Kumbukumbu 27:11-26
Kumbukumbu 27:11-26 NENO
Siku ile ile Musa akawaagiza watu: Mtakapovuka Mto Yordani, makabila haya yatasimama juu ya Mlima Gerizimu kubariki watu: Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari, Yusufu na Benyamini. Makabila haya yatasimama juu ya Mlima Ebali kwa kutamka laana: Reubeni, Gadi, Asheri, Zabuloni, Dani na Naftali. Nao Walawi watawasomea watu wote wa Israeli kwa sauti kubwa: “Alaaniwe mtu afanyaye sanamu ya kuchonga au mwenye kusubu sanamu, kitu ambacho ni chukizo kwa Mwenyezi Mungu, kazi ya mikono ya fundi stadi, na kuisimamisha kwa siri.” Kisha watu wote watasema, “Amen!” “Alaaniwe mtu amdharauye baba yake na mama yake.” Kisha watu wote watasema, “Amen!” “Alaaniwe mtu asogezaye jiwe la mpaka wa jirani yake.” Kisha watu wote watasema, “Amen!” “Alaaniwe mtu ampotoshaye kipofu njiani.” Kisha watu wote watasema, “Amen!” “Alaaniwe mtu apotoshaye haki ya mgeni, yatima au mjane.” Kisha watu wote watasema, “Amen!” “Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na mke wa baba yake, kwa maana anadharau malazi ya baba yake.” Kisha watu wote watasema, “Amen!” “Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na mnyama yeyote.” Kisha watu wote watasema, “Amen!” “Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na dada yake, binti ya baba yake au binti ya mama yake.” Kisha watu wote watasema, “Amen!” “Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na mama mkwe wake.” Kisha watu wote watasema, “Amen!” “Alaaniwe mtu amuuaye jirani yake kwa siri.” Kisha watu wote watasema, “Amen!” “Alaaniwe mtu apokeaye rushwa ili kumuua mtu asiye na hatia.” Kisha watu wote watasema, “Amen!” “Alaaniwe mtu yule ambaye hatashikilia maneno ya sheria hii kwa kuyatekeleza.” Kisha watu wote watasema, “Amen!”