Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 4:28-37

Danieli 4:28-37 NEN

Haya yote yalimpata Mfalme Nebukadneza. Miezi kumi na miwili baadaye, mfalme alipokuwa akitembea juu ya paa la jumba la kifalme la Babeli, alisema, “Je, huu si Babeli mji mkuu nilioujenga kama makao ya kifalme, kwa uwezo wangu mkubwa, na kwa ajili ya utukufu wa enzi yangu?” Maneno hayo yalikuwa bado katika midomo yake wakati sauti ilipokuja kutoka mbinguni, ikisema, “Mfalme Nebukadneza, hiki ndicho kilichoamriwa kwa ajili yako: Mamlaka yako ya ufalme yameondolewa kutoka kwako. Utafukuzwa mbali na wanadamu, ukaishi pamoja na wanyama pori, na utakula manyasi kama ngʼombe. Nyakati saba zitapita juu yako, mpaka utakapokubali kuwa Yeye Aliye Juu Sana ndiye anayetawala juu ya falme za wanadamu, naye humtawaza yeyote amtakaye.” Papo hapo yale yaliyokuwa yamesemwa kuhusu Nebukadneza yakatimia. Alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani kama ngʼombe. Mwili wake uliloweshwa kwa umande wa mbinguni mpaka nywele zake zikakua kama manyoya ya tai na kucha zake kama makucha ya ndege. Mwisho wa huo wakati, mimi Nebukadneza, niliinua macho yangu kuelekea mbinguni, nazo fahamu zangu zikanirudia. Ndipo nikamsifu Yeye Aliye Juu Sana, nikamheshimu na kumhimidi yeye aishiye milele. Utawala wake ni utawala wa milele; ufalme wake hudumu kutoka kizazi na kizazi. Mataifa yote ya dunia yanahesabiwa kuwa si kitu. Hufanya kama atakavyo kwa majeshi ya mbinguni, na kwa mataifa ya dunia. Hakuna anayeweza kuuzuia mkono wake au kumwambia, “Umefanya nini wewe?” Wakati huo huo fahamu zangu ziliponirudia, nikarudishiwa heshima yangu na fahari yangu kwa ajili ya utukufu wa ufalme wangu. Washauri wangu na wakuu wangu walikuja kunitafuta, nami nikarudishwa kwenye kiti changu cha ufalme hata nikawa mkuu kuliko mwanzoni. Basi mimi, Nebukadneza, humhimidi, na humtukuza na kumsifu Mfalme wa mbinguni, kwa sababu kila kitu afanyacho ni haki, na njia zake zote ni adili. Nao waendao kwa kiburi anaweza kuwashusha.