwa kwa uthabiti sana. Ndipo Mfalme Nebukadneza akashangaa, akainuka kwa haraka na kuwauliza washauri wake, “Je, hawakuwa watu watatu ambao tuliwafunga na kuwatupa ndani ya moto?” Washauri wakajibu, “Hakika, ee mfalme.” Mfalme akasema, “Tazama! Naona watu wanne wakitembeatembea ndani ya moto, hawajafungwa wala kudhurika, naye mtu yule wa nne anaonekana kama mwana wa miungu.” Ndipo Nebukadneza akaukaribia mdomo wa ile tanuru iwakayo moto na kupaza sauti, “Shadraki, Meshaki na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, tokeni! Njooni hapa!” Ndipo Shadraki, Meshaki na Abednego wakatoka ndani ya moto. Nao maliwali, wasimamizi, watawala na washauri wa mfalme wakakusanyika kuwazunguka. Waliona kwamba moto haukudhuru miili yao, wala unywele wa vichwa vyao haukuungua, majoho yao hayakuungua, wala hapakuwepo na harufu ya moto kwenye miili yao. Ndipo Nebukadneza akasema, “Ahimidiwe Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego, ambaye amemtuma malaika wake na kuwaokoa watumishi wake. Walimtumaini na kukaidi amri ya mfalme, nao wakawa tayari kufa kuliko kutumikia au kuabudu mungu mwingine yeyote isipokuwa Mungu wao. Kwa hiyo ninaamuru kwamba watu wa taifa lolote au lugha yoyote watakaosema kitu chochote dhidi ya Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego wakatwe vipande vipande na nyumba zao zifanywe kuwa malundo ya kokoto, kwa maana hakuna mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.” Kisha mfalme akawapandisha vyeo Shadraki, Meshaki na Abednego katika jimbo la Babeli.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Danieli 3:19-30