Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 30

30
Mafanikio baada ya kumgeukia Mwenyezi Mungu
1Baraka hizi zote pamoja na laana nilizoziweka mbele yako zitakapokujia, nawe ukazitafakari moyoni popote Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakapokutawanya miongoni mwa mataifa, 2hapo wewe na watoto wako mtakapomrudia Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na kumtii kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote kulingana na kila kitu ninachokuamuru leo, 3ndipo Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakapokurudisha kutoka utumwani na kukuhurumia, naye atakukusanya tena kutoka mataifa yote kule alikutawanya. 4Hata kama umefukuziwa katika nchi ya mbali kiasi gani chini ya mbingu, kutoka huko Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakukusanya na kukurudisha. 5Yeye Mwenyezi Mungu atakurudisha katika nchi iliyokuwa mali ya baba zako, nawe utaimiliki. Naye atakufanya ufanikiwe sana na kukuzidisha kwa idadi kuliko baba zako. 6Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ataitahiri mioyo yenu na mioyo ya wazao wenu ili mweze kumpenda kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote ukaishi. 7Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ataweka laana hizi zote juu ya adui zako ambao wanakuchukia na kukutesa. 8Utamtii tena Mwenyezi Mungu na kuzishika amri zake zote ninazokupa leo. 9Ndipo Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakapokufanikisha sana katika kazi zote za mikono yako na katika uzao wa tumbo lako, wadogo wa mifugo yako na mazao ya nchi yako. Mwenyezi Mungu atakufurahia tena na kukufanikisha, kama alivyowafurahia baba zako, 10kama utamtii Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na kuzishika amri zake na maagizo yake ambayo yameandikwa katika Kitabu hiki cha Torati, na kumgeukia Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote.
Uzima na Mauti
11Ninachokuagiza leo sio kigumu sana kwako au usichokiweza. 12Hakiko juu mbinguni, ili uulize, “Ni nani atakayepanda mbinguni kukileta na kututangazia ili tuweze kutii?” 13Wala hakiko ng’ambo ya bahari, ili uulize, “Ni nani atakayevuka bahari kwenda kukichukua na kututangazia ili tupate kutii?” 14La hasha! Lile neno liko karibu sana nawe; liko kinywani mwako na ndani ya moyo wako ili uweze kulitii.
15Tazama, naweka mbele yako leo uzima na mafanikio, mauti na maangamizi. 16Ninakuamuru leo kwamba umpende Mwenyezi Mungu, Mungu wako, utembee katika njia zake, na kutunza maagizo yake, amri na sheria zake; ndipo utakapoishi na kuongezeka, naye Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakubariki katika nchi unayoingia kuimiliki.
17Lakini kama moyo wako ukigeukia mbali ukawa huna utii, kama umevutwa kuisujudia miungu mingine na kuiabudu, 18nakutangazia siku ya leo kwamba hakika utaangamizwa. Hutaishi maisha marefu katika nchi unayovuka Yordani kuiingia na kuimiliki.
19Leo ninaziita mbingu na nchi kama mashahidi dhidi yako kwamba nimeweka mbele yako uzima na mauti, baraka na laana. Basi sasa chagueni uzima, ili wewe na watoto wako mpate kuishi, 20na ili upate kumpenda Mwenyezi Mungu, Mungu wako, uisikilize sauti yake na kuambatana naye. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye uzima wako, na atakupa wingi wa siku ili upate kuishi katika nchi aliyoapa kuwapa baba zako Ibrahimu, Isaka na Yakobo.

Iliyochaguliwa sasa

Kumbukumbu 30: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia