Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 28

28
Baraka za utiifu
(Walawi 26:3-13; Kumbukumbu 7:12-24)
1Ukimtii Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa ukamilifu na kufuata amri zake zote ninazokupa leo kwa makini, Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakuweka juu ya mataifa yote katika dunia. 2Baraka hizi zote zitakuja juu yako na kukupata, kama ukimtii Mwenyezi Mungu, Mungu wako:
3Utabarikiwa mjini na utabarikiwa mashambani.
4Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na mazao ya nchi yako na mifugo wako wachanga, yaani ndama wa makundi yako ya ng’ombe, na wana-kondoo wa makundi yako.
5Kapu lako na vyombo vyako vya kukandia vitabarikiwa.
6Utabarikiwa uingiapo na utabarikiwa utokapo.
7Mwenyezi Mungu atasababisha adui wainukao dhidi yako kushindwa mbele yako. Watakujia kwa njia moja lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba.
8Mwenyezi Mungu ataagiza baraka juu ya ghala zako na juu ya kila kitu utakachogusa kwa mkono wako. Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakubariki katika nchi anayokupa.
9Mwenyezi Mungu atakufanya kuwa taifa lake takatifu, kama alivyokuahidi kwa kiapo, ukishika maagizo ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na kwenda katika njia zake. 10Kisha mataifa yote ya dunia wataona kuwa unaitwa kwa jina la Mwenyezi Mungu, nao watakuogopa. 11Mwenyezi Mungu atakupa kustawi kwa wingi, katika tunda la uzao wa tumbo lako, katika wanyama wachanga wa mifugo yako na katika mazao ya ardhi yako, katika nchi aliyowaapia baba zako kukupa wewe.
12Mwenyezi Mungu atafungua mbingu, ghala zake za baraka, kukupa mvua kwa majira yake na kubariki kazi zako zote za mikono yako. Utakopesha mataifa mengi lakini hutakopa kwa yeyote. 13Mwenyezi Mungu atakufanya kichwa, wala si mkia. Kama utazingatia maagizo ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ninayokupa siku hii ya leo na kuyafuata kwa makini, daima utakuwa juu, kamwe hutakuwa chini. 14Usihalifu amri zangu zozote ninazokupa leo, kwa kwenda kuume au kushoto, kwa kufuata miungu mingine na kuitumikia.
Laana kwa kutokutii
(Walawi 26:14-46)
15Lakini kama hutamtii Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na kuzishika kwa makini amri zake zote na maagizo ninayokupa leo, laana hizi zote zitakuja juu yako na kukupata:
16Utalaaniwa mjini na utalaaniwa mashambani.
17Kapu lako na chombo chako cha kukandia kitalaaniwa.
18Uzao wa tumbo lako utalaaniwa, mazao ya ardhi yako, ndama wa makundi yako ya ng’ombe na wana-kondoo wa makundi yako.
19Utalaaniwa uingiapo na utokapo.
20Mwenyezi Mungu ataleta laana juu yako, fadhaa na kukaripiwa katika kila kitu unachokigusa kwa mkono wako, hadi uwe umeharibiwa na kuangamizwa ghafula kwa ajili ya maovu uliyoyafanya kwa kumwacha yeye. 21Mwenyezi Mungu atakupiga kwa magonjwa hadi akuangamize kutoka nchi unayoingia kuimiliki. 22Mwenyezi Mungu atakupiga kwa magonjwa ya kudhoofisha, kwa homa na kuwashwa, hari na kwa ukame, kutu na kuwa na uchungu ambavyo vitakupiga hadi uangamie.
23Anga juu yako itakuwa shaba, na ardhi chini yako itakuwa chuma. 24Mwenyezi Mungu atafanya mvua ya nchi yako kuwa mavumbi na mchanga; vitakujia kutoka angani hadi uangamie.
