Danieli 3
3
Sanamu ya dhahabu na tanuru la moto
1Mfalme Nebukadneza alitengeneza sanamu ya dhahabu, yenye kimo cha dhiraa sitini#3:1 Dhiraa sitini ni sawa na mita 27., na upana wa dhiraa sita#3:1 Dhiraa sita ni sawa na mita 2.7., akaisimamisha kwenye tambarare ya Dura katika jimbo la Babeli. 2Kisha mfalme akaita wakuu, wasimamizi, watawala, washauri, watunza hazina, waamuzi, mahakimu, na maafisa wengine wote wa jimbo kuja kuizindua sanamu ambayo Mfalme Nebukadneza alikuwa ameisimamisha. 3Basi wakuu, wasimamizi, watawala, washauri, watunza hazina, waamuzi, mahakimu, na maafisa wengine wote wa jimbo wakakusanyika ili kuizindua sanamu ile Mfalme Nebukadneza alikuwa ameisimamisha, nao wakasimama mbele ya hiyo sanamu.
4Ndipo mpiga mbiu akatangaza kwa sauti kubwa, “Enyi watu wa makabila yote, na mataifa, na wa kila lugha, hili ndilo mnaloamriwa kulifanya: 5Mara mtakaposikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari, na aina zote za sauti za ala za uimbaji, lazima msujudu na kuabudu sanamu ya dhahabu ambayo Mfalme Nebukadneza ameisimamisha. 6Mtu ambaye hataanguka chini na kuiabudu sanamu hiyo, atatupwa saa hiyo hiyo ndani ya tanuru linalowaka moto.”
7Kwa hiyo, mara waliposikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari, na aina zote za sauti za ala za uimbaji, watu wa makabila yote, na mataifa, na wa kila lugha wakasujudu na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu ambayo Mfalme Nebukadneza alikuwa ameisimamisha.
8Wakati huo baadhi ya Wakaldayo walijitokeza na kuwashtaki Wayahudi. 9Wakamwambia Mfalme Nebukadneza, “Ee mfalme, uishi milele! 10Ee mfalme, umetoa amri kwamba kila mmoja atakayesikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari, na aina zote za sauti za ala za uimbaji, lazima asujudu na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu, 11na kwamba yeyote ambaye hatasujudu na kuiabudu atatupwa saa hiyo hiyo ndani ya tanuru linalowaka moto. 12Lakini wako baadhi ya Wayahudi ambao umewaweka juu ya mambo ya jimbo la Babeli, yaani Shadraki, Meshaki na Abednego, ambao hawakujali wewe, ee mfalme. Hawaitumikii miungu yako wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”
13Mfalme Nebukadneza, akiwa amekasirika na mwenye ghadhabu kali, akawaita Shadraki, Meshaki na Abednego. Hivyo watu hawa wakaletwa mbele ya mfalme, 14naye Nebukadneza akawauliza, “Je, ni kweli kwamba ninyi Shadraki, Meshaki na Abednego hamuitumikii miungu yangu wala kuiabudu sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? 15Basi wakati mtakaposikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari na aina zote za ala za uimbaji, kama mtakuwa tayari kusujudu na kuiabudu hiyo sanamu niliyoitengeneza, vyema sana. Lakini kama hamtaiabudu, mtatupwa saa hiyo hiyo ndani ya tanuru linalowaka moto. Naye ni mungu yupi ataweza kuwaokoa ninyi kutoka mkononi mwangu?”
16Shadraki, Meshaki na Abednego wakamjibu mfalme, “Ee Nebukadneza, hatuhitaji kujitetea mbele zako kuhusu jambo hili. 17Ikiwa tutatupwa ndani ya tanuru linalowaka moto, Mungu tunayemtumikia anaweza kutuokoa na moto, naye atatuokoa kutoka mkononi mwako, ee mfalme. 18Lakini hata ikiwa hatatuokoa, ee mfalme, tunataka ufahamu kwamba hatutaitumikia miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”
19Ndipo Nebukadneza akawa na ghadhabu kali sana kwa Shadraki, Meshaki na Abednego, nayo nia yake ikabadilika kwao. Akaagiza tanuru lichochewe moto mara saba kuliko kawaida yake, 20na akawaamuru baadhi ya askari wake wenye nguvu zaidi katika jeshi lake kuwafunga Shadraki, Meshaki na Abednego, na kuwatupa ndani ya tanuru lililowaka moto. 21Hivyo watu hawa walifungwa na kutupwa ndani ya tanuru hilo wakiwa wamevaa majoho yao, suruali, vilemba, na nguo zao nyingine. 22Amri ya mfalme ilikuwa ya haraka sana na tanuru lilikuwa na moto mkali kiasi kwamba miali ya moto iliwaua wale askari waliowapeleka Shadraki, Meshaki na Abednego. 23Watu hawa watatu walianguka ndani ya tanuru hilo la moto wakiwa wamefungwa kwa uthabiti sana.
24Ndipo Mfalme Nebukadneza akashangaa, akainuka kwa haraka na kuwauliza washauri wake, “Je, hawakuwa watu watatu ambao tuliwafunga na kuwatupa ndani ya moto?”
Washauri wakajibu, “Hakika, ee mfalme.”
25Mfalme akasema, “Tazama! Naona watu wanne wakitembeatembea ndani ya moto; hawajafungwa wala kudhurika, naye mtu yule wa nne anaonekana kama mwana wa miungu.”
26Ndipo Nebukadneza akaukaribia mdomo wa lile tanuru lililowaka moto na kuita kwa sauti kuu, “Shadraki, Meshaki na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, tokeni! Njooni hapa!”
Ndipo Shadraki, Meshaki na Abednego wakatoka ndani ya moto. 27Nao maliwali, wasimamizi, watawala na washauri wa mfalme wakakusanyika kuwazunguka. Waliona kwamba moto haukudhuru miili yao, wala unywele wa vichwa vyao haukuungua, majoho yao hayakuungua, wala hawakuwa na harufu ya moto.
28Ndipo Nebukadneza akasema, “Ahimidiwe Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego, ambaye amemtuma malaika wake na kuwaokoa watumishi wake. Walimtumaini na kukaidi amri ya mfalme, nao wakawa tayari kufa kuliko kutumikia au kuabudu mungu mwingine yeyote isipokuwa Mungu wao. 29Kwa hiyo ninaamuru kwamba watu wa taifa lolote au lugha yoyote watakaosema kitu chochote dhidi ya Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego wakatwe vipande vipande, na nyumba zao zifanywe kuwa malundo ya kokoto, kwa maana hakuna mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.”
30Kisha mfalme akawapandisha vyeo Shadraki, Meshaki na Abednego katika jimbo la Babeli.
Iliyochaguliwa sasa
Danieli 3: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.