29
Kufanya upya agano
1Haya ndio maneno ya agano Mwenyezi Mungu alilomwagiza Musa kufanya na Waisraeli huko Moabu, yakiwa nyongeza ya agano alilofanya nao huko Horebu.
2Musa akawaita Waisraeli wote, akawaambia:
Macho yenu yameona yale yote Mwenyezi Mungu aliyofanya kwa Mfalme Farao huko Misri, kwa maafisa wake wote na kwa nchi yake yote. 3Kwa macho yenu wenyewe mliona yale majaribu makubwa, ishara zile za miujiza na maajabu makubwa. 4Lakini hadi leo Mwenyezi Mungu hajawapa akili ya kuelewa au macho yanayoona au masikio yanayosikia. 5Kwa muda wa miaka arobaini niliyowaongoza jangwani, nguo zenu hazikuchakaa, wala viatu miguuni mwenu. 6Hamkula mkate na hamkunywa divai wala kileo chochote. Nilifanya hivi ili mpate kujua kuwa mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
7Mlipofika mahali hapa, Sihoni mfalme wa Heshboni na Ogu mfalme wa Bashani walikuja kupigana dhidi yetu, lakini tuliwashinda. 8Tuliichukua nchi yao na kuwapa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase kama urithi wao.
9Zingatieni masharti ya agano hili, ili mweze kustawi katika kila kitu mnachofanya. 10Ninyi nyote leo mnasimama mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu; mkiwa viongozi na wakuu wenu, wazee na maafisa wenu, na wanaume wengine wote wa Israeli, 11pamoja na watoto wenu, wake zenu na pia wageni wanaoishi katika kambi zenu wanaowapasulia kuni na kuwachotea maji. 12Mnasimama hapa ili kufanya agano na Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, agano ambalo Mungu analifanya nanyi siku hii ya leo na kulitia muhuri kwa kiapo, 13kuwathibitisha ninyi siku hii ya leo kama taifa lake, ili aweze kuwa Mungu wenu kama alivyowaahidi na kama alivyowaapia baba zenu Ibrahimu, Isaka na Yakobo. 14Ninafanya agano hili pamoja na kiapo chake, sio na ninyi tu 15mnaosimama hapa na sisi leo mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, bali pia pamoja na wale ambao hawapo hapa leo.
16Ninyi wenyewe mnajua jinsi tulivyoishi nchini Misri na jinsi tulivyopita katikati ya nchi hadi tukafika hapa. 17Mliona miongoni mwao machukizo yao, na sanamu za miti na mawe, za fedha na dhahabu. 18Hakikisheni kwamba hakuna mwanaume au mwanamke, ukoo au kabila miongoni mwenu leo ambalo moyo wake utamwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kwenda kuabudu miungu ya mataifa hayo. Hakikisheni hakuna mzizi miongoni mwenu unaotoa sumu chungu ya namna hii.
19Mtu wa namna hii asikiapo maneno ya kiapo hiki, hujibariki mwenyewe, na kisha hufikiri, “Nitakuwa salama, hata nikiendelea kuifuata njia yangu mwenyewe.” Hili litaleta maafa juu ya nchi iliyoneshewa sawasawa na nchi kame. 20Mwenyezi Mungu kamwe hatakuwa radhi kumsamehe, ghadhabu na wivu wa Mungu vitawaka dhidi ya mtu huyo. Laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki zitamwangukia na Mwenyezi Mungu atafuta jina lake chini ya mbingu. 21Mwenyezi Mungu atamtwaa peke yake kutoka makabila ya Israeli kwa maangamizi, kulingana na laana zote za agano zilizoandikwa kwenye Kitabu hiki cha Torati.
22Watoto wako watakaofuata baada yako katika vizazi vya baadaye na wageni ambao watakuja kutoka nchi za mbali, wataona maafa, yaliyoipata nchi na magonjwa ambayo Mwenyezi Mungu aliyaleta juu yake. 23Nchi yote itakuwa jaa linaloungua la chumvi na kiberiti: hakutakuwa kilichopandwa, hakutakuwa kinachochipua, wala hakutakuwa na mimea inayoota juu yake. Itakuwa kama maangamizi ya Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu, ambazo Mwenyezi Mungu aliangamiza kwa hasira kali. 24Mataifa yote yatauliza: “Kwa nini Mwenyezi Mungu ameifanya hivi nchi hii? Kwa nini hasira hii kali ikawaka?”
25Na jibu litakuwa: “Ni kwa sababu watu hawa waliacha agano la Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, agano alilofanya nao alipowatoa katika nchi ya Misri. 26Walienda zao na kuabudu miungu mingine na kuisujudia, miungu wasioijua, miungu ambayo Mungu hakuwapa. 27Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi ya nchi hii, hivyo Mungu akaleta juu yake laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki. 28Katika hasira kali na katika ghadhabu kuu Mwenyezi Mungu aliwang’oa kutoka nchi yao na kuwasukumia katika nchi nyingine, kama ilivyo sasa.”
29Mambo ya siri ni ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, bali yaliyofunuliwa ni yetu na watoto wetu milele, ili tuweze kuyafanya maneno yote ya sheria hii.