25Mwenyezi Mungu atakufanya ushindwe mbele ya adui zako. Utawajia kwa njia moja lakini utawakimbia mbele yao kwa njia saba, nawe utakuwa kitu cha kuchukiza kwa falme zote za dunia. 26Mizoga yenu itakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi, wala hapatakuwa na mtu yeyote wa kuwafukuza. 27Mwenyezi Mungu atakupiga kwa majipu ya Misri na kwa vidonda vinavyotoa usaha na kuwashwa, ambavyo huwezi kuponywa. 28Mwenyezi Mungu atakupiga kwa wazimu, upofu na kuchanganyikiwa kwa akili. 29Adhuhuri utapapasapapasa kama kipofu gizani. Hutafanikiwa katika lolote ufanyalo; siku baada ya siku utadhulumiwa na kunyang’anywa, wala hakuna yeyote atakayekuokoa.
30Utaposa mke, lakini mtu mwingine atakutana naye kimwili. Utajenga nyumba, lakini hutaishi ndani yake. Utapanda shamba la mizabibu, lakini hutakula matunda yake. 31Ng’ombe wako atachinjwa mbele ya macho yako lakini hutakula nyama yake. Punda wako atachukuliwa kwa nguvu kutoka kwako wala hatarudishwa. Kondoo wako watapewa adui zako, wala hakuna mtu yeyote wa kuwaokoa. 32Wanao wa kiume na wa kike watatolewa kwa mataifa mengine, nawe utayachosha macho yako ukiwatazamia siku baada ya siku, hutakuwa na nguvu kuinua mkono. 33Taifa usilolijua watakula mazao ya nchi yako na taabu ya kazi yako, hutakuwa na chochote, bali kuonewa kikatili siku zako zote. 34Vitu utakavyoviona kwa macho yako vitakufanya wazimu. 35Mwenyezi Mungu atayapiga magoti yako na miguu yako kwa majipu yenye maumivu makali yasiyoponyeka, yakienea kutoka nyayo za miguu yako hadi utosini.
36Mwenyezi Mungu atakupeleka wewe na mfalme uliyemweka juu yako uende kwenye taifa ambalo hukulijua wewe wala baba zako. Huko utaabudu miungu mingine, miungu ya miti na mawe. 37Utakuwa kitu cha kuchukiza, tena kitu cha kudharauliwa na kudhihakiwa kwa mataifa yote huko Mwenyezi Mungu atakakokupeleka.
38Utapanda mbegu nyingi katika shamba lakini utavuna haba, kwa sababu nzige watazila. 39Utapanda mashamba ya mizabibu na kuyapalilia, lakini hutakunywa divai yake wala hutakusanya zabibu, kwa sababu wadudu watazila. 40Utakuwa na mizeituni katika nchi yako yote, lakini hutatumia hayo mafuta yake, kwa sababu zeituni zitapukutika. 41Utakuwa na wana wa kiume na wa kike, lakini hawatakuwa nawe, kwa sababu watachukuliwa mateka. 42Makundi ya nzige yatavamia miti yako yote na mazao ya nchi yako.
43Mgeni anayeishi miongoni mwako atazidi kuinuka juu yako, lakini wewe utaendelea kushuka chini zaidi. 44Yeye atakukopesha, lakini wewe hutamkopesha. Yeye atakuwa kichwa, lakini wewe utakuwa mkia.
45Laana hizi zote zitakuja juu yako. Zitakufuatia na kukupata hadi uangamizwe, kwa sababu hukumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na kuzishika amri zake na maagizo yake aliyokupa. 46Zitakuwa ishara na ajabu kwako na kwa wazao wako milele. 47Kwa sababu hukumtumikia Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa furaha na kwa moyo wakati wa kufanikiwa kwako, 48kwa hiyo katika njaa na kiu, katika uchi na umaskini wa kutisha, utawatumikia adui ambao Mwenyezi Mungu atawatuma dhidi yako. Yeye ataweka nira ya chuma shingoni mwako hadi amekwisha kukuangamiza.
49Mwenyezi Mungu ataleta taifa dhidi yako kutoka mbali, kutoka miisho ya dunia, kama tai ashukavyo chini, taifa ambalo hutaijua lugha yake, 50taifa lenye uso mkali lisilojali wazee wala kuwahurumia vijana. 51Watakula wadogo wa mifugo yako na mazao ya nchi yako hadi umeangamia. Hawatakuachia nafaka, divai mpya au mafuta, wala ndama wowote wa kundi lako au wana-kondoo wa kundi lako hadi umekuwa magofu. 52Nao wataizingira miji yote katika nchi yako, hata kuta ndefu za ngome ambazo unazitegemea zimeanguka. Watazingira miji yote katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wako, anakupa.
53Utakula uzao wa tumbo lako, nyama ya wana wako wa kiume na wa kike, ambao Mwenyezi Mungu, Mungu wako, amekupa, kwa sababu ya mateso yale adui zako watakayokuletea wakati wa kukuzingira. 54Hata yule mtu muungwana sana na makini miongoni mwako hatakuwa na huruma kwa ndugu yake mwenyewe au kwa mke ampendaye au watoto wake waliosalia, 55naye hatampa hata mmoja wao nyama ya watoto wake ambao anawala. Kwa kuwa hakuna kitu kingine kilichosalia kwake katika mazingirwa makali ambayo adui yako watakuletea kwa miji yako yote. 56Mwanamke ambaye ni muungwana sana na makini miongoni mwako, yaani ambaye ni makini sana na muungwana kiasi kwamba asingethubutu kugusa ardhi kwa wayo wa mguu wake, yeye atakuwa mchoyo kwa mume ampendaye na mwanawe mwenyewe au binti yake, 57kondoo wa nyuma kutoka tumbo lake na watoto anaowazaa. Kwa kuwa anakusudia kuwala kwa siri wakati wa kuzingirwa na katika taabu zile adui yako atazileta juu yako na miji yako.
58Kama hutazingatia maneno yote ya sheria hii, ambayo yameandikwa katika kitabu hiki na kama hutalicha hili jina la fahari na la kutisha, yaani la Mwenyezi Mungu, Mungu wako, 59Mwenyezi Mungu ataleta mapigo ya kutisha juu yako na kwa wazao wako, maafa makali na ya kudumu, magonjwa mazito na ya kudumu. 60Atakuletea juu yako magonjwa yote ya Misri yale uliyoyaogopa, nayo yataambatana nawe. 61Pia Mwenyezi Mungu atakuletea kila aina ya ugonjwa na maafa ambayo hayakuandikwa humu katika kitabu hiki cha sheria, hadi utakapokuwa umeangamizwa. 62Ninyi ambao mlikuwa wengi kama nyota za angani mtaachwa wachache tu, kwa sababu hamkumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. 63Kama ilivyompendeza Mwenyezi Mungu kuwafanya ninyi mstawi na kuongezeka kwa idadi, ndivyo itakavyompendeza kuwaharibu na kuwaangamiza ninyi. Mtang’olewa kutoka nchi mnayoiingia kuimiliki.
64Kisha Mwenyezi Mungu atawatawanya miongoni mwa mataifa yote, kutoka mwisho mmoja wa dunia hadi mwingine. Huko mtaabudu miungu mingine, miungu ya miti na ya mawe, ambayo ninyi wala baba zenu hamkuijua. 65Miongoni mwa mataifa hayo hamtapata amani, wala mahali pa kupumzisha wayo wa mguu wenu. Huko Mwenyezi Mungu atawapa mahangaiko ya mawazo, macho yaliyochoka kwa kungojea na moyo uliokata tamaa. 66Utaishi katika mahangaiko siku zote, ukiwa umejaa hofu usiku na mchana, wala hutakuwa kamwe na uhakika wa maisha yako. 67Asubuhi utasema hivi, “Laiti ingekuwa jioni!” Jioni utasema, “Laiti ingekuwa asubuhi,” kwa sababu ya hofu ile itakayojaza moyo wako na vitu vile macho yako yatakavyoviona. 68Mwenyezi Mungu atawarudisha tena Misri kwa meli, safari niliyosema kamwe hamngeenda tena. Huko mtajiuza ninyi wenyewe kwa adui zenu kama watumwa wa kiume na wa kike, lakini hakuna yeyote atakayewanunua.

Iliyochaguliwa sasa

Kumbukumbu 28: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia