Danieli 3:8-30
Danieli 3:8-30 NENO
Wakati huo baadhi ya Wakaldayo walijitokeza na kuwashtaki Wayahudi. Wakamwambia Mfalme Nebukadneza, “Ee mfalme, uishi milele! Ee mfalme, umetoa amri kwamba kila mmoja atakayesikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari, na aina zote za sauti za ala za uimbaji, lazima asujudu na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu, na kwamba yeyote ambaye hatasujudu na kuiabudu atatupwa saa hiyo hiyo ndani ya tanuru linalowaka moto. Lakini wako baadhi ya Wayahudi ambao umewaweka juu ya mambo ya jimbo la Babeli, yaani Shadraki, Meshaki na Abednego, ambao hawakujali wewe, ee mfalme. Hawaitumikii miungu yako wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.” Mfalme Nebukadneza, akiwa amekasirika na mwenye ghadhabu kali, akawaita Shadraki, Meshaki na Abednego. Hivyo watu hawa wakaletwa mbele ya mfalme, naye Nebukadneza akawauliza, “Je, ni kweli kwamba ninyi Shadraki, Meshaki na Abednego hamuitumikii miungu yangu wala kuiabudu sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? Basi wakati mtakaposikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari na aina zote za ala za uimbaji, kama mtakuwa tayari kusujudu na kuiabudu hiyo sanamu niliyoitengeneza, vyema sana. Lakini kama hamtaiabudu, mtatupwa saa hiyo hiyo ndani ya tanuru linalowaka moto. Naye ni mungu yupi ataweza kuwaokoa ninyi kutoka mkononi mwangu?” Shadraki, Meshaki na Abednego wakamjibu mfalme, “Ee Nebukadneza, hatuhitaji kujitetea mbele zako kuhusu jambo hili. Ikiwa tutatupwa ndani ya tanuru linalowaka moto, Mungu tunayemtumikia anaweza kutuokoa na moto, naye atatuokoa kutoka mkononi mwako, ee mfalme. Lakini hata ikiwa hatatuokoa, ee mfalme, tunataka ufahamu kwamba hatutaitumikia miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.” Ndipo Nebukadneza akawa na ghadhabu kali sana kwa Shadraki, Meshaki na Abednego, nayo nia yake ikabadilika kwao. Akaagiza tanuru lichochewe moto mara saba kuliko kawaida yake, na akawaamuru baadhi ya askari wake wenye nguvu zaidi katika jeshi lake kuwafunga Shadraki, Meshaki na Abednego, na kuwatupa ndani ya tanuru lililowaka moto. Hivyo watu hawa walifungwa na kutupwa ndani ya tanuru hilo wakiwa wamevaa majoho yao, suruali, vilemba, na nguo zao nyingine. Amri ya mfalme ilikuwa ya haraka sana na tanuru lilikuwa na moto mkali kiasi kwamba miali ya moto iliwaua wale askari waliowapeleka Shadraki, Meshaki na Abednego. Watu hawa watatu walianguka ndani ya tanuru hilo la moto wakiwa wamefungwa kwa uthabiti sana. Ndipo Mfalme Nebukadneza akashangaa, akainuka kwa haraka na kuwauliza washauri wake, “Je, hawakuwa watu watatu ambao tuliwafunga na kuwatupa ndani ya moto?” Washauri wakajibu, “Hakika, ee mfalme.” Mfalme akasema, “Tazama! Naona watu wanne wakitembeatembea ndani ya moto; hawajafungwa wala kudhurika, naye mtu yule wa nne anaonekana kama mwana wa miungu.” Ndipo Nebukadneza akaukaribia mdomo wa lile tanuru lililowaka moto na kuita kwa sauti kuu, “Shadraki, Meshaki na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, tokeni! Njooni hapa!” Ndipo Shadraki, Meshaki na Abednego wakatoka ndani ya moto. Nao maliwali, wasimamizi, watawala na washauri wa mfalme wakakusanyika kuwazunguka. Waliona kwamba moto haukudhuru miili yao, wala unywele wa vichwa vyao haukuungua, majoho yao hayakuungua, wala hawakuwa na harufu ya moto. Ndipo Nebukadneza akasema, “Ahimidiwe Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego, ambaye amemtuma malaika wake na kuwaokoa watumishi wake. Walimtumaini na kukaidi amri ya mfalme, nao wakawa tayari kufa kuliko kutumikia au kuabudu mungu mwingine yeyote isipokuwa Mungu wao. Kwa hiyo ninaamuru kwamba watu wa taifa lolote au lugha yoyote watakaosema kitu chochote dhidi ya Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego wakatwe vipande vipande, na nyumba zao zifanywe kuwa malundo ya kokoto, kwa maana hakuna mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.” Kisha mfalme akawapandisha vyeo Shadraki, Meshaki na Abednego katika jimbo la Babeli.