Danieli 6:16-28
Danieli 6:16-28 NEN
Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, na wakamtupa ndani ya tundu la simba. Mfalme akamwambia Danieli, “Mungu wako unayemtumikia daima na akuokoe!” Jiwe likaletwa na kuwekwa kwenye mdomo wa tundu, naye mfalme akalitia muhuri kwa pete yake mwenyewe pamoja na kwa pete za wakuu wake, ili hali ya Danieli isiweze kubadilishwa. Kisha mfalme akarudi kwenye jumba lake la kifalme, naye usiku kucha hakula chakula wala kutumia viburudisho alivyoletewa. Lakini hakuweza kulala. Asubuhi na mapema, mfalme akaondoka na kuharakisha kwenda kwenye tundu la simba. Wakati alipokaribia lile tundu, akamwita Danieli kwa sauti ya uchungu, “Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai! Je, Mungu wako unayemtumikia daima, ameweza kukuokoa kwa simba?” Danieli akajibu, “Ee mfalme, uishi milele! Mungu wangu alimtuma malaika wake, naye akafunga vinywa vya hawa simba. Hawajanidhuru, kwa sababu nilionekana sina hatia mbele zake. Wala kamwe sijafanya jambo lolote baya mbele yako, ee mfalme.” Mfalme akafurahi mno, naye akatoa amri Danieli atolewe kutoka kwa lile tundu. Danieli alipotolewa kutoka kwa lile tundu, hakukutwa na jeraha lolote, kwa sababu alikuwa amemtumaini Mungu wake. Kwa amri ya mfalme, wale watu waliokuwa wamemshtaki Danieli kwa uongo waliletwa na kutupwa ndani ya lile tundu la simba, pamoja na wake zao na watoto wao. Nao kabla hawajafika chini kwenye sakafu ya lile tundu, simba wakawakamata na kusaga mifupa yao yote. Kisha Mfalme Dario akawaandikia kabila zote za watu, mataifa, na watu wa kila lugha katika nchi yote: “Ninyi na mstawi sana! “Natoa amri hii, kwamba katika kila sehemu ya ufalme wangu, lazima watu wamwogope na kumheshimu Mungu wa Danieli. “Kwa maana yeye ni Mungu aliye hai, naye hudumu milele, ufalme wake hautaangamizwa, nao utawala wake hauna mwisho. Huponya na kuokoa; hufanya ishara na maajabu mbinguni na duniani. Amemwokoa Danieli kutoka nguvu za simba.” Hivyo Danieli akastawi wakati wa utawala wa Dario, na utawala wa Koreshi Mwajemi